Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Magama amesema kuwa nchi inahitaji uwekezaji zaidi wa mashamba makubwa ili kufungua fursa ya ajira kupitia kilimo kama ilivyokuwa kwa shamba kubwa la kahawa Afrika Mashariki la Aviv Tanzania Limited lililopo katika Kijiji cha Lipokela Wilayani Songea Mkoani Ruvuma lililoajiri watu zaidi ya 800.
Waziri Jenista Mhagama ameyasema hayo wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kahawa Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Lipokela Wilayani Songea Mkoani Ruvuma ambako liko shamba hilo lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 2000.
Maadhimisho hayo yameendana na maonyesho ya unywaji wa kahawa ambapo Waziri Mhagama amefurahishwa na ubora wa Kahawa ya Aviv ambapo amesema Tanzania inasomeka vema kwenye ramani ya dunia kwa kuwa na Kahawa bora.
Amesema Shamba hilo ni Muhimu kwa Taifa kwa kuwa limetoa ajira kwa Wananchi wa Mikoa mbalimbali nchini ikiwemo ya Ruvuma na Mtwara na kusaidia fedha za kigeni Nchini kwa kuwa wanauza kahawa yao moja kwa moja nje ya Nchi.
Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa Kampuni ya Aviv Tanzania Muthana Maruvanda amesema Kampuni hiyo kupitia Shamba lao la Kahawa imedhamiria kukuza zao la kahawa kwa miundombinu bora ya umwagiliaji ambayo Wakulima wa kahawa Mkoani Ruvuma wanajifunza kilimo cha kisasa kupitia Shamba hilo.
Nae Meneja wa Shamba la Kahawa la Aviv,Hamza Kassim amesema shamba hilo linachangia Asilimia 4.5 ya Kahawa yote inayozalishwa Nchini na wanazalisha kwa tija kubwa.
Mmoja wa Wananchi waliopata Ajira Shambani hapo Rose Choma anasema kupitia Shamba hilo anaweza kuishi vizuri na kusomesha Watoto wake ambapo anasema licha ya ajira waliyopata pia wamepewa miche ya kahawa kwa ajili ya kupanda kweye mashamba yao.