Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mgombea wa urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),Sweetbert Nkuba ameelezea namna ambavyo amejipanga kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo.
Moja ya mipango yake amesema ni kuboresha miundombinu ya TLS, uimarishaji wa miundombinu ya kisheria na kiteknolojia ili kuwezesha huduma bora kwa wanachama na jamii hususani kuongeza uwekezaji katika mifumo ya kidijitali ya kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma za kisheria na kuboresha ofisi za TLS katika mikoa mbalimbali kwa vifaa vya kisasa na miundombinu bora.
Jambo la pili anasema atasisitiza mafunzo endelevu kwa wanachama wa TLS ili kuhakikisha kuwa wanasheria wanakuwa na ujuzi wa kisasa na uwezo wa kushindana kimataifa ikijumuisha kuanzisha programu za mafunzo ya mara kwa mara kuhusu sheria mpya na mabadiliko ya sheria pamoja na kushirikiana na taasisi za kimataifa kwa mafunzo na kubadilishana uzoefu.
La tatu anasema atahakikisha TLS inakuwa na sauti yenye nguvu katika masuala ya kitaifa na kimataifa yanayohusu sheria na haki ikiwamo kuanzisha mikakati ya ushawishi kwa serikali na bunge ili kuboresha mfumo wa sheria nchini na kutoa msaada wa kisheria kwa jamii, hususani makundi yenye uhitaji maalum.
Nkuba anasema jambo la nne atasimamia kwa uwazi na uwajibikaji katika shughuli zote za TLS ili kujenga imani kwa wanachama na wadau wengine ikiwamo kuboresha mifumo ya ukaguzi wa ndani na nje ili kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali yake, kuanzisha utaratibu wa kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wanachama kuhusu shughuli na matumizi ya fedha za taasisi hiyo.
Pia, anasema jambo la tano atajenga na kuimarisha mahusiano na wadau mbalimbali, ikiwamo serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na taasisi za kimataifa pamoja na kuanzisha na kudumisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa ya kisheria kwa manufaa ya wanachama wa TLS na kushirikiana na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu katika kutoa elimu ya sheria na mafunzo ya vitendo.
Jambo la sita anasema ni kuhakikisha wanachama wa TLS wanashiriki kikamilifu katika maamuzi na uongozi wa chama ikiwamo kuanzisha mifumo ya ushirikishwaji wa wanachama katika maamuzi muhimu pamoja na kutoa fursa kwa wanachama wote hususani wanawake na vijana, kushiriki katika nafasi za uongozi.
“Kwa sera na mtazamo huu, ninaamini nitafanikiwa kuiboresha TLS na kuifanya kuwa chama imara na chenye ushawishi mkubwa katika sekta ya sheria nchini Tanzania,”anasema Nkuba.
“Naomba support yenu na kura zenu ili kujenga TLS moja, imara na huru ili kuhakikisha tunaondoa matabaka miongoni mwetu pamoja na kusimamia madhumuni ya TLS kama yalivyoainishwa kwenye kifungu cha 4 cha Sheria ya TLS, madhumuni na shabaha mbalimbali zilizopo kwenye mpango mkakati.”
Kadhalika, Nkuba anasema akichaguliwa kuwa rais wa TLS, ataanzisha mfuko wa malipo ya ada ya Mwaka kwa unafuu,
kuanzisha na kusimamia vituo vya malezi kwa mawakili wapya, pamoja na upatikanaji wa bima ya afya kwa utaratibu wa kulipa kidogo kidogo.
Nyingine anasema atasimamia kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa bima ya maisha kupitia makundi utakaosaidia familia ya wakili atakayefariki kulipwa sio chini ya Sh.milioni 100,000,000 ili kuondoa utaratibu wa kizamani ambapo familia hulipwa Sh.milioni 6,000,000 tu.
Nkuba anasema atahamasisha kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa lengo likiwa kuweka msingi wa kuanzisha taasisi kubwa ya fedha ya mawakili ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa inawakopesha mawakili.
Pia, anasema atahakikisha mahusiano yenye afya na wadau wote serikali, mahakama, Polisi na vyombo vyote, jamii na mawakili yanadumishwