Mhubiri mmoja wa Kiinjilisti nchini Marekani amewaomba waumini wake kuchanga pesa za kumsaidia kununua ndege yake ya nne.

Amesema hata kama Yesu angekuwepo siku hizi, “hangekuwa anapanda punda”.

Jesse Duplantis amesema Mungu amemwambia anunue ndege aina ya Falcoln 7X ambayo inagharimu $54m (£41m).

Ameongeza kwamba alikuwa na shaka pia kuhusu kuendelea na ununuzi huo mwanzoni, lakini Mungu alimwambia: “Sikukwambia uilipie. Nilikwambia uamini na utaipata.”

Ingawa si jambo nadra kwa wahubiri kumiliki ndege zao binafsi, ombi lake kwa waumini kuchangia limezua shutuma.

Watu kwenye Twitter wamepokea ombi hilo kwa mshangao, wengi wakinukuu aya kwenye Biblia zinazotahadharisha dhidi ya ulafi na “manabii wa uongo”.

Wengine wanasema pesa hizo zingetumika vyema kuwasaidia maskini.

Kwenye ujumbe wa video ambayo imepakiwa kwenye mtandao wake, Duplantis mwenye umri wa miaka 68 alisema: “Mwajua, nimemiliki ndege tatu maishani mwangu, na nimezitumia na kuchoma mafuta kwa ajili ya Bwana Yesu Kristo.

“Sasa, baadhi ya watu wanaamini kwamba wahubiri hawafai kuwa na ndege. Ninaamini kwamba wahubiri wanafaa kwenda kwenye kila redio (au kipaza sauti), kwenye kila chombo (cha habari), kuwezesha Injili kuenezwa kote duniani.”

Huku akiwa amesimama karibu na picha za ndege zake anazozimiliki sasa, mhubiri huyo alisema ndege aliyoinunua miaka 12 iliyopita kwa sasa haitoshi kwa utumishi na matumizi ya kanisa lake.

Alisema ni kwa sababu ndege hiyo haiwezi kusafiri mbali bila kutua, hiyo ikiwa na maana kwamba hulazimika kulipa pesa nyingi kutua ili kuiongeza mafuta.

Picha nyingine iliyooneshwa kwenye video hiyo ilimuonyesha mhubiri huyo akiwa amesimama na ndege hizo tatu, na juu ya picha hiyo maelezo: “Si kuhusu vitu unavyomiliki, bali vitu unavyovipa kipaumbele.”

Bw Duplantis ametetea ombi lake la kutaka kununuliwa ndege akisema Yesu aliwaambia wafuasi wake “nendeni kote duniani na mkahubiri Injili kwa kila kiumbe, sasa tutawezaje kutimiza hilo? Siwezi kuishi muda mrefu wa kutosha kusafiri kote kwa kutumia gari au meli au treni, lakini ninaweza kusafiri mbali kwa kutumia ndege.”

Mwaka 2015, Bw Duplantis alitokea kwenye video na mhubiri mwingine Kenneth Copeland, ambapo Bw Copeland alieleza kusafiri kwenye ndege za kibiashara, pamoja na watu wengine wa kawaida, kama kusafiri “katika mkebe mkubwa uliojaa mashetani.”