Na Majid Abdulkarim, Dodoma

Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Mama na Mtoto, Wizara ya Afya, Dkt. Ahmad Makuwani amelitaka Baraza la Famasi Tanzania kuwa chachu ya kuboresha huduma za dawa katika Sekta ya Afya nchini ili wananchi waweze kupata huduma bora kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Dkt. Makuwani ametoa wito huo leo jijini Dodoma alipotembelea Jengo la Baraza la Famasi Tanzania linalojengwa Jijini Dodoma na kupanda miti katika kuelekea kilele cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake 2003.

Dkt. Makuwani amesema kuwa amefarijika kuona maendeleo ya ujenzi huo unaenda vizuri ambapo amesema baada ya muda si mrefu jengo hilo litakuwa limekamilika na kuanza kutumika ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya miaka 20 ya baraza hilo.

Aidha amesema kuwa Baraza hilo limefanya jambo zuri kupanda miti katika maendeleo ya jengo lao ikiwa ni ishara ya kulinda na kutunza mazingira ya jengo.

“Niwatakie kila la kheri katika kusherekea miaka 20 ya Baraza la Famasi Tanzania hivyo ni imani yangu kuwa huduma za dawa zitaimarika na kuwa bora ili wananchi wanufaike na kada hii ya wafamasia hapa nchini”, amesema Dkt. Makuwani

Kwa upande wake Msajili wa Baraza la Famasi Tanzania, Bi. Elizabeth Shekalaghe amesema katika kuelekea kilele cha kuadhimisha miaka 20 ya Baraza wanaunga mkono juhudu za Serikali kwa kutekeleza agizo la kuhamia Dodoma ambapo amesema hivi karibuni watakuwa wameamia katika jengo lao ambalo lipo katika hatua za mwisho kukamilika.

Bi.Elizabeth amesema kuwa ndani ya miaka 20 ya mafanikio yao wafamasia nchini walikuwa 423 lakini kwa sasa wafamasia wamefika 3317 ambao wamesambazwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuwasongezea wananchi huduma za famasi karibu yao.

“Idadi hii tunaweza kutekeleza majukumu yetu ipasavyo kama wafamasia nchini kwa kuongeza nguvu ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi hususani huduma za dawa”, ameeleza Bi. Elizath

Lakini pia ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kwa kutoa vibali vya ajira kwa kada ya famasi na kupelekea wafamasia kuhudumu nchi nzima sasa kuanzia ngazi ya msingi hadi ngazi ya Taifa.

Vile vile amesema kuwa kwa miaka 20 ya baraza hilo wanajivunia kuwa na mazingira mazuri ya kazi yameboreshwa,bajeti ya upatikanaji wa dawa imeongezwa zaidi ya asilimia 104 ambapo inawapa jukumu la kuhakikisha wanasimamia kikamilifu na wananchi wanapata dawa kwa usahihi na wakati.