Mgomo wa madereva wa daladala na bajaji iliyokuwa ikiendelea katika jiji la Arusha na kushindwa kupatiwa ufumbuzi imedaiwa kumng’oa aliyekuwa Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini( LATRA) Mkoa wa Arusha, Amani Mwakalebela.

Imeelezwa kuwa ofisa huyo alishindwa kutatua migogoro hiyo na kusababisha usumbufu kwa wananchi, wafanyabiashara na wanafunzi kukosa usafiri leo.

Mwakalebela amepata uhamisho wa ghafla wakati bado sakata la mgomo wa daladala halijapoa huku Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela akiwa ameunda kamati ya usuluhishi juu ya mgogoro huo na kuja na majibu yenye tija.

Leo wakati ofisa mpya mwandamizi wa LATRA mkoani Arusha, Joseph Michael akitinga ofisini rasmi kuchukua nafasi ya Mwakalebela, daladala zimegoma tena na kusababisha shida kwa wananchi.

Akiongea na vyombo vya habari, Joseph Michael aliwataka wamiliki wa daladala katika kusitisha mgomo wao na kurejesha usarifi kwa kuwa mamlaka yao yameanza kutekeleza maoni ya kamati iliyoundwa na RC Mongela.

Alisema iwapo daladala zitaendelea na msimamo wa kutotii mamlaka ya kuwataka wasitishe mgomo mara moja, LATRA itafuta leseni zao kama sheria inavyotaka.

“Mimi nimeingia ofisini leo tulikutana na viongozi wa vyombo vya usafirishaji kwa lengo la kujitambulisha kama afisa mpya wa LATRA, na Leo nimejaribu kuzungukia baadhi ya maeneo ikiwemo ruti za daladala zaidi ya 145 ,mimi na wenzangu tupo katika hatua ya kutekeleza maoni ya kamati hiyo. ” alisema Michael

Kuhusu ofisa aliyekuwepo kuondolewa  ghafla katika kituo chake cha kazi Mkoani Arusha, alisema ni uhamisho wa kawaida haihusiani na mgogoro wa daladala na bajaj.