Mwezi kama huu takriban miaka 26 iliyopita Tanzania ilikumbwa na msiba mkubwa wa kihistoria kuwahi kutokea baada ya meli ya abiria iliyokuwa ikitoka Bukoba, Kagera kuelekea Mwanza kupinduka na kuzama kwenye Ziwa Victoria.
Ingawa hakuna idadi kamili iliyotolewa, lakini kwa namna yoyote ile, wengi miongoni mwa abiria waliokuwa wakisafiri kwa meli hiyo inayosadikika kubeba zaidi ya uwezo wake wanahofiwa kufa maji kutokana na kuwapo
kwa manusura wachache.
Miaka mingi sasa imepita lakini waliowapoteza wapendwa wao katika ajali hii bado wana kumbukumbu ya majonzi
yaliyowakuta na kwa hakika wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla hawatamani kushuhudia tena tukio kama lile.
Wakati Watanzania wenzetu ambao baadhi yao mabaki yao yamehifadhiwa katika makaburi ya pamoja Igoma, jijini Mwanza, wakiwa wamepumzika, ni vema kama taifa tukajiuliza hali ikoje kwa sasa katika usafiri wa maziwa yetu?
Je, usafiri wa majini ni salama mwaka 2022 kuliko ulivyokuwa mwaka 1996? Vyombo vinavyotumika kusafirisha abiria na mizigo majini vinao ubora stahiki?
Watanzania wanaoishi visiwani na mwambao wa maziwa na bahari wamefikiwa na maendeleo yaliyofanyika? Kwa namna fulani, usafiri wa ardhini umeimarika zaidi nchini kwa sasa na hili ni suala la kuipongeza serikali, kwa kuwa maeneo mengi, karibu makao makuu ya mikoa yote nchini isipokuwa Katavi na Kigoma, Mara na Arusha; yameunganishwa kwa barabara za lami.
Ujenzi wa reli ya kisasa nao unaendelea ikiwa ni ishara ya kuimarika kwa usafiri wa treni ndani ya miaka michache
ijayo, kitendo kitakachoondoa adha kwa wananchi na kuimarisha usalama.
Ni bahati mbaya kwamba usafiri wa majini, ukiondoa usafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar, bado haujafikia
ubora stahiki. Usafiri unaotumika kwa asilimia kubwa ya visiwa vilivyopo kwenye maziwa ya Tanganyika, Nyasa na
Victoria ni duni, wa hatari na wa kienyeji kabisa.
Ingawa macho ya serikali yameelekezwa zaidi Ziwa Victoria ambako kuna meli kubwa ya kisasa inajengwa, ukweli ni kwamba ni mitumbwi, maboti ya kizamani na vivuko chakavu ndivyo vinavyounganisha visiwa vingi ziwani humo vyenyewe kwa vyenyewe na mwambao wa ziwa.
Ziwa Tanganyika hakuna hata meli moja ya abiria ya kisasa inayotumika. Hii maana yake ni kwamba, miaka 26
baada ya ajali ya MV Bukoba, usafiri wa majini kwa Tanzania haujaimarika na ni vema sasa serikali na wadau wengine wakatupia jicho upande huo.
Mungu awalaze pema peponi ndugu zetu waliofariki dunia katika ajali ya MV Bukoba Mei 21, 1996. Amina!