Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemfikisha mahakamani Mhasibu wa Wizara ya Afya, Yahaya Athuman (39) akishitakiwa kwa makosa 20 yakiwamo ya kughushi nyaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 34 zilizotolewa na serikali mwaka 2014 kwa ajili ya warsha kuhusu chanjo ya Rubela.
Mhasibu huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, mbele ya Hakimu Pamela Meena na kusomewa mashitaka 20 na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Samwel Kaaya na kurejeshwa rumande kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kutoa dhamana kwa makosa ya uhujumu uchumi yanayozidi thamani ya Sh milioni 10 hadi Mahakama Kuu.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani hapo, makosa tisa ni kughushi nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na hati za malipo kinyume cha Kifungu cha 22 (1) cha Sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007, makosa yanayodaiwa kutendeka kwa nyakati tofauti kati ya Okotoba Mosi hadi Oktoba 30, 2014.
Mshitakiwa huyo pia anakabiliwa na mashitaka tisa ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri baada ya kuwasilisha nyaraka za kughushi kwa ajili ya madai ya fedha, kuonyesha kuwa kiwango hicho cha fedha kilitumika.
Kosa la 19 ni ufujaji na ubadhirifu kinyume cha Kifungu cha 28(1) cha Sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007, ambapo mshitakiwa huyo anadaiwa kujinufaisha mwenyewe na kujipatia takriban Sh milioni 34.2.
Katika kosa la 20, mshitakiwa huyo anadaiwa kuisababishia hasara ya takriban Sh milioni 34.2 serikali, kinyume cha Sheria ya uhujumu uchumi aya ya 10(1) ya jedwali la kwanza na aya ya 57(1) na 60(2) sura ya 200.
Shauri hilo litaendelea tena Jumatano wiki hii ambapo upande wa mashitaka unatazamiwa kumsomea maelezo ya awali ya kosa kabla ya kesi hiyo kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Kabla ya mhasibu huyo kufikishwa mahakamani, Takukuru ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari na kueleza kuwa mwaka 2014 Wizara ya Afya iliendesha zoezi la chanjo ya Rubela katika halmashauri mbalimbali nchini ikiwamo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini.
Kwamba, Wizara ya Afya ilituma wahasibu katika maeneo husika kwa ajili ya usimamizi wa matumizi ya fedha hizo ambazo zilitengwa na wizara kwa ajili ya chanjo hiyo na kupeleka marejesho ya matumizi ya fedha hizo wizarani.
Taarifa hiyo ikafafanua kuwa, mshitakiwa huyo aliteuliwa kusimamia matumizi ya fedha hizo mkoani Kilimanjaro ambapo kiasi cha Sh 491,828,000 ziliingizwa kwenye akaunti ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RMO) zikiwa na maelekezo ya kumkabidhi mshitakiwa huyo ili asimamie matumizi ya fedha hizo katika halmashauri zote saba za mkoa huo.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, taarifa ya Takukuru inaeleza kuwa Sh 99,522,838 zilitolewa kwa ajili ya shughuli hiyo ya chanjo lakini uchunguzi wa taasisi hiyo ukabaini kuwa mshitakiwa huyo alifuja Sh 34,230,000.
Takukuru kupitia kwa Kamanda wake wa Mkoa, Holle Makungu, imeweka wazi kuwa uchunguzi wa matumizi ya fedha hizo za chanjo katika halmashauri za wilaya za Siha, Hai, Rombo, Mwanga, Same na Moshi Manispaa unaendelea na kuwaonya watumishi wa umma kuacha kuchezea fedha zinazotengwa na serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo.