Gazeti la JAMHURI limepokea barua ya malalamiko ya askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Joseph D. Bundara (JB/MT 80304PTE), aliyomwandikia Rais ili asaidiwe kupata haki yake. Hii ndiyo barua aliyomwandika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…

Yah: Kurejeshewa malimbikizo ya mshahara, malipo stahiki na haki zote za mwanajeshi MT 80304KJ.

Mheshimiwa Rais, rejea kichwa cha habari hapo juu. Mtajwa ni askari wa JWTZ katika kikosi cha 711KJ, Kamandi ya Wanamaji (Navy).

Mheshimiwa Rais, naomba kurejeshewa mshahara, marupurupu na haki zote stahiki kwa askari mwanajeshi wa JWTZ. Mheshimiwa Rais, sijalipwa mshahara, marupurupu na haki zote stahiki tangu Mei 26, 2009 hadi leo.  

Kwa nyaraka za kughushi ambazo ni barua yenye kumb MMN 3042-1 JB/MT80304 ya Mei 26, 2009 iliyoghushiwa na Kamanda Kikosi 711KJ, Lt. Col. O. R. Shawa, iliyoambatishwa kama uthibitisho au ushahidi usioacha shaka juu ya kughushi huko kinyume na kifungu 333,335 (a) na (d) I na 338 vya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mheshimiwa Rais, katika barua hiyo inaonesha kuwa niliachishwa kazi jeshini kwa aya ya 8.01 kifungu cha 2(a) kuanzia Mei 25, 2009, kifungu ambacho hakimo katika juzuu ya kwanza ya utawala, kitabu kinachosimamia Sheria za Utawala Jeshini, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, naomba urejee mkuu.

Mheshimiwa Rais, nilipohoji kwa kuzingatia taratibu za kijeshi za kuwasilisha malalamiko ya wanajeshi kwa kuzingatia kanuni ya 12.26 ya sheria inayotoa haki kwa afisa au askari kuwasilisha malalamiko yake kwa wakuu pale anapoona hajatendewa haki, Navy Kamanda wakati huo, Meja Jenerali mstaafu S. S. Omary, alidai nilifikishwa katika mahakama ya Kamanda wa Kikosi 711KJ Mei 26, 2009, mahakama ambayo sikuwahi kufikishwa na inatofautiana na kifungu 2(a) alichotumia katika barua niliyoitaja hapo awali.

Mheshimiwa Rais, nilimwandikia barua ya kumjibu Navy Kamanda Julai 29, 2013 yenye kumb MMN/1295-1JB MT80304 PTE Joseph Bundara bila majibu. Niliendelea kufuatilia kwa mujibu wa sheria na taratibu kwa kumwandikia barua mwajiri Makao Makuu ya Jeshi, Wizara ya Ulinzi bila mafanikio kwani Kamanda huyo, Lt. Col. O. R. Shawa, alitumia madaraka yake kuhakikisha suala langu halipatiwi ufumbuzi, ndipo nilipomwandikia Wazairi Mkuu mnamo Novemba 5, 2013. 

Desemba 31, 2013 niliwasilisha malalamiko haya Ofisi ya Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, iliyetoa maagizo ya kutatuliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa suala langu kwa Col. Likangaa aliyekuwa DMP Makao Makuu ya Jeshi, lakini tulipofika Makao Makuu ya Jeshi Ngome, kinyume na maelekezo aliyopewa, yeye alimwagiza Capt. Kigopola na Koplo Theodory kunipeleka polisi na kunibambikia kesi ya uongo ili kuficha ukweli na kumlinda Lt. Col. Shawa pamoja na ofisi ya mwajiri CP.

Mheshimiwa Rais, nilifunguliwa kesi ya uongo ili nifungwe haki yangu ipotee. Kesi hii namba CD/RB/17313/2013, au CD/IR/4922/2013 katika  Kituo cha Kati Dar es Salaam, kwa kosa la kupatikana na sare za jeshi – JWTZ  nilizokuwa nimevaa kihalali kwa lengo la kupotosha nisipate haki zangu huku wakijua wazi kwamba mimi ni askari halali niliyekuwa nadai haki yangu kisheria.

Niliteswa sana kwa maelekezo kutoka 711KJ, Makao Makuu ya Navy, Makao Makuu ya Jeshi, nikiwa katika Kituo hicho cha Polisi Kati Dar es Salaam kinyume cha sheria za nchi na jeshi.

Mheshimiwa Rais, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kanda ya Dar es Salaam ilipotaka uthibitisho wa tuhuma hizo ili nifikishwe mahakamani, mwajiri JWTZ alishindwa kuthibitisha madai yake dhidi yangu kwani ni ya kughushi, hivyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilielekeza faili la kesi yangu polisi lifungwe, mimi niachiwe huru niendelee kufuatilia madai yangu dhidi ya mwajiri wangu kisheria.

Mheshimiwa Rais, pamoja na kuwasilisha tena madai yangu Ofisi ya Mwajiri, hakuna majibu yoyote ya kuridhisha niliyoyapata na  bado naendelea kutaabika hadi leo, huku makamanda hawa wakiendelea kufuja mshahara wangu kinyume cha sheria.

Mheshimiwa Rais, rejea barua ya Mei 12, 2015 kutoka kwa Navy Kamanda kwenda kwa Kamanda 711KJ, iliyoghushiwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwajiri – wameghushi tena kifungu 5(c) ambao ni mkataba, kiwe mbadala wa kifungu 2 (a) na wafanye mabadiliko ili ionekane nimestaafu kwa mkataba, kitu ambacho ni uongo.

Mheshimiwa Rais, ikumbukwe kwamba sijafikia umri wa kustaafu kwani nilizaliwa Juni 1978 na kujiunga na kisha kuajiriwa JWTZ Machi 4, 2002 Kunduchi Dar es Salaam, wala simo katika kundi la wastaafu wa mwaka 2009 katika kikosi cha 711KJ. 

Mheshimiwa Rais, nilipofuatilia Ofisi ya Mkurugenzi wa Malipo (DPA) Makao Makuu ya Jeshi, zilionekana pay slip mbili tu – ya Mei 2009 na Oktoba 2009, nyingine zote hazionekani kwenye mtandao kwa lengo la kupoteza ushahidi. Kama mshahara wangu ulisitishwa Mei 2009 kihalali, swali langu ni je, nani alikopa kwa kutumia pay slip yangu Oktoba 2009 katika duka la TMS NEW?(Tanzania Military Shop). Kamanda huyo atoe maelezo juu ya hilo na anilipe madai yangu.

Mbaya zaidi, kamanda huyo amewapa amri polisi jeshi wa Navy kunizuia nisiingie kambini tangu Januari 2016. Je, niende wapi kupata suluhisho la madai yangu? Naomba msaada wako Amiri Jeshi Mkuu.

Mheshimiwa Rais, nina imani na wewe na tatizo langu litapata ufumbuzi. Naomba nitendewe haki.

Wako katika ulinzi wa Taifa.

 

Bundara anapatikana kwa Na. 

0677 913 448