Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mhandisi Anthony Sanga amekemea tabia ya baadhi ya watu kuita ardhi ya eneo fulani ni mali ya kabila fulani na badala yake amewakumbusha kuwa sera ya ardhi inatamka kuwa mali ya watanzania wote.
Mhandisi Sanga amesema hayo kupitia kliniki ya ardhi inayoendelea Jijini Arusha na kusema kuwa ni kosa kwa kabila lolote kuzuia mtu mwingine ambaye siyo kutoka kabila lao kumiliki ardhi yoyote kihalali kwani sera ya ardhi inatamka wazi kuwa ardhi ni ya watanzania wote.

“Mtanzania anaweza kukaa sehemu yoyote na kufanya shughuli zozote bila kuvunja Sheria, tabia hii tumeikemea jana na sisi kama wizara tutaendelea kukemea siku zote”
Amesema kupitia kliniki hiyo wamegundua wananchi wanajirudia kuleta malalamiko yao na kuwataka kuridhika na majibu wanayopatiwa.
“Kwenye haki ya ardhi kuna pande mbili, Kuna mtu ambaye anataka haki yake na kuna mtu ambaye haridhiki na majibu aliyopewa, kwa hiyo tunawasihi, wale ambao wanaambiwa hii siyo haki yako waridhike, wasimuone kiongozi mpya wakaanza kurudisha kesi hiyo hiyo upya”
Hata hivyo amewaambia wananchi hao kuwa zoezi linaloendelea halibatilishi hukumu ya Mahakama bali wao wanatoa ushauri na badala yake kama mtu ameona hukumu haijamtendea haki anapaswa kukata rufaa Mahakama ya juu.
Katika hatua nyingine Mhandisi Sanga amesema wamegundua kuwa mkoa wa Arusha pamoja na mikoa jirani wana migogoro mingi ya ardhi ya kifamilia iliyotokana na urithi.
Amesema wakazi wa mikoa hiyo wanajua thamani ya ardhi lakini pia kukosekana kwa upendo ndani ya familia kunachochea migogori hiyo na kwamba wao wanaendelea kutoa elimu kwa familia ili kuepukana na tatizo hilo.

“Migogoro hii inatokana na migawanyo ya urithi kwenye familia nyingi, lakini kikubwa ambacho tumekuwa tukiwasihi ni kuwa na uvumilivu na kupendana katika familia, jana tumesuluhisha migogori mingi lakini mengi ilikuwa ya kifamilia” amesema Mhandisi Sanga.
“Na migogoro hii mingi haijafikia kiwango cha kuwa kesi, bali ni kutoelewana miongoni mwao, utakuta mtoto mmoja haelewani na mwenzake au mzazi haelewani na mtoto” amesema Mhandisi Sanga.