DAR ES SALAAM
Na Dk. Felician Kilahama
Nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mambo mengi anayotutendea siku hata siku, ikiwa ni pamoja na zawadi ya uhai; hivyo kila mwenye pumzi na amsifu Mungu.
Tunapomkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere; kama angekuwa hai angetimiza miaka 100, maana alizaliwa mwaka 1922. Ni ukweli usiopingika kuwa walio wengi hawamfahamu vizuri na kwa undani huyu tunayemfanyia kumbukizi.
Kimsingi Mwalimu Nyerere ndiye aliyepambana, kwa nguvu zote, hadi tukawa na taifa huru. Desemba 9, 1961 bendera ya Waingereza iliteremshwa, tukapandisha ya kwetu ambayo inapepea hadi sasa.
Mwalimu Nyerere hakuishia kupata uhuru tu alikazana ili makabila zaidi ya 120 yawe jamii moja na kuwa na lugha moja kuwasiliana. Hivyo Kiswahili kikapewa kipaumbele sasa tunajivunia kuwa lugha ya taifa.
Vilevile, alituunganisha kupitia shule maalumu za sekondari ambazo zilipokea wanafunzi: Kidato cha kwanza kutoka mikoa yote. Mwaka 1968 wanafunzi watano walichaguliwa kujiunga na Kibaha Sekondari kutoka Mkoa wa Ziwa Magharibi (sasa Kagera), mimi nikiwa mmoja wao.
Hatua hiyo ililenga kuleta fikra za utaifa na kuimarisha Kiswahili kama lugha ya mawasiliano kwa makabila yote. Kadhalika, Aprili 24, 1964 Mwalimu na Sheikh Abeid Amani Karume (aliyekuwa Rais wa Zanzibar) wakakubaliana Tanganyika na Zanzibar zikaungana kukazaliwa taifa moja, Tanzania.
Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi shupavu na kupitia Chama tawala; Tanganyika African National Union (TANU); Februari, 1967 likapitishwa ‘AZIMIO LA ARUSHA’. Azimio hilo likawa dira na nguzo muhimu kujenga umoja kitaifa.
Sijui kama watu wengi wanalifahamu hilo Azimio? Tunapofanya kumbukizi ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere; kinachoshamiri zaidi ndani yangu: ni Azimio la Arusha na kujiuliza, je, bado liko hai na linatekelezwa ipasavyo? Azimio la Arusha liliainisha masuala ya msingi ya kiitikadi na kuweka sera sahihi kwa ajili ya ustawi wetu na taifa kwa ujumla.
Kupitia Azimio, masuala kama ‘Binadamu wote ni sawa na Africa ni moja’ yaliainishwa na hakuna sababu ya kumdharau binadamu mwenzako lakini pia kusisitiza kuwa bara letu ni moja, hivyo tuishi kama ndugu na kuheshimiana bila kuwapo fikra za ‘ubwana’ na ‘utwana’.
Pamoja na Azimio la Arusha kuliwekwa ‘miiko’ kwa chama na watumishi wa umma (Serikali). Miiko hiyo ililenga kuimarisha utawala bora na utumishi uliotukuka kwa kuzingatia uzalendo na uwajibikaji.
Mathalani, miiko kama: “Nitasema kweli daima, fitina kwangu ni mwiko”; “Sitatoa wala kupokea rushwa”. Kadhalika kulikuwapo na kanuni muhimu sana ambayo ilikataza watumishi na viongozi wa serikali na chama kutojihusisha na biashara.
Tunapofanya kumbukizi miaka 100 ya Baba wa Taifa; tujitathmini kwa undani zaidi ili tulipokosea turekebishe kwa faida ya Watanzania wote. Sijawahi kusikia kama Azimio la Arusha lilifutwa lakini kinachoeleka ni maudhui yake kudhoofishwa kwa faida binafsi tu.
Msingi wa utumishi bora uliotukuka, yaani wakuu wa serikali na watumishi wake kutojihusisha na biashara; ulifutwa kwa masilahi binafsi. Kwa bahati mbaya wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wanaifahamu fursa hiyo, hivyo wanaitumia ipasavyo pia kwa manufaa yao.
Kwa mtazamo wangu haikuwa muafaka kufuta kanuni ya kutenganisha biashara na uongozi wa umma au utawala bora. Utashi wa kisiasa wa aina hiyo haukuwa rafiki kwa maendeleo ya Mtanzania aliyezungukwa na changamoto lukuki za kijamii na kiuchumi.
Ni ukweli usiopingika kwamba kiongozi wa chama na serikali yake; hawezi akasimamia haki ipasavyo. Haiwezekani kutumikia ‘mabwana wawili’ kwa wakati mmoja lazima mmoja adhoofishwe na mwingine ashamiri.
Tunapoweka bayana kwa kusema miaka 100 ya Mwalimu Nyerere tujitathmini ipasavyo, je, tuko sawasawa kwa kufanya rejea kwenye misingi aliyoiweka ili kuwapo ‘siasa safi’ na ‘uongozi bora’?
Narudia, tutake tusitake ni vigumu kwa binadamu kusimamia utekelezaji wa Sera na Sheria ipasavyo; wakati huo huo akiwa ni mfanyabiashara yeye mwenyewe au kupitia watu wengine, ikiwamo ndugu na marafiki/wadau wa karibu naye.
Kwa vyovyote na falsafa hiyo ya kudhoofisha Azimio la Arusha na kufuta misingi imara ya uongozi bora; hapa kuna kulaliana kuliko kusimamia utekelezaji wa sera, sheria na kanuni ipasavyo.
Kuna kitu kinaitwa ‘mlipakodi’, lakini kiuhalisia mlipakodi mkubwa haumii sana kama ilivyo kwa walipakodi wadogo kupitia huduma na bidhaa wanazonunua. Wanalipa kodi wakati, wawekezaji na wafanyabiashara wananufaika kupitia ongezeko la bei.
Inatokea kwamba kwenye majukwaa matamko makali yanaweza kutolewa lakini ukifuatilia utekelezaji unaweza kukuta ni kinyume chake.
Mathalani, kwa nini tushindwe kudhibiti na kumaliza biashara ya dawa za kulevya? Inakuwaje migogoro ya wakulima na wafugaji ishamiri? Kiwanda kuchafua mazingira au wafanyabiashara kuficha bidhaa kama sukari, mafuta ya kupikia au ngano?
Haya ni baadhi ya maeneo ambayo viongozi wanaweza kujihusisha kirahisi na kunufaika kwa kutumia udhaifu uliopo katika maudhui ya utawara bora.
Tunapofanya kumbukizi ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere, ni vizuri tukafanya tathmini ya kina kwa kuangalia tumetoka wapi, tupo wapi na tunaelekea wapi? Wakati fulani Mwalimu alisema: “Uwepo wa mamilionea katika jamii yoyote si ushahidi wa mafanikio ya jamii husika.”
Kinachojiri hapa ni jinsi gani hao matajiri wamekuwa hivyo? Yawezekana ikawa kupitia udanganyifu, wizi, ufisadi, rushwa na kuhujumu uchumi kwa ujumla.
Moja ya misingi ya Azimio la Arusha ilikuwa kuwezesha taifa, kupitia serikali; ‘kusimamia sawasawa njia kuu za kuzalisha mali na kufuata siasa ambayo inawezesha taifa kumiliki kikamilifu mali/rasilimali zake’. Miaka 100 ya Mwalimu Nyerere je, hali ni hivyo?
Inawezekana si hivyo, lakini hapakosi ‘visababu’ vya kujitetea kama utandawazi na hatuwezi kuishi kama kisiwa, dunia ni moja na kadhalika. Ikiwa hali ni hivyo, tusijipime kwa kutumia vigezo ambavyo hatuna.
Mataifa yaliyoendelea si sawa na taifa letu, wako mbali sana, sisi bado tunakazana kujikwamua: umaskini, maradhi na ujinga pamoja na miundombinu. Mwalimu Nyeyere aliwahi kusema ‘wanapotembea sisi tukimbie’.
Sasa miaka 60 baada ya uhuru lakini bado tunahangaikia changamoto zilezile ikiwa ni huduma duni za kijamii: afya, elimu, maji, ugani katika kilimo, mifugo, misitu na maendeleo ya jamii.
Vilevile, miundombinu vijijini mathalani, barabara, umeme na umwagiliaji pamoja na sekta nyingi nilizozitaja zinahitaji miundombinu imara: bado ni kitendawili.
Tunapofanya kumbukizi miaka 100 ya Mwalimu Nyerere, ni vema kama taifa na watu wake kukawepo mjadala wa kitaifa, je, ni haki kwa watunga sera na wasimamizi wa sheria na kanuni zake kuwa sehemu ya wafanyabiashara?
Je, kwa kufanya hivyo wanatenda haki ipasavyo? Je, huo ndio mtazamo sahihi wa kuwapo siasa safi na uongozi bora? ‘Kumbuka mshika mbili moja humponyoka’.