Tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa, aage dunia Oktoba 14, 1999, kila mwaka ifikapo kipindi hicho Watanzania tumekuwa tukiadhimisha kifo chake huku tukishuhudia maneno mengi kwenye vyombo vya habari na kwenye mihadhara na makongamano.
Lakini yatupasa tujiulize, kwa miaka 20 baada ya yeye kufariki dunia, viongozi na wananchi kwa ujumla wetu tumefanya nini kwa yale tunayoyazungumzia kuhusu Mwalimu na yanayopendekezwa kila mwaka yafanyike kama njia ya kumuenzi kwa kuyaishi maisha yake ya uadilifu na uongozi wake uliotukuka?
Yaliyotokea wakati wa msiba wa Mwalimu, yakiwahusisha viongozi na watu mbalimbali kutoka nje ya nchi, yalidhihirisha Mwalimu alikuwa kiongozi wa namna gani.
Salamu za rambirambi za kusifia uongozi wake zilitoka kwa viongozi, watu mashuhuri na wananchi wa kawaida duniani kote. Walitusikitikia sana kwa kumpoteza kiongozi kama yule na kutuasa tudumishe misingi aliyotuwekea na kuendeleza yale yote aliyoyasimamia kwa manufaa ya taifa letu.
Je, sisi Watanzania tulielewa na tunajua vizuri umuhimu wa mawazo na vitendo vya Mwalimu Nyerere katika kuliletea maendeleo taifa letu? Tunafahamu thamani na maana ya uongozi wake uliotukuka uliotujengea umoja, amani na utulivu nchini mwetu mpaka akasifiwa kiasi hicho?
Miaka 20 sasa tangu amefariki dunia, sisi Watanzania tumefanya nini kumuenzi kwa vitendo kama walivyotuasa viongozi hao kutoka nje ya nchi wakati wa msiba?
Moja lililosemwa kwenye vyombo vya habari vya nje ni kwamba: “Tanzania imepoteza mtu aliyekuwa shujaa na mashuhuri duniani. Aliyekuwa na akili nyingi kuweza kubuni Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea – itikadi iliyoendana na mazingira ya nchi yake.”
Kwa maoni yangu, ‘kujitegemea’ ni jambo jepesi kueleweka. Hata katika maisha ya kawaida, ni aibu kwa mtu mzima kuishi kwa kumtegemea mjomba! Lakini inashangaza kuona Watanzania wengi wakiuchukulia Ujamaa kuwa kama jambo gumu sana!
Kwenye hotuba zake na maandiko yake, Mwalimu alitufundisha kwamba hii Siasa ya Ujamaa ina nguzo tano tu muhimu na iwapo tukizikubali na kuzifuata kwa dhati, tutaelekea kuwa Wajamaa kamili. Katika kijitabu alichoandika kinachoitwa ‘UJAMAA NI IMANI’, Mwalimu anaeleza kwamba ili tuwe Wajamaa yatubidi tuwe na Imani ya Ujamaa, yaani tuamini katika Ujamaa.
Akizielezea nguzo hizo, anasema ya kwanza ni: USAWA – alitutaka tuamini kwamba binadamu wote ni sawa. Pili: KAZI – tuamini kwamba tunapaswa kuishi kwa kufanya kazi kwa bidii. Tatu: HAKUNA UNYONYAJI – tuamini kwamba kila mtu lazima afanye kazi; siyo mtu akae tu na kutaka afanyiwe kazi na wengine. Nne: Tuamini kwamba vitu muhimu kwa maendeleo ya binadamu, kama vile ARDHI, viwe vya wote na tano: Tuamini kwamba nchini mwetu kusiwe na tabaka la mabwana na watwana. Kusiwepo mabwana wanaofanyiwa kazi na watwana wanaofanyishwa kazi.
Je, kuna ugumu gani kuziamini na kuzifanyia kazi nguzo hizo tano?
