πŸ“Œ Asisitiza umoja na ushirikiano Arusha

πŸ“Œ Awataka Watanzania kuenzi Muungano

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kuishi kwa upendo na kushirikiana kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Amesema katika kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano ambapo amewahimiza Watanzania kukumbuka kuwa kuwa Mwl. Julius Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume waliunganisha Tanganyika na Zanzibar katika misingi ya umoja, amani, ushirikiano na kuheshimiana hivyo, muhimu kuendeleza misingi hiyo ili kuenzi Muungano.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 26, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Soko la Kilombero, Wilaya ya Arusha Mjini, Mkoa wa Arusha.

β€œ Arusha mfanye kazi kwa kushirikiana, muijenge Arusha yenu mkumbuke kwenye nafasi zetu za uongozi mjue kesho hamtakuwepo mtaondoka, kila mahala ulipo acha alama njema itakayo kumbukwa na wengine. Sisi tuliopo leo tutakumbukwa kwa lipi, iwe changamoto tunapokumbuka miaka 61 ya Muungano tujue ni alama gani tutaacha kwa watoto wetu,” amesema Dk. Biteko.

Amesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2025 Watanzania waishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana na kuwa wamoja kwa kuchagua viongozi wanaoweza kuwasilisha ajenda zao kwa wananchi.

β€œ Hicho ndicho kiwe kipimo na viongozi tusitumie tofauti zetu kutafuta kura, usiende kanisani au msikitini kwako kutumia uhalali watofauti zetu kutafuta kura asitokee yeyote kufanya hivyo tuuenzi Muungano na Rais Samia ameapa kuulinda Muungano huu kwa wivu mkubwa,” amesema Dk. Biteko.

Dkt. Biteko amebainisha Watanzania wasiruhusu Taifa kugawanyika kwa sababu yoyote ile wakumbuke kuwa kama hakuna amani hakuna biashara wala maendeleo yanayoweza kufanyika.

Pamoja na hayo, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ndani ya kipindi cha miaka minne, imetekeleza miradi mingi na kusimamia sera na mikakati mbalimbali ili kuuletea maendeleo Mkoa wa Arusha huku akitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni kuboresha miundombinu ya barabara, ambayo inaiunganisha Arusha na mikoa na maeneo yote ya kimkakati. Kwa mfano, Barabara Arusha- Namanga –ambayo inakwenda hadi Nairobi nchini Kenya.

Hatua nyingine ni kuweka Sera na Mipango mbalimbali ya kuiendeleza Arusha kimkakati. Kwa mfano, kuwa mwenyeji wa Makao Makuu ya EAC pamoja na Taasisi zake nyingine. Pamoja na kuiendeleza Arusha kuwa mwenyeji wa Taasisi nyingi za Kimataifa kwa sasa na kwa kipindi cha baadaye. Kwa mfano Chuo cha ESAMI, Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu pamoja na Taasisi nyingine.

Fauka ya hayo Dkt. Biteko amelipongeza Shirika la Umeme – Tanzania kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya umeme na kusema kuwa Serikali itahakikisha inafikisha huduma ya umeme kwa wananchi wote.
Kuhusu nishati safi ya kupikia Dkt. Biteko amegawa mitungi 500 ya gesi kwa baba lishe na mama lishe kwa lengo la kuwapa hamasa wanachi ili kuondokana na matumizi ya nishati isiyo safi. Huku akiwataka kuwa mabalozi wema wa nishati hiyo kwa jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema katika awamu ya kwanza Mkoa huo umepokea mitungi ya gesi 1,000 na majiko kwa ajili ya kusambaza kwa mama na baba lishe mkoani humo.

Ameongeza kuwa Serikali ina mpango wa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kwa kutumia Mfuko maalum wenye fedha shilingi bilioni 10 na wamemuomba Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima azindue Mfuko huo mkoani humo ili kutoa fursa pia ya wafanyabiashara wa mkoa huo kunufaika.

Vilevile, amesema Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuuletea maendeleo Mkoa huo kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kukuza uchumi wa nchi sambamba na kuimarisha sekta ya utalii kwa kujenga barabara mpya ya bypass yenye urefu wa km 70, reli ya kisasa kutoka Dar es salaam hadi Tanga, bandari ya nchi kavu yenye uwezo wa kuhifadhi magari 600.

Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Mrisho Gambo amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia mradi mkubwa wa maji na kuwaomba AUWSA kusaidia kuboresha ufungaji wa mita za maji kwa wananchi hasa zilizo mbali na makazi yao.

Aidha, amesema katika upande wa sekondari Rais Samia amejenga shule mpya za sekondari tano na shule mpya za msingi. Pia ameomba wanafunzi wanaofaulu wapangiwe shule hizo kwa kuzingatia maeneo wanayoishi.

β€œTunamshukuru pia Rais Samia kwa kutujengea uwanja wa mpira unaogharimu shilingi bilioni 286, barabara za lami na viwanja vipya vitano vidogo vya michezo,” amesema Mhe. Gambo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha – AUWSA, Mhandisi Justine Rujomba akitoa taarifa ya mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha amesema kuwa mradi huo umegharimu shilingi bilioni 520 ikiwa ni fedha za Serikali na mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa sasa unazalisha maji zaidi ya lita milioni 200 ambapo mahitaji ni lita milioni 139.

Licha ya mradi huo kufanikiwa kupita lengo la upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi kama lilivyoelezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Mhandisi Rujomba ametaja faida za mradi huo kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya wateja hadi kufikia 100,000, kuongezeka kwa uwezo wa kutibu maji taka na kununua mtambo wa kupima utendaji kazi wa dira za maji.

β€œKupitia mradi huu wakandarasi wameweza kununua vifaa kwenye soko la ndani vya gharama ya shilingi bilioni 150 hivyo umesaidia kukuza uchumi, pia tumepata ajira a watu 2,000 ikiwemo wanawake , tumeweza kujenga ofisi za kanda ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, na tuna uwezo wa kuhifadhi maji zaidi ya nane hata kama kuna matengenezo ,” amesema Mhandisi Rujomba.

Naye, Meneja Mradi Upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Njiro kilichoongezwa transforma yenye uwezo wa MVA 90 kufanya kituo kuwa na uwezo wa MVA 210, Mhandisi Japhari Msuya ametaja faida za kukamilika kwa mradi huo kuwa ni kutaimarisha upatikanaji wa umeme kwenye mikoa ya kanda ya kaskazini na kuendelea kufungua fursa za kiuchumi kwenye mikoa ya kanda ya kaskazini na kuimarisha sekta ya utalii, viwanda na biashara.

Akiwasilisha salamu za Muungano, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mratibu wa Muungano, Bw. Tumsifu Mwasamale amesema kuwa kwa mwaka huu 2025 ilielekezwa kuwa sherehe hizo zifanyike kwa wananchi na hivyo kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa uratibu na maandalizi mazuri ya sherehe hizo za Muungano.

Dkt. Biteko amehitimisha ziara yake siku tano mkoani humo kwa kutembelea Wilaya za Monduli, Longido, Aumeru na Arusha Mjini ambako amekagua na kuzindua miradi kutembelea, kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo, kupanda miti miti ya kumbukumbu na kuhutubia wananchi mikutano ya hadhara ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.