Mwishoni mwa juma lililopita, Rais John Magufuli, alipokea taarifa ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma wakati wa hafla iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma. Ropoti iliwasilishwa kwake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki.
Yaliyoibuka kwenye taarifa hiyo hayapendezi hata kidogo. Karibia watumishi wa umma 10,000 wameonekana kuwa na vyeti vya kughushi.
Aidha, wapo wafanyakazi 1,538 waliobainika kuwa na vyeti ambavyo vinatumiwa na mtumishi zaidi ya mmoja. Isitoshe, kuna watumishi wengine zaidi ya 10,000 ambao kumbukumbu zao zinaashiria kukosekana kwa vyeti vyao vya kidato cha nne, au cha sita, ingawa wamewasilisha vyeti vya taaluma kwa waajiri wao.
Akiwasilisha taarifa yake kwa Rais, Waziri alitamka kuwa kazi ya uhakiki ilihusu watumishi wa mamlaka za serikali za mitaa, taasisi, mashirika ya umma, tume, wakala za serikali, na serikali kuu ikimaanisha waajiriwa wa wizara.
Alidokeza pia kuwa uhakiki huo haukuhusisha mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, na madiwani; na akatetea kuachwa kwa kundi hilo kwa kutaja Ibara ya 67(1) ya Katiba inayoainisha kwamba sifa za msingi za kundi hilo la viongozi ni uwezo wa kusoma na kuandika.
Kwa matamshi yake hayo juu ya sifa za kundi hili la viongozi, waziri amewasha ‘moto’ katika kona mbalimbali za nchi akipingwa kwa aliyoyasema.
Wengi wa waliomkosoa wanahoji iweje viongozi waruhusiwe kuwa na vyeti vya kughushi ilihali watumishi hawapaswi kuwa navyo? Hakusema viongozi wanaruhusiwa kuwa na vyeti feki. Lakini ambayo hakuyasema yana uzito kama wa yale aliyosema.
Waziri angeishia tu kusema kuwa hadidu za rejea za kazi aliyoikamilisha haikuhusisha kundi hilo la mawaziri, wabunge, na madiwani. Utata umeibuka alipotetea hoja yake kwa kusema hao wanahitaji kujua kusoma na kuandika tu.
Waliomkosoa hawapaswi kuhoji sababu ya viongozi kuwekewa sifa ya kusoma na kuandika tu, hiyo ni kazi ambayo ingeambatana na hoja za kubadilisha Katiba. Wao wangepaswa kuhoji sababu ya hadidu za rejea kuacha kazi ya kuhakiki vyeti vya mawaziri, wabunge, na madiwani, na wakuu wa mikoa na wilaya.
Ziko sababu kadhaa kwanini ni muhimu kundi hilo nalo lihakikiwe. Nitataja mbili. Mosi, ni waziri mwenyewe ambaye alisisitiza kwenye hotuba yake kuwa kughushi cheti ni kosa la jinai. Moja ya majukumu ya msingi ya Serikali ni kusimamia raia kufuata sheria zilizopo, ikiwa ni pamoja na mtu kutumia cheti ambacho ni chake na si cha mtu mwingine.
Hawa watumishi wanaokaribia 10,000 waliobainika kutumia vyeti visivyo halali ni raia kama ambavyo wale viongozi waliyoachwa kwenye huu uhakiki ni raia pia. Sheria inapaswa kuwagusa raia wote bila kuwabagua.
Kwa hiyo, inaweza kuwa sawa kwa waziri kutamka kuwa uhakiki haukujumuisha vyeti vya kundi hilo, lakini haitakuwa sahihi kuacha hali hiyo hivyo hivyo kwa sababu Serikali itakuwa inasahau moja ya majukumu yake ya msingi ya kusimamia sheria.
Pili, ni kuwa kukamilika kwa uhakiki huu wa kundi hili lililosahaulika kutaimarisha kauli za viongozi wetu dhidi ya makosa yanayotendeka ndani ya jamii, ikiwa ni pamoja na desturi hii inayojengeka ya kughushi vyeti.
Sina shaka kuwa Waziri Angellah Kairuki ana vyeti halali vya masomo aliyosoma katika ngazi zote. Lakini hebu tutafakari kidogo iwapo angekuwa na vyeti visivyo halali, halafu kadamnasi yote ile aliyoihutubia pale Chuo Kikuu cha Dodoma, pamoja na Rais Magufuli, ikifahamu hivyo. Kwamba anayekaripia kosa, naye ni mkosaji hata kama hadidu za rejea hazikumhusu kwenye uhakiki huu. Ingekuwa ni jambo la kushangaza sana.
Lakini kushangaa huko hakuishii hapo tu, bali kunadhoofisha imani ya raia kwa viongozi wao, imani ya raia kwa serikali yao, na kunajenga uhusiano dhaifu kati ya Serikali na watu inaowaongoza.
Ni hivyo hivyo kwa Bunge na wabunge wetu. Bunge linapitisha miswada ya sheria na ni wajibu wa wabunge kuhoji sheria zinapokiukwa. Hivi karibuni Bunge limekuwa sehemu ambako baadhi ya wabunge wamehoji uhalali wa vyeti vya elimu vya kiongozi mmoja serikalini.
Wakristu kwenye Biblia, Mateo 7:1-5, wanaambiwa wasimhukumu mtu mwingine kabla ya kuhakikisha kuwa wao hawana kosa lile lile wanalohukumu. Naamini ni somo ambalo hata wasio Wakristu wanalikubali. Viongozi wote, pamoja na wabunge, ni watu ambao tunawachagua na ambao katika utekelezaji wa majukumu yao wanakosoa utendaji katika ngazi mbalimbali za Serikali na mamlaka za Serikali. Wanapomshutumu mtu kwamba hana vyeti halali ni vyema raia tuwe tumejiridhisha kuwa viongozi hao pia hawana hitilafu hiyo.
Hali hiyo itajenga imani ya raia juu ya mhimili huu muhimu na juu ya wale waliochaguliwa kuwakilisha wapiga kura.
Ni bahati mbaya sana kuwa tunaishi kwenye nyakati ambako masuala mengi ndani ya jamii, yawe yanahusu serikali au vyama vya siasa, yanapimwa kwa msingi wa jinsi gani suala lenyewe lina maslahi kwa chama tawala au chama ambacho hakiongozi Serikali. Ni desturi ambayo inawafumba watu macho kuchambua suala au uamuzi kwa maslahi ya wote. Na ikumbukwe pia kuna Watanzania wengi ambao si wanachama wa vyama vya siasa.
Sina hakika kuna viongozi wangapi ambao wataweka pembeni maslahi ya vyama vyao vya siasa na kuhakikisha kuwe yale masuala ya msingi yanasimamiwa vyema na yanalindwa.
Uhakiki wa vyeti, kwa ujumla wake, ni suala la msingi kabisa ambalo halipaswi kuingiliwa na malumbano ya mashabiki wa vyama vya siasa.
Suala la kuhakiki vyeti vya mawaziri, wabunge, na madiwani, na wakuu wa mikoa na wilaya ni suala ambalo naamini linapaswa kupewa uzito unaovuka maslahi ya vyama vya siasa. Likikamilika, litaongeza imani ya raia kwa viongozi wao, na kudumisha mshikamano. Tunauhitaji uhakiki kwa kundi hili la wanasiasa.