NCAA yawezesha kina mama wajasiriamali
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeanzishwa kisheria kama eneo la matumizi mseto ya ardhi ikiwa na dhima tatu kuu. Dhima hizo ni Uhifadhi wa maliasili katika Eneo la Hifadhi; Kuendeleza wenyeji na shughuli zao za ufugaji; na Kuendeleza utalii. Hii imekuwa dira ya Mamlaka hii tangu ilipoanzishwa miaka 60 iliyopita.
Wengi wanapozungumzia Ngorongoro huangalia zaidi uhifadhi na utalii. Wanasahau eneo muhimu kabisa la namna NCAA inavyotekeleza kwa vitendo dhima ya uendelezaji wa shughuli za wenyeji ikiwa ni pamoja na ufugaji.
Jamii zinazoishi ndani na kando ya eneo la NCAA zimekuwa zikinufaika na uwepo wa Mamlaka hii kwa kuiwezesha kwenye nyanja mbalimbali.
Makumbusho ya Olduvai Gorge – mahali ambako ndiko kwenye chimbuko la binadamu – imekuwa kivutio kikuu cha utalii. Idadi ya watalii inaongezeka kwa kasi. Hatua hii imekuja baada ya kazi kubwa ya ujenzi wa majengo na miundombinu ya kisasa.
Wingi wa wageni katika eneo hili kumeifanya NCAA ibuni njia nyingine ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa NCAA, Bashiru Nchila, anasema: “Katika Makumbusho ya Olduvai kuna wageni wengi wanafika pale. Kwenye miundombinu mipya iliyojengwa hapa ni pamoja na Jengo la Maendeleo. Hili ni mahususi kwa ajili ya wajasiriamali wakazi wa humu ndani ya NCCA na vijiji jirani. Hapa wanauza vitu vya urembo na vifaa vingine. Mradi umeanza karibuni, lakini tayari umeshaanza kuonyesha mafanikio makubwa.”
Kinachofanywa ni kwa kina mama wajasiriamali vijijini hutengeneza vitu hivyo na kisha huvikusanya pamoja na kuwapa wale waliowateua kusimamia uuzaji.
Kwenye duka la jamii ya Wadatoga, anayesimamia duka ni Udagwason Gidabaso (21), anayetoka katika Kijiji cha Qangded, Mang’ora, wilayani Karatu. Huyu ni binti aliyesoma na kuishia kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Tumaini. Alikwama kuendelea na masomo baada ya mfadhili wake kufariki dunia.
“Alipofariki dunia ikabidi nibaki nyumbani, lakini nikaanza kufuatili historia ya Wamang’ati na Wahadzabe na vifaa ninavyouza hapa vimekusanywa kutoka kwa kina mama vijijini,” anasema.
Anasema fedha anazopata huzirejesha vijijini kisha hufanyika utaratibu wa kuzigawa kwa kina mama kulingana na kiasi kilichopatikana.
“Pesa ninazopeleka zinawasaidia kina mama katika maisha yao, lakini kubwa zaidi zinatumika kusaidia elimu kwa watoto. Nauza shanga, vibuyu na mapambo mengine ya urembo,” anasema Gidabaso.
Anasema japo biashara hiyo imeanza miezi miwili iliyopita, matumaini ya mafanikio yameshaanza kuonekana. Wastani wa mauzo kwa siku ni dola 50 [Sh zaidi ya 100,000]. Wateja wake wengi ni raia wa Marekani na Ufaransa.
Katika duka la jamii ya Wahadzabe yupo Isila Abeda (31). Vifaa anavyouza vinakusanywa kutoka vijiji vya QangDEND, Mandagaw na Murus.
“Kikundi chetu ni cha kina mama wa jamii ya Wahadzabe waishio Mang’ora, Tarafa ya Eyasi. Tunawashuruku NCAA walitufuata na kutueleza kuwa kuna nafasi ya kufanyia biashara hapa. Tunauza vitu mbalimbali vya urembo na dawa kama za kukata sumu za nyoka. Tunauza mbegu zinazotumika kutengeneza sabuni za kufulia – mbegu zake ni ndogo ndogo kama shanga. Wageni wengi wamevutiwa na vitu vyetu vya asili,” anasema Abeda.