Mwalimu Nyerere aliasisi Siasa ya Ujamaa na kuliweka Azimio la Arusha ndani ya siasa hiyo baada ya kuangalia mazingira ya nchi yetu na kubaini machungu na shida za maskini na wanyonge wa nchi yake. Hakutaka nchi iwe kama nchi zingine ambazo viongozi, kwa makusudi, huamua kujenga tabaka la walionacho na wasionacho, huamua kujitajirisha wao, ndugu zao na marafiki zao na kuwaacha wananchi wengine wakibaki kwenye lindi la umaskini maisha yao yote na ya vizazi vyao.
Naomba radhi mapema endapo nitakosea kwa kuuliza; Je, viongozi wetu wa ngazi zote kwa miaka hii 20 bila ya Mwalimu, wamemuenzi vipi kwa vitendo katika kutekeleza siasa hii ya Ujamaa na Kujitegemea?
Kwa maoni yangu, wamekuwepo baadhi ya viongozi ambao tangu Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iasisiwe ndani ya Chama cha TANU na baadaye CCM, wao wamekuwa wanafiki tu walioikubali siasa hiyo kwa shingo upande au kwa maneno tu.
Ushahidi mmoja uliopo ni kwamba baada ya Mwalimu kuondoka kwenye madaraka serikalini na kwenye chama, baadhi ya viongozi walibadilika. Waliamua ‘kulichakachua’ Azimio la Arusha ambalo ndilo lilikuwa mhimili wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Mwalimu alinung’unika kuhusu suala hilo na kuhitimisha manung’uniko yake kwa kauli: “…watu wenye akili tukajua limekwisha!..” Waliolichakachua Azimio wakajitetea na wanaendelea kujitetea kwamba walikuwa wanakwenda na wakati.
Viongozi na wanachama wa CCM wakalisahau hata onyo la Mwalimu lililomo ndani ya Azimio hilo kwamba rushwa ni adui wa haki, wakanunua uongozi kwa kutoa rushwa kwa wapiga kura. Walianza kujificha kwa kuiita ‘takrima’, baadaye mambo yakaenda kombo na rushwa ikashamiri ndani ya Chama Cha Mapinduzi!
Wakati ule wa kifo cha Mwalimu, tuliambiwa na Rais wa India kwamba Mwalimu atakumbukwa kwa juhudi zake katika kutafuta ufumbuzi wa maendeleo ya kiuchumi. Je, juhudi hizo za Mwalimu ziliendelezwa? Kama ni ndiyo, ziliendelezwaje?
Ndani ya miaka hii 20 bila Mwalimu tumeona viongozi wetu badala ya kutafakari jinsi ya kuendeleza juhudi za Mwalimu kwa kuiboresha Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na kuleta matokeo chanya, wao walijitahidi kufanya ‘majaribio’ katika kutafuta maendeleo kwa itikadi isiyoeleweka mpaka ikafikia hatua wakawepo watu waliosema hawajui CCM ilikuwa inaendesha nchi kwa itikadi ipi!
Wapo pia waliokejeli na kusema kuwa tangu Mwalimu afariki dunia, CCM ilikuwa ikiimba wimbo wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na kucheza ngoma ya Ubepari na Utegemezi!
Wapo viongozi na wachumi nchini ambao walitaka tuamini kwamba kuwa na maghorofa marefu mijini na wananchi wengine kuishi kwenye nyumba duni ndiyo maendeleo; tuamini kuwa kuuza viwanda alivyovijenga Mwalimu na kutaifisha hata mashirika yaliyokuwa hayana matatizo; kutokusanya kodi ipasavyo na kutegemea wafadhili na mikopo kutoka nje ndiyo kutaleta maendeleo.
Wapo pia Watanzania wa kawaida walioamini kwamba kuishi kwa kushinda vijiweni bila kufanya kazi, ama kujihusisha na biashara haramu; kupiga dili za hapa na pale; kuuza dawa za kulevya; kuishi kwa kutoa na kupokea rushwa na kadhalika, ndiyo namna bora ya kuishi na kutafuta maendeleo ya kiuchumi! Viongozi wetu wakayafumbia macho mambo hayo wakidhani yatajirekebisha yenyewe bila kuchukua hatua kali. Kumbe sivyo!
Tulichokifanya Watanzania miaka yote hii baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere ni kuvuruga sifa aliyotujengea Mwalimu na kutambulika hadi nje ya mipaka yetu. Wana CCM wakavuruga uzuri wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyosifiwa kwamba ni itikadi ya aina yake miaka 20 iliyopita!
Waandishi wa habari nchini mwetu wamekuwa makini sana kwenye utafutaji wa habari mbaya na nzuri. Katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 waliandika mengi kuhusu Chama Cha Mapinduzi na serikali yake ilivyokuwa katika hatihati ya kutokubalika na kutishiwa kuondolewa madarakani kutokana na kujaribu ‘kuitelekeza’ Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere.
Waandishi wa habari waliifanya CCM izinduke kutoka kwenye ‘majaribio’ yaliyokwenda kinyume cha misingi ya chama iliyokuwa imejengwa na Mwalimu Nyerere – muasisi wa chama hicho, ambaye mara kwa mara alikuwa akiwakumbusha viongozi wa CCM kwamba endapo watakiuka misingi ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa kisingizio cha kwenda na wakati, watakwenda na maji.
CCM walipozinduka, wakatengeneza Ilani ya Uchaguzi iliyosheheni mambo chungu nzima ya kufanya ili kurejesha imani ya wananchi kwa chama hicho! Waandishi wa habari wakaendelea kufanya kazi yao kwa kueleza jinsi vyama vya upinzani, hususan Chadema walivyokuwa wanautumia udhaifu huo wa CCM kujipatia wafuasi wengi waliokuwa tayari kuwapigia kura katika Uchaguzi Mkuu.
Waandishi hao hao, walitujuza juu ya kazi kubwa aliyoifanya mgombea wa CCM wa nafasi ya urais, Dk. John Magufuli akishirikiana na timu yake hadi CCM ikaweza kupata ushindi wa asilimia 58 tu. Vyama vya upinzani vikafanikiwa kuongeza namba ya wabunge kutokana na kosa la ‘kiufundi’ la CCM la kukiuka misingi aliyoijenga muasisi wa chama chao.
Kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo kwa kuidumisha itikadi ya UJAMAA na KUJITEGEMEA ni jambo linalowezekana. Alipoingia madarakani miaka minne iliyopita, Rais Magufuli aliamua kwamba yeye hana muda wa kufanya ‘majaribio-jaribio’!
Naamini alikwisha kugundua hata kabla hajawa rais kwamba Mwalimu Nyerere alikwisha kuonyesha njia sahihi, kilichotakiwa ni kutumia akili kujua namna ya kuifuata njia hiyo na kutekeleza kulingana na wakati uliopo na kulingana na yaliyomo kwenye Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Rais Magufuli alikwisha kugundua pia kwamba juhudi alizokuwa amezianza Mwalimu za kutafuta ufumbuzi wa kiuchumi, kama alivyosema Rais wa India, ndizo hasa zinapaswa ziendelezwe. Rais Magufuli hakuhitaji kufanya ‘utafiti’, alijua kwamba Mwalimu alikuwa sahihi. Kwa kufuata nyayo za Mwalimu, aliamua kujikita katika sera ya viwanda, akihimiza ujenzi wa viwanda kama ambavyo Mwalimu alifanya.
Wengi wakajiuliza, atapata wapi fedha za kufanya hivyo? Akaja na mkakati wa kudhibiti ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma na atakusanya kodi ipasavyo. Mwalimu aliwahi kulalamika kwamba serikali ilikuwa haikusanyi kodi!
Rais Magufuli ameanzia Mwalimu alipoishia katika kujenga umeme wa Stiegler’s Gorge na kuamua kuupa mradi huo jina la Mwalimu.
Rais magufuli anasambaza umeme vijijini kwa kasi ya ajabu, tayari serikali yake imekwisha kuhamia Dodoma, mji ambao umefanywa kuwa makao makuu ya nchi. Anatoa elimu bure, amejenga vituo vya afya 365 na hospitali za wilaya zaidi ya 60.
Anajenga reli ya Standard gauge ambayo itawarahisishia uchukuzi na usafiri majirani zangu huku niliko wanaotoka Mkoa wa Mara kufika kwao kwa siku moja badala ya kutumia siku tatu – reli itakayokuwa na manufaa mengine mengi kiuchumi.
Amefufua Shirika la Ndege kwa kununua ndege saba kwa fedha za ndani. Amedhibiti wizi wa madini uliokuwa ukifanywa na kampuni za nje kwa kushirikiana na viongozi wetu wasio waadilifu katika kutengeneza mikataba mibovu.
Haya pamoja na mengine mengi yamefanywa ndani ya miaka minne tu!
Kwa hakika, Rais Magufuli amejithibitisha kuwa ndiye kiongozi anayemuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo. Viongozi wengine na sisi wananchi kama tuna nia njema ya kumuenzi Mwalimu Nyerere tunapaswa kumuunga mkono kwa dhati Dk. Magufuli na si kwa kumpiga vita na kunung’unikia anayofanya ambayo huko nyuma hakuna aliyeweza kuyafanya.
Na tumuunge mkono si kwa unafiki ule wa kukubali Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na baadaye kuidhoofisha kutokana na ubinafsi tu.
Kama alivyosema Mama Madeline Albright, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani aliyekuja nchini wakati wa mazishi ya kitaifa ya Baba wa Taifa: “Tunapaswa kumuenzi Mwalimu kwa kuiga maisha yake na kuendeleza yale yote aliyokuwa akiyakazania kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania na Afrika.”
Rais wetu wa kipindi hicho, Benjamin Mkapa, alihitimisha mazishi hayo ya kitaifa yaliyofanyika Uwanja wa Taifa (Uhuru) Oktoba 21, 1999 na yaliyohudhuriwa na umati wa Watanzania walioungana na marais na viongozi wa juu kutoka nchi 92 duniani, kwa kusema: “…kwa kuja kwao (viongozi hao 92 na watu wengine kutoka nje) wanatuhimiza tuwe warithi waadilifu watakaoendeleza yote aliyoyafanya Mwalimu hata yakampa umaarufu huo.”
Haya maneno aliyotuasa Rais Mkapa miaka 20 iliyopita, yanapaswa yatekelezwe kwa vitendo sasa. Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea inapaswa kutafsiriwa na kufanyiwa kazi kwa vitendo na kwa nguvu zote. Chama Cha Mapinduzi kisiionee aibu Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa sababu ikisimamiwa na kuendelezwa ipasavyo tungeendelea kuonekana tuna itikadi ya aina ya pekee iliyofanikiwa kuleta maendeleo ya haraka nchini.
Wanaotaka kugombea uongozi kupitia Chama Cha Mapinduzi chenye itikadi hiyo, waamue kuwa waadilifu na waaminifu kwa Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, vinginevyo wasiwe wanafiki na kugombea ilhali mioyoni mwao hawalitaki Azimio hilo na hawaitaki Siasa ya Ujamaa.
Pamoja na hayo yote, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, Oktoba 23, 1999 wakati Mwalimu akizikwa nyumbani kwake kijijini Butiama, alisema: “… maisha ya Mwalimu ni kioo cha kujitazamia na kujichunguza…”
Tangu Mwalimu afariki dunia, viongozi wetu na wananchi kwa ujumla tulipaswa kuwa tunajitazama kwenye kioo cha maisha ya Mwalimu yaliyotukuka na kujirekebisha ipasavyo. Kama kwa miaka 20 hatukuwa tukijitazama kwenye kioo hicho, sasa tunapaswa kuanza kujitazama, kujichunguza na kujirekebisha ili tuanze kuiga maisha ya Mwalimu Nyerere kwa ustawi wa maendeleo yetu. Tunapaswa tujidhihirishie na tuidhihirishie dunia kwamba kweli tunamuenzi Mwalimu kwa vitendo.
Hatujachelewa sana. Kama alivyowahi kusema Mwalimu mwenyewe: “Inatubidi tukimbie wakati wenzetu walioendelea wanatembea!”
Anna Julia Mwansasu ni Katibu Muhtasi mstaafu.
Anapatikana Yangeyange – Msongola. Simu: 0655774967