Juzi Jumapili nchi yetu imetimiza miaka 51 ya Uhuru tangu tulipoupata Desemba 9, 1961 na mwaka mmoja baadaye ndhi yetu ikawa jamhuri. Kwa hiyo tumetimiza pia miaka 50 ya Jamhuri ingawa hili halitajwi sana.
Najua wapo Watanzania wasioweza kulielewa vyema hili kwamba namaanisha nini kwa kusema tumetimiza miaka 50 ya Jamhuri, hivyo kidogo nitapaswa kulifafanua hili. Ninapozungumzia Jamhuri katika makala haya ya leo sizungumzii JAMHURI gazeti hili unalolisoma. Nasi katika historia ya wiki iliyopita Desemba 6, tumetimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa gazeti hili.
Nimeandika makala ya kuwashukuru wadau kwa kutuunga mkono, nawashukuruni nyote mlionipigia simu, mlionitumia parua pepe au kunitumia ujumbe mfupi wa simu (sms). Nawaahidini nyote kuwa yote mliyonishauri nitayazingatia.
Sitanii, Jamhuri ninayoizungumzia leo ni Taifa letu. Tulipopata Uhuru mwaka 1961, nchi yetu iliendelea kuwa chini ya nalkia kama nkuu wa nchi. Hivyo Mwalimu Julius Nyerere alibaki kuwa Waziri Mkuu Mtendaji katika nchi ya Tanganyika, suala ambalo ni wazi nchi haikuwa na mamlaka kamili. Kwa nchi kuwa na mamlaka kamili, kiongozi wa juu anayechaguliwa ndiye anayepaswa kuwa mkuu wa nchi na mkuu wa majeshi (Amiri Jeshi Mkuu).
Kwa wanaosikia historia ya nchi hii, mara kadhaa mmesikia Mzee Rashidi Mfaume Kawawa akisifia mwaka 1962 alipoachiwa nchi na Mwalimu Nyerere, wakati Mwalimu Nyerere alipojiuzulu wadhifa huo kwa nia ya kugombea urais wa Tanganyika na hatimaye kuchaguliwa kama kiongozi mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, hivyo kuhitimisha mamlaka ya Malkia wa Uingereza katika nchi ya Tanganyika.
Tukio hili lilitokea ndani ya mwaka mmoja wa Uhuru na hivyo Desemba 9, 1962 Tanganyika ilipata Rais wa Kwanza na kiongozi wa juu wa nchi mwenye mamlaka ya mwisho, hivyo Tanganyika ikawa Jamhuri (Republic). Ndiyo maana nasema Jumapili tumesherehekea miaka 51 ya Uhuru na miaka 50 ya Uhuru kamili – Jamhuri.
Katika miaka ya mwanzo ya Uhuru, Mwalimu Nyerere aliwaambia Watanganyika na hatimaye Watanzania, kuwa nchi hii ilipigania Uhuru kwa nia ya kuwaletea wananchi wake maendeleo, kuondoa unyanyasaji, kuweka usawa mbele ya sheria, kuhakikisha kila mwananchi anapata haki bila kubaguliwa, kutozwa tozo (rushwa) nje ya malipo halali (mshahara), na kubwa kuliko yote kufuta maadui watatu – ujinga, maradhi na umasikini.
Sitanii, kufanikisha hayo, Mwalimu Nyerere alisema ili tupate maendeleo ya kweli tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Najua watu tunao na hili halina ubishi. Ardhi nayo tunayo, tena iliyosheheni madini, gesi na mafuta. Tatizo letu hapa ni siasa safi na uongozi bora. Uongozi bora unazaliwa na siasa safi, hivyo kwa kuwa tulianza safari yetu na mguu wa kushoto, ni wazi hatuwezi kupata uongozi bora.
Namaanisha nini kwa siasa safi? Hapa namaanisha mfumo. Viongozi wetu kwa bahati mbaya Katiba imewakasimu mamlaka makubwa. Inasema wazi kuwa Rais hawezi kuhojiwa, kushitakiwa au kusutwa kwa jambo lolote alilofanya au asilofanya kwa kipindi alichokuwa madarakani. Hapa ndipo kitanzi chetu kilipo.
Marekani ilipopata uhuru mwaka 1776 kutoka kwa Waingereza, Rais wao George Washington, wanayemwita ‘Baba wa Taifa’ kwao, alisimamia uandishi wa Katiba inayotoa uhuru mkubwa kwa wananchi wa Marekani. Tangu mwaka huo, Katiba ya Marekani ilifumua mfumo wa kikoloni na kuingiza mfumo wao wa utawala wautakao.
Kwamba kama Katiba ya Mwingereza aliyekuwa akiwatawala ilikuwa inasema Rais hatahojiwa na mtu yeyote, Katiba yao ikasema Rais atahojiwa na mtu yeyote kutokana na matendo yake anapokuwa madarakani. Katiba ya mkoloni ilikuwa inazuia maandamano na inajenga matabaka kwa nia ya kuendeleza ubaguzi, Katiba hii ya Wamarekani ya mwaka 1776 ikaruhusu mikutano ya hadhara, maandamano, uhuru wa kuabudu, haki ya kuishi, haki ya kupata habari (uhuru wa vyombo vya habari) na vinginevyo.
Chini ya mkoloni, uongozi wa kifalme ulikuwa ukimruhusu malkia au mfalme wa Uingereza aliyekuwa mkuu wa makoloni ya Amerika, kuunda wizara idadi yoyote atakayo, lakini Katiba hii ya Wamarekani ikasema wazi kuwa idadi ya Wizara na mawaziri kuanzia wakati huo zitakuwa 16. Hadi leo Rais yeyote wa Marekani akiingia madarakani hana uhuru wa kuunda wizara mpya aitakayo kama ya Rais Jakaya Kikwete alivyotutangazia kama Taifa kuwa ameamua kuunda ‘Wizara ya Kitoweo’!
Kiwango cha Serikali kuchukua mikopo kutoka nje kiliwekwa tangu mwaka 1776, lakini kwetu hapa deni linakua tu hatuambiwi tunakopa kiasi gani na kwa kazi gani kabla ya kufanya hivyo. Kwa Marekani Katiba inazuia hilo. Rais aliyeko madarakani anakopa fedha baada ya Bunge kuidhinisha mkopo husika na wanataka matokeo ya kazi ya mkopo husika.
Wenzetu Kenya wameliona hilo. Katiba yao waliyoiandika mwaka 2010 imeweka wazi mamlaka na mipaka ya Rais wa Kenya. Kuanzia mwakani yeyote atakayeshinda Uchaguzi wa Urais Machi 6, 2013 atalazimika, kwa mujibu wa Katiba, kuunda Baraza la Mawaziri 22 tu, kutoka idadi ya sasa ya 42 na naibu mawaziri utitiri. Hapa kwetu tunao mawaziri wangapi? Hata idadi haifahamiki vizuri. Nasikia tunao jumla 50 ukichanganya na naibu mawaziri wao.
Sitanii, ingawa tunasema tunayo Dira ya Taifa 2025, dira hii ipo kwenye vitabu zaidi kuliko uhalisia. Ndiyo maana leo tuna mikakati mingi ya kuondoa umasikini lakini hatuoni matokeo ya wazi. Upo Mkukuta, Mkurabita, Mku, Vision 2025, Tasaf na mingine mingi lakini wanaoiona miradi hii ni wafadhili.
Tunabaki kuambiwa kuwa tumeufuta umasikini kwa kuchukua pato la Said Salim Bakharesa na kugawia idadi ya Watanzania, kisha tunatamba kuwa uchumi umekua, kumbe ni hewa. Fedha hizo wanazo watu wasiozidi 10 hapa nchini.
Mwaka 1906 Mjerumani alikamilisha ujenzi wa Reli ya Dar es Salaam hadi Mwanza. Julai 1914, Mjerumani alikamilisha ujenzi wa Reli ya Tabora hadi Kigoma, hivyo akawa ameiunganisha nchi. Alijenga mtanado hadi Tanga kwa ajili ya bandari, akajenga reli hadi Arusha. Mimi wakati nasafiri kwenda Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nilitumia treni kutoka Mwanza-Dar es Salaam-Arusha. Leo uliza, kiko wapi?
Hakuna nchi iliyoendelea kokote duniani, kwa kutumia malori kusafirisha mizigo. Nimekwenda Lubumbashi, Katanga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wana maelfu ya tani za shaba inayotaka kusafirishwa nje ya nchi na wanalia Tanzania iboreshe reli waanze kutulipa dola kupitisha mizigo yao hapa, lakini tumeziba masikio.
Sitanii, tunakumbuka shuka kumeishakucha. Miaka 50 baada ya Uhuru ndipo tunakimbia kuandika Katiba. Katiba tunayoitumia sasa nathubutu kusema kuwa ni mawazo ya watawala. Wananchi hawakupaswa kushirikishwa, ambapo wangeweza kukataa Rais kuwa mungu wa pili hapa duniani. Kwamba Rais asihojiwe kwa lolote alilolitenda hata kama kabofoa ni hatari kwa maendeleo ya taifa.
Ndiyo maana nikasema hapo juu kuwa kama nchi tunahitaji siasa safi, itakayozaa uongozi bora, uongozi huu ukaunganisha watu kutumia ardhi tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kwa nia ya kujiletea maendeleo kama mtu mmoja mmoja na hatimaye kama taifa zima. Masikitiko yangu katika hili ni kasi tuliyonayo katika kuandika Katiba hii na aina ya hadidu za rejea walizopewa akina Jaji Joseph Warioba.
Mwaka 2007 nilipata kuzungumza na Rais Jakaya Kikwete kwa muda mrefu tukiwa wawili tu kwenye simu. Katika kushauriana akaniambia kuwa anataka kuchukua mkopo mkubwa (sovereign bond), ambao angeutumia kujenga reli ya umeme kutoka Dar es Salaam hadi Bujumbura, Burundi. Nilimwambia bila kificho kuwa angeliweza hilo, basi angekuwa ameandika historia ya kuifutia umasikini nchi hii.
Niliuze kilichofuata. Niliendelea kufuatilia Rais Kikwete na kumkumbusha mara kwa mara mpango huu umefikia wapi. Mara ya mwisho aliniambia uchumi wa dunia uliyumba mwaka 2008 kukatokea mdororo wa uchumi, na hivyo riba ya mikopo mikubwa ikaenda juu. Kwa mantiki hiyo akasitisha mpango huu wa kukopa kujenga reli. Lakini hakusitisha mpango wa kukopa kujenga barabara zinazoharibiwa na malori.
Ingawa alikuwa anaogopa ukubwa wa riba kujenga reli, tumeshuhudia deni la taifa likipanda chini ya utawala wake kutoka wastani wa Sh trilioni 5.5 aliloacha Mzee Mkapa baada ya kusamehewa madeni, na sasa tunavyozungumza deni la taifa limefikia Sh trilioni 22. Hii ni kwa uchache tu nimejaribu kuonesha madhara ya nchi kuachwa mikononi mwa mtu mmoja kuamua analodhani linafaa kwa ajili ya wananchi.
Sitanii, katika miaka hii 51 ya Uhuru na 50 ya Jamhuri, tulikosea kutokuwa na Katiba inayoeleza bayana madaraka ya Rais, uwezo wa wananchi kudai maendeleo, uwazi, uhuru wa vyombo vya habari na kiwango cha mkopo inachoweza kuidhinisha Serikali bila kuomba kibali cha Bunge.
Tukirejea kosa hilo katika Katiba mpya, la kumwacha Rais kuwa kama mfalme kufanya atakalo bila kuhojiwa, nchi hii itageuzwa Saccos. Fursa ni hii. Tusome Katiba ya Kenya, sura na mwelekeo wa Katiba yetu ubane mianya kama Kenya walivyofanya, maendeleo yataota kaa uyoga. Mugu ibariki Tanzania.