Na Lookman Miraji

Kwa huu 2024 taifa la Zambia limetimiza miaka 60 ya kuwa taifa huru linalojiongoza lenyewe kupitia mfumo wake wa kikatiba.

Rejea historia ya taifa la Zambia inatueleza kuwa taifa hilo lilijitwalia uhuru wake mnamo oktoba 24 ,1964 kutoka katika utawala wa waingereza kufuatia jitihada kubwa za kudai uhuru zilizoongozwa na kiongozi wa taifa hilo Hayati Kenneth Kaunda.

Hayati Kenneth Kaunda anatajwa na kufahamika zaidi kama muasisi wa taifa la Zambia kwa jitihada kubwa alizozifanya kwa watu wa rhodesia kaskazini kuhakikisha linapata uhuru wake wa kujiongoza kisiasa.

Kenneth Kaunda alizaliwa Aprili 28, 1924 katika kijiji cha Chinsali nchini Zambia. Hayati Kaunda aliongoza Zambia kama rais wa kwanza wa taifa hilo kwa kipindi cha miaka 27, kuanzia mwaka 1964 mpaka mwaka 1991.

Mahusiano kati ya taifa la Zambia na Tanzania yamekuwepo kwa muda mrefu ambapo urafiki kati ya waasisi wa mataifa hayo mawilli Mwalimu Julius Nyerere na Kenneth Kaunda ni hoja mama yenye kuthibitisha uhusiano huo.

Ikiwa taifa hilo la Zambia likiadhimisha kutimia kwa miaka 60 uhuru linajivunia urafiki uliopo kati yao na Tanzania.

Akiongoza shughuli za maadhimisho hayo ya kutimia kwa miaka 60 ya Uhuru wa Zambia balozi wa Zambia nchini Tanzania, Mathews Jere ameelezea kwa ukubwa zaidi uhusiano kati ya Zambia na Tanzania ulivyo na kuitaja miradi mbalimbali mikubwa inayozinufaisha nchi mbili ambapo ukiwemo mradi wa reli ya TAZARA, bomba la mafuta, ziwa Tanganyika pamoja na sekta ya usafiri wa anga.

“Tanzania na Zambia hawajaunganishwa tu na mipaka bali tunaungana kwa njia nyingi ambazo miongoni mwake ni kupitia muungano wa reli iliyojengwa kati ya Dar es salaam na kapirimposhi, tumeunganishwa pia na bomba la mafuta (TAZAMA) ambalo kiukweli linatusaidia kupunguza gharama za mafuta nchini Zambia.”

“Na zaidi pia kwa upande wa anga sote tunajua kuwa Air Tanzania na Zambian airways zinatusaidia kurahisisha usafiri kwa watu wetu kusafiri kati ya nchi hizi mbili. Na hata pia kwa maji tumeunganishwa ambapo pia tunachangia mpaka kupitia ziwa Tanganyika, kwahivyo hivi ndivyo namna kwanini mahusiano yetu ni makubwa.”

Aidha Balozi Jere pia ameongeza juu ya mipango ya serikali za nchi hizo mbili kuona ni namna gani zitaweza kushirikiana na kuleta mageuzi katika sekta ya biashara ambapo ameelezea vipaumbele ambavyo tayari vimeshajadiliwa na wakuu wa nchi hizo mbili na kusema lengo kuu ni kukuza uchumi wa biashara katika mataifa hayo.

“Ujumbe kutoka kwa rais wa Zambia, amekuwa akiongelea kuwa tunahitaji kuwekeza katika biashara kati ya haya mawili. Ukiangalia bidhaa tunazozitoa na kuziingiza kutoka mabara mengine utagundua tunatumia gharama kubwa za fedha na tukisema tuangalie mchango wa thamani kati ya mataifa yetu mawili maana yake pesa itabaki nasi hapa Afrika kuliko kutoa fursa kwa mataifa mengine.”

“Kwahiyo mpango uliowekwa kati ya wakuu hawa wawili wa nchi hizi ni kwamba sasa tugeukie katika biashara.


Na kwa kutambua hilo tayari tumeweka kituo kimoja cha biashara kati ya mataifa yetu kilichopo Nakonde ili kutengeneza mazingira rahisi kwa wafanyabiashara kusafirisha biashara zao. Kama haitoshi tumetoa tathmini juu ya bidhaa ambazo watu wanaweza kuuza na kununua katika nchi hizi mbili hivyo ndivyo namna tunatakiwa kwenda tunahitaji kuwasaidia i u wetu kurahisisha biashara kati ya mataifa yetu mawili.” Aliongeza balozi Jere.

Kwa upande mwingine pia salamu za pongezi za miaka 60 ya uhuru wa Zambia ziliwasilishwa na waziri wa nchi, ikulu ya Zanzibar, Mhe: Ali Suleiman Ameir ambae kupitia hotuba yake aliyoisoma amesema kuwa maadhimisho hayo ni wakati mwafaka wa kutafakari mafanikio ambayo serikali ya Zambia imeyapata tangu 1964 na kukiri kuwa maendeleo ya taifa hilo ni ushuhuda wa uamuzi na uthabiti wa bidii ya watu wa taifa hilo.

“Maadhimisho haya ya miaka 60 ya uhuru wa Zambia ni wakati mwafaka wa kutafakari mafanikio ambayo serikali ya Zambia imeyapata tangu mwaka 1964. Katika suala hili nikitafakari safari mliyoifanya ,nina hakika nyote mtakubaliana nami kwamba Zambia imepiga hatua kubwa sana katika nyanja mbalimbali, zikiwemo siasa, uchumi, biashara, miundombinu,na maendeleo ya kijamii. Maendeleo hayo ni ushuhuda wa uamuzi, uthabiti na bidii ya watu Zambia. ” Alisema.