Kama ilivyo kwa watu wa jamii ya Wadatoga, Abeda anasema nao hukusanya bidhaa kutoka vijijini kwa kina mama; na baada ya kuuza huwapelekea fedha ambazo hugawana.
Anasema pamoja na nia nzuri kabisa ya NCAA ya kuwatengea eneo maalumu la biashara, tatizo kubwa wanalokabiliana nalo ni zuio la madereva na waongoza watalii ambao hawataki kabisa wageni wao waingie kwenye maduka yao ya ujasiriamali.
“Changamoto kubwa hapa ni madereva wanaotufukuza. Hawataki tuwasogelee wageni, wanataka wawapeleke kwenye maboma ambako huwa wanapewa bakshishi tofauti na sisi hapa. Hili linapaswa litazamwe na uongozi ili madereva wasituzuie,” anasema Abeda.
Kwa upande wa jamii ya Wamasai, mwakilishi wao ni Ngoona Langoi, anayewaongoza wanavikundi wenzake kutoka kata saba za Tarafa ya Ngorongoro.
Pamoja naye, wapo kina mama wengine: Matasia Nengoyo, Sipapei Orkery na Nabulu Yakon.
“Hapa tulianza Julai 11, 2019. Tunauza shanga na mapambo mengine ya asili ya Kimasai. Wazo hili tulipewa na uongozi wa Mamlaka ya Ngorongoro. Tunashukuru hapa tunapata pesa nyingi tofauti na kule kwenye maboma.
“Tunachoomba sasa ni kupewa mafunzo ya kijasiriamali ili tufanye kazi zetu vizuri zaidi na kwa njia za kisasa. Tunahitaji mafunzo yatakayotuwezesha kuboresha bidhaa zetu zaidi ili ziwavutie zaidi wateja wetu,” anasema.
Kiongozi wa wajasiriamali hawa, Sadera Laizer, kama Abeda, anasema anapambana na wakati mgumu kutoka kwa madereva wanaowazuia watalii kwenda kununua bidhaa zao.
“Hawa ninaowapata hapa ninawapata kwa kuvizia-vizia, madereva hawataki kabisa waje huku, sisi ni wachanga, hatuwezi kuwapa tip kama wanavyofanyiwa maeneo mengine.
“Tunapendekeza kuwekwe spika itakayosaidia kuwatangazia wageni wanapokuwa ule upande wa makumbusho kuwa kuna bidhaa za asili wanazoweza kununua kama zawadi.
“Lakini tunapendekeza pia kwa NCAA waweke mabango hapa makubwa yatakayowaelekeza wageni mahali kulipo na maduka ya wajasiriamali – tena yawe katika lugha tofauti tofauti,” anasema Laizer.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa NCAA, Nchila, anasema lengo la Mamlaka, na hasa kwa upande wa ofisi yake, ni kuhakikisha kuwa wananchi wanawezeshwa kwa fursa mbalimbali zinazopatikana.
Anasema mwitikio wa wananchi umekuwa mzuri, na kwamba wanachotakiwa ni kuhakikisha wanatengeneza bidhaa nyingi na zenye mvuto ili kuwavutia watalii kununua bidhaa zao.
Kuhusu changamoto ya madereva kuzuia watalii kuzuru maduka ya wajasiriamali, Nchila, anasema atawasilisha suala hilo kwenye mamlaka husika ili kulipatia ufumbuzi.
“Niseme tu kuwa hili tumelipokea na naamini uongozi hauwezi kushindwa kulipatia ufumbuzi maana bila kupata wageni hili jengo litakuwa halina faida. Lilijengwa ili kuisaidia jamii ijikwamue kiuchumi,” anasema Nchila.