Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Musoma

Katika tukio la nadra, mgogoro ulioibuka kwenye familia ya marehemu Meja Jenerali Prof. Dk. Yadon Kohi, umesababisha kufukuliwa kwa mwili wake na kuzikwa upya katika kitongoji kingine.
Tofauti na mazishi ya awali yaliyopambwa na taratibu za kijeshi, safari hii amezikwa kimyakimya bila kuwapo mwanajeshi hata mmoja.

Meja Jenerali Prof. Dk. Kohi, alifariki dunia Aprili 02, 2023 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikokuwa akitibiwa.

Alizikwa siku chache baadaye kijijini kwa wazazi wake, Busegwe, Wilaya ya Butiama mkoani Mara. Mtanzania mwingine mashuhuri aliyezaliwa na kuzikwa Busegwe ni mwanasiasa na mwanasheria nguli, Nimrod Mkono.

Meja Jenerali Prof. Dk. Kohi anayetajwa kuwa mmoja wa wasomi wa hali ya juu kabisa ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alizikwa kwa heshima zote za kijeshi ikiwa ni pamoja na kupigiwa mizinga 17.

Hata hivyo, Desemba 22, 2024 kundi la watu waliokodiwa likilindwa na polisi wenye silaha na gesi za kutoa machozi, lilifika nyumbani na kubomoa kaburi lililosakafiwa kwa zege.
Hatua hiyo imetokana na mgogoro kati ya mjane wa marehemu, Thecla Kohi (73), na upande wa ndugu wa marehemu Meja Jenerali Kohi, wakiwamo kaka na dada zake.

Desemba 8, 2024 kibali kinachodaiwa kuwa kinatoka kwa Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mohamed Nahoda, kilitoa ruhusa ya kufukuliwa kwa kaburi hilo.

Kibali hicho kinasomeka: “Ofisi ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama imeridhia kuhamishwa kwa kaburi la marehemu ndugu Yadon Mtarima Kohi aliyezikwa katika Kijiji cha Busegwe, Kitongoji cha Mission na kuhamishiwa katika Kijiji cha Busegwe, Kitongoji cha Kunga. Naomba apatiwe ushirikiano katika kufanikisha zoezi (kazi) hili.”

Thecla alifungua shauri katika Mahakama ya Mwanzo Zanaki kabla ya shauri kupelekwa katika Mahakama ya Wilaya ya Butiama, na kupewa Na. 26421/2023.

Katika maombi yake ya Novemba 6, 2024, Thecla ambaye ni mkazi wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, anasema alifunga ndoa na Yadoni Kohi mwaka 1977 na wamefanikiwa kupata watoto wanne.
“Mume wangu alifariki dunia Aprili 2, 2023 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na alizikwa Busegwe Mission wilayani Butiama kwenye ardhi ya familia, ingawa wakati wa uhai wake alisisitiza azikwe katika eneo la ardhi alilonunua na kujenga makazi katika Kitongoji cha (Kunga) Isinuru kijijini Busegwe,” amesema kwenye kiapo chake.

Anasema kwa kuwa ndiye msimamizi wa mirathi, anaiomba Mahakama imruhusu afukue mwili wa marehemu mumewe na kwenda kuuzika Isinuru ambako ndiko kwenye makazi ya familia ya marehemu Meja Jenerali Kohi.

Ameeleza utayari wake wa kugharimia shughuli zote za ufukuaji, na mazishi mapya ya mwili wa mumewe.

Katika kuweka uzito wa shauri hilo, kuliambatanishwa hati ya maandishi inayodaiwa ni kiapo cha Esther Kohi (73), ambaye ni dada yake marehemu Meja Jenerali Kohi.

Hakimu Judith Semkiwa alikubaliana na maombi hayo na kutoa ruhusa ya ufukuaji na uzikaji upya wa mwili huo kama alivyoomba Techla.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Esther ambaye aliambiwa anatakiwa mahakamani, bila kujua alichoitiwa, anadaiwa kutotambua kiapo na maelezo yanayoelezwa kuwa ni yake, na kwamba yeye, kama walivyo ndugu wengine haafiki uhamishaji wa mwili wa kaka yake.

Hatua hiyo ilichochea na kuwaamsha ndugu wa Meja Jenerali Kohi na kuwafanya wajipange kuzuia utekelezaji wa hukumu hiyo.

“Siku ya kwanza walifika nyumbani wakitaka kufukua. Walikuwa na polisi kutoka Butiama, ndugu wakachachamaa na kuwafanya watu hao waondoke, lakini Jumapili wakaja na kundi kubwa la polisi kutoka Musoma na watu maalumu wa kuvunja kaburi. Wakautoa mwili. Walikuja na jeneza jingine jipya.

“Walianza kuvunja kaburi kwa nyundo huku wakilindwa kwa mitutu hadi walipomaliza. Lilikuwa tukio baya na la huzuni kwa sababu ndugu walianza kulia upya kana kwamba Jenerali ndiyo kwanza alikuwa amefariki dunia,” anasema mmoja wa majirani.

Upande wa ndugu haujaridhishwa na uamuzi huo, na tayari umekwenda Mahakama Kuu Musoma kufungua kesi ukilalamika kukiukwa kwa taratibu za ufukuaji na uhamishaji mwili; pia wakisema kitendo kilichofanywa ni cha kumdhalilisha ndugu yao na kwamba hakijawahi kufanywa kwenye ukoo wao na eneo kubwa la Butiama.

“Matukio haya tumezoea kusikia yakitokea kwenye ujenzi wa miundombinu, lakini si kwa kuhamisha mwili kwa aina hii, tena kwa mtu ambaye ni jenerali wa Jeshi,” amesema mmoja wa majirani.
Kauli yake inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kijiji cha Busegwe, Magori Nashoni, akisema kilikuwa kitendo cha kusikitisha.

“Ni masuala ya kifamilia. Ni mgogoro kati ya mke na watoto wa Jenerali kwa upande mmoja; na kaka na dada zake kwa upande mwingine. Kwa hiyo sisi kama serikali tulichokifanya na kuhakikisha na kusimamia amani, kazi tuliyoifanya kikamilifu,” anasema.

Nashoni anasema asingependa kuona hali kama hiyo ikijitokeza tena, akishauri jamii kujenga tabia ya kuandika wosia ili kuepusha migogoro kama hiyo.

Ofisa mmoja wa JWTZ aliyezungumza na JAMHURI kuhusu nafasi ya jeshi katika sakata kama hilo, alisema kwa ufupi:
“Jeshi kazi yake ni kuzika. Tukishamaliza hilo masuala mengine yanabaki kwa familia.” Kisha akakata simu.

Kwa upande mwingine, Msemaji wa Jeshi, Kanali Gaudentius Ilonda, alipotafutwa na JAMHURI siku ya Jumamosi iliyopita kuombwa kuzungumzia suala hilo, aliahidi kutoa majibu siku inayofuata, yaani Jumapili.Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni Jumapili jioni hatukupata jibu kutoka kwake.

WASIFU

Meja Jenerali Prof. Dk. Yadon Kohi alizaliwa Machi 29, 1949 katika Kijiji cha Busegwe, Kata ya Butuguri (sasa Kata ya Busegwe), Tarafa ya Makongoro, Wilaya ya Musoma (sasa Wilaya ya Butiama) mkoani Mara.

Alisoma Shahada ya Kwanza (LLB) na Shahada ya Uzamili (LLM) za Sheria kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Shahada ya Kwanza ya Udaktari wa Tiba (MB ChB) kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda na Shahada ya Uzamili ya Udaktari wa Tiba kutoka Chuo Kikuu cha Glasgow, Scotland.

Alikuwa daktari wa kwanza wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu (neurosurgeon) nchini Tanzania.

Profesa Kohi alikuwa na taaluma mahsusi katika utumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 30.
Alihudumu katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), akipanda cheo hadi kuwa Meja Jenerali.
Aidha, kwa miaka 14 kuanzia 1992 alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH); shirika la serikali lililobuniwa kwa ajili ya kukuza na kuendeleza utafiti wa kisayansi na maendeleo.

Pia ni Makamu wa Rais wa Mfuko wa Mtandao wa Malaria Afrika (Africa Malaria Network Trust) na ameshika nafasi za kufundisha katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Profesa Kohi alikuwa mwanachama wa Chuo cha Sayansi cha Tanzania (Tanzania Academy of Sciences) na Mjumbe wa Chuo cha Wataalamu wa Upasuaji cha Royal College of Surgeons cha Glasgow.

Pia amekuwa Mwenyekiti wa taasisi ya REPOA inayojihusisha na masuala ya utafiti, sera na uchumi.

Kadhakika amekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Afya Ifakara.
Profesa Kohi alikuwa mtaalamu mashuhuri katika nyanja za Sheria za Tiba, Matatizo ya Tiba, na Uzembe wa Kitiba.

Alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Mei 6, 1976. Alihudhuria kozi ya Afisa Mwanafunzi nchini Tanzania na kutunukiwa Kamisheni Novemba 20, 1976.
Meja Jenerali Kohi utumishi wake JWTZ ulifikia tamani na aliagwa rasmi jeshini pamoja na majenerali wenzake Agosti 17, 2011.

USULI

Sheria ya kufukua au kuhamisha maiti Tanzania inaongozwa na taratibu na sheria mbalimbali zinazolenga kuhakikisha heshima kwa marehemu na kuzingatia afya ya umma. Mchakato huo unahusisha kibali rasmi kutoka kwa mamlaka husika.

Vifungu kadhaa vya sheria vinavyohusika na mchakato huu ni:
Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16 Kifungu cha 128: Kinaeleza kuwa ni kosa la jinai kufukua maiti bila kibali halali kutoka kwa mamlaka husika. Adhabu kwa kosa hili inaweza kuwa kifungo cha hadi miaka saba.

Sheria ya Afya ya Umma, 2009 Kifungu cha 55: Kinaweka masharti kuhusu usimamizi wa makaburi na taratibu za kufuata endapo kuna haja ya kufukua au kuhamisha maiti ili kulinda afya ya umma.
Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Births and Deaths Registration Act), Sura ya 108 Kifungu cha 22: Kinaeleza utaratibu wa kupata kibali cha kufukua maiti kwa madhumuni ya uchunguzi au kuhamisha mwili kwenda eneo jingine.

Sheria ya Makaburi na Mazishi (Cemeteries and Burials Act), Sura ya 117 Kifungu cha 9: Kinafafanua taratibu za kuhamisha maiti kutoka kaburi moja kwenda jingine na mamlaka zinazohusika kutoa vibali hivyo.

Sheria ya Polisi (Police Force and Auxiliary Services Act), Sura ya 322 Kifungu cha 35: Kinaeleza wajibu wa Jeshi la Polisi katika kusimamia na kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa wakati wa kufukua au kuhamisha maiti.

“Ni muhimu kufuata taratibu hizi na kupata vibali husika kutoka kwa mamlaka zinazohusika kabla ya kufukua au kuhamisha maiti ili kuepuka uvunjifu wa sheria na kuhakikisha heshima kwa marehemu inalindwa,” amesema mwanasheria mmoja.