Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato

MKAZI wa kijiji cha Msilale,Mkama Mwizarubi (26) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto mwenye ulemavu wa kusikia na kuongea (Bubu) kinyume cha sheria za nchi.

Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama ya Wilaya ya Chato mkoani Geita baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa pasipo kuacha shaka.

Katika kesi hiyo namba 21023 ya mwaka 2024,mshitakiwa alidaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Desemba 2023 hadi Julai 2024.

Awali mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya mashitaka Wilaya ya Chato, Mauzi Lyawatwa, ameileza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alitenda makosa mawili kinyume cha sheria licha ya kujua wazi kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Ameileza mahakama hiyo kuwa kosa la kwanza, ni kumbaka mtoto chini ya miaka 18 ambalo ni kinyume na kifungu cha 130(1) (2)(e) sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Huku kosa la pili (kumpa mimba mwanafunzi) ni kinyume na kifungu cha 60 A (3) cha sheria ya elimu sura ya 353 iliyofanyiwa marejeo yake mwaka 2009.

Hata hivyo baada ya mahakama hiyo kupitia ushahidi uliowasilishwa mbele yake na upande wa mashitaka ikiwemo fomu maalumu ya matibabu kutoka kwa Jeshi la Polisi (PF3) maelezo ya mashahidi pamoja na daktari aliyefanya uchunguzi wa afya ya mtoto huyo, vilitosha kuithibitishia mahakama hiyo kuwa mshitakiwa anayo hatia ya kutenda kosa.

Kabla ya kutolewa huku hiyo,mshitakiwa alipewa nafasi ya kuomba kupunguziwa adhabu,ambapo aliiomba mahakama hiyo kumwachia huru kwa kuwa anayo familia inayomtegemea.

Mbali na maungamo hayo,Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama hiyo,Erick Kagimbo amesema kutokana na ushahidi na maelezo yaliyotolewa na pande zote mbili katika kosa la kwanza, mahakama hiyo imejiridhisha kuwa mshitakiwa anayo hatia ya kumbaka mwanafunzi wa darasa la tatu kitengo cha watoto wenye mahitaji maalumu kinyume cha sheria.

Ambapo katika kosa hilo,mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kufanya makosa kama hayo.

Amesema katika kosa la pili la kumpatia mimba mwanafunzi,upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa ujauzito huo ni mali halali ya mshitakiwa na kwamba mahakama hiyo imemwachia huru.

Kadhali askari waliokuwa eneo la mahakama hiyo,wamemchukua mshitakiwa huyo na kumpeleka kwenye Gereza la Wilaya ya Chato ili kuanza kutumikia adhabu yake.