Leo ni Juni 16, 2015. Tarehe kama hii mwaka 1976 katika mji wa Soweto nchini Afrika Kusini, watoto wa shule wapatao 600 waliuawa na utawala wa Wazungu (makaburu) kwa kumiminiwa risasi za moto wakiwa katika maandamano ya amani kupinga mtaala mpya na lugha ya Afrikaan kutumika katika kufundishia.
Kwanza naomba nieleze sababu zilizonishawishi kushika kalamu na kuandika kwa ufupi tukio hilo la kihistoria. Mosi, uzalendo wangu kwa watoto wa Afrika na bara langu la Afrika kukumbuka tukio hilo la kikatili lililotokea miaka 39 iliyopita, bado lina simanzi na makiwa moyoni wangu.
Nawatakia rehema kwa Mwenyezi Mungu aweke roho zao Mahali Pema Peponi. Amin!
Pili, kuonesha enzi hizo umoja, msimamo, mshikamano na uzalendo ulivyowajaa, si watu wazima tu bali hata watoto shuleni, walivyokuwa na hamasa na ari kupinga utawala uliojaa ubaguzi wa rangi, dhuluma, mateso na manyanyaso, uliofanywa na walowezi makaburu dhidi ya wenye mali na nchi – Waafrika.
Tatu, kusisitiza umuhimu wa elimu shuleni. Masomo ndiyo shule. Walimu, vitabu, madawati, majengo na kadhalika ni njenzo za kufundishia na kujifunzia kupata elimu bora. Kuweka mitaala na lugha isiyofahamika ya kufundishia, ukweli ni kubagua utaratibu mzuri wa utoaji elimu bora na hatimaye kuua elimu na kuwafanya watoto kuwa wajinga. Elimu ni hazina kubwa na urithi wa uhakika usio na mtetereko.
Nne, kukumbusha na kufahamisha daima adui ni nduguyo na kikulacho kimo maungoni mwako. Watoto wale walifyatuliwa risasi na askari 48 waliopangwa kutekeleza operesheni ile. Kati ya askari wale Wazungu walikuwa wanane na Waafrika walikuwa 40.
Sababu hizo zimenifanya leo kushika kalamu kuandika na kutia ubani kuwaombea rehema kwa Mwenyezi Mungu. Laiti watoto wale wasingenyang’anywa uhai wao hapana shaka baadhi yao leo wangekuwa walimu, viongozi wa serikali au siasa, waganga na wauguzi, manahodha na marubani, madereva na mafundi mchundo. Achilia mbali wahandisi na wataalamu. Bila kusahau viongozi wa dini, wanamichezo na wasanii, polisi na askari jeshi na waandishi wa habari wangepatikana.
Sasa nije kwenye habari yetu. Chokochoko ya kuuawa watoto wa shule inaanzia mbali kihistoria na kijiografia ya nchi ya Afrika Kusini. Nchi hii ina mali na rasilimali nyingi aina mbalimbali kama madini, misitu, ardhi yenye rutuba na bahari mbili – ya Hindi na Kusini Atlantiki – zenye samaki na viumbe vingi vya baharini na pepo mwanana.
Majangwa ya Kalahari na Namib, uwanda wa juu na safu za milima pamoja na uwanda wa pwani unaotiririsha joto la wastani na baridi nyembamba, zinajenga mandhari safi na mvuto kwa mtu yeyote kuashiki kuishi Afrika Kusini. Maumbile na tabia za wananchi ni sumaku kali zinazovuta kila mtu apitaye au anayevinjari katika nchi hiyo.
Wahenga wamesema mti wenye matunda huponzwa kupopolewa mawe na matunda yake. Utajiri wa nchi na ukarimu wa wananchi uliwavuta Wareno, Wadachi, Wafaransa, Wajerumani na Waingereza kufanya utalii, biashara na kuweka makazi ya kudumu.
Makazi hayo yakastawisha ukoloni mkongwe na utawala wa kibaguzi wa rangi, dhuluma, ukatili, uonevu na dharau kwa wananchi – Waafrika.
Wadachi ndiyo walioanza kujazana mithili ya kumbikumbi kwenye kichuguu na hatimaye kuwakaribisha Wazungu wenzao kutoka mataifa ya Ulaya kuja kulowea na kushika hatamu za utawala, njia kuu za uchumi na kumiliki ardhi yote na kuwaacha wananchi wenye mali na haki patupu.
Mshairi Nahodh Ibrahim Mbiu Bendera anatutonesha kwa utenzi usemao:-
Ardhi ilivyo nzuri, walitwa kwa jeuri,
Wakailima kwa jeuri, kote waliingilia,
Afrika Kusini moja, ilianza kwa kuonja,
Vita vyao walokuja, Weupe wagombania,
Wadachi na Waingereza, walianza heleleza,
Vita kuviendeleza, ulowezi shindania,
Hivi ni vita vya mali, kupata rasilimali,
Kunyang’anya wa asili, aridhi walorithia,
Wananchi walishindwa kuhimili utawala wa makaburu na waliamua kuanzisha mapambano kudai uhuru wa nchi yao na ukombozi wao. Walianza kidogo kidogo kuunda chama cha ukombozi. Januari 8, 1912 Chama African National Congress (ANC) kilianza kama mchirizi wa maji ardhini.
Mchirizi ule ulipanuka na kuwa kijito na kurefuka kama Mto Nile. Kuanzishwa Chama cha Pan African Congress (PAC) na Inkatha Freedom Party ndani ya kijito hicho, wapigania uhuru na ukombozi wa Mwafrika akina Albertina Sisulu, Oliver Tambo, Enock Sontonga, Steve Biko, Nelson Mandela na wengine wengi pamoja na makundi ya wananchi walipanua kijito na kuwa mto mpana na mkubwa.
Mto huu uliwapa wananchi hao nafasi ya kuogelea na kupiga mbizi bila kujali mawimbi mazito na makubwa na mwendokasi wa maji. Kwani waliweza kuibuka kila mara na mambo mikononi. Waliibuka na lulu kwa kumchagua Nelson Mandela kuwa rais mpya wa chama chao cha ANC mnamo Juni 26, 1961. Kuanzia hapo nginjanginja ya kudai uhuru ikatikisa utawala wa makaburu na kuuweka kwenye kingo ya mto.
Hali haikuwa shwari kwa makaburu. Walianzisha kamata kamata na kuwatia korokoroni viongozi wa siasa, wanachama na wanaharakati kuzuia mawimbi ya mapambano.
Katika mkumbo huo, kinara wa mapambano ya ukombozi, kijana Nelson Rolihlahla Mandela, aliyeanzisha ‘Umkhonto we Sizwe’ maana yake ‘Mkuki wa Taifa’ Kwanza, alikamatwa na kuswekwa jela kifungo cha maisha mnamo Novemba 6, 1964.
Makaburu hawakutambua mto ule ulitiririsha maji yake mabondeni na vilimani, mijini na vijijini, mchana na usiku na kuhamasisha wananchi. Waume kwa wanawake, wazee kwa vijana na kadhalika watoto. Wote walioga na kuyanywa maji hayo na kuhisi tamu ya maji ingawa yalikuwa na ugwadu.
Katika hali ya kutapatapa, utawala wa makaburu zaidi ya kuwatupa wapigania uhuru magerezani, ulianzisha na uliweka vikwazo mbalimbali vya kiuchumi, kuzuia safari za nje ya nchi kwa viongozi wa ukombozi na kuanzisha taratibu za kudumaza na kunyima elimu bora kwa watoto wa Kiafrika, kwa kupitisha sheria, sera na mitaala ya mafunzo.
Agizo la kuacha kutumia lugha ya Kiingereza kufundishia na badala yake kutumia lugha ya Afrikaan inayotumiwa na makaburu wenyewe (Afrikaners-Wadachi, Wafaransa na Wajerumani). Lugha hiyo kwa Waafrika ni ngeni na ina ukakasi.
Agizo hilo halikuwafurahisha wazazi, walimu na watoto wa shule. Mchakato na maelezo mbalimbali yalitolewa kupinga agizo hilo na kamati iliundwa kusimamia upingaji. Migomo ya hapa pale ilianzishwa shuleni.
Hatimaye mpango uliwekwa kufanya maandamano ya amani kusisitiza kukataa agizo la utawala wa makaburu. Naam, mipango ilipangika, watoto wa mjini Soweto waliingia mitaani kwa maandamano ya amani.
Kwa watoto yalikuwa ya amani, lakini kwa makaburu kisirani. Mshairi gwiji na maarufu Ibrahim Mbiu Bendera anateremka na tunzi ifuatayo:-
Ni Juni kumi na sita, wanafunzi wamesita,
Hawautaki utata, elimu duni susia,
Walikutana Soweto, kundi kubwa la watoto,
Nyimbo zao motomoto, mbele wanakimbilia.
Kaburu hawakusita, kuyakabili matata,
Kwa risasi tata tata, watoto kushambulia,
Migomo ikaanzia, nchi nzima ikaingia,
Kaburu akapania, watoto kuwafungia.
Magereza yafurika, watoto wa kila rika,
Yakaingia mashaka, pembe zote za dunia,
Fika sabini na saba, Steven Biko walimkaba,
Kaburu hana mahaba, mahabusu kajifia.
Kaburu ni wa ajabu, kawazulia sababu,
Watoto kawasulubu, kalaaniwa na dunia,
Leo duniani kote wapenda amani wanaomboleza vifo vya watoto waliouawa kwa sababu tu ya kudai uhuru na haki yao. Ni tendo ambalo halitasahaulika daima. Ni miaka 39 tangu tukio hilo litokee na tunawalaani makaburu kwa tabia na matendo yao ya kikatili.
Jambo la kushangaza na kusikitisha hapa nchini. Wapo baadhi ya Watanzania wenye hadhi na heshima zao wanadiriki kuwaua watoto wenye ulemavu wa ngozi. Je, watu hawa hawafanani na waliokuwa makaburu?
Wakati tunaomboleza vifo vya watoto wa mjini Soweto, Afrika Kusini, tusisahau kutia ubani na kuwatakia rehema kwa Mwenyezi Mungu watoto wote duniani waliouawa kikatili kwa ajili ya kulinda na kutimiza maslahi ya wakubwa kiutawala na kiuchumi.
Tukumbuke watoto ni tunu wala hawahitaji hukumu. Ni johari zinazohitaji ulinzi na malezi. Hawamalizi hamu kuwaenzi. Naiomba Serikali kuendelea kukomesha ukatili dhidi ya watoto. Na wanasiasa tuache pekepeke katika nyendo zetu tuwape watoto malezi azizi.