Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC, Juma Mgunda, yupo Jijini Tanga na timu yake ya Simba SC tayari kukabiliana na klabu ya Coastal Union ambaye ameinoa kwa muda mrefu kabla ya kujiunga na Simba SC ya Jijini Dar es Salaam.
Juma Mgunda anaijua vyema Coastal Union huku wachezaji nao wakiwa wanamfahamu Juma Mgunda na mbinu zake zote za ufundishaji. Kuelekea mechi ya kesho Jumamosi kocha Mgunda amekiri kuwa mechi dhidi ya Coastal Union sio mechi rahisi kwa kuwa Coastal Union ni washindani wa kweli.
Kwa upande wa kocha wa Coastal Union, Yusufu Chippo, yeye amesema kuwa kesho ni siku ya kuwafurahisha mashabiki wa Coastal Union baada ya matokeo yasiyoridhisha katika mechi za hivi karibuni.
Mechi kati ya Coastal Union na Simba SC itapigwa kesho katika Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga majira ya saa 10:00 Alasiri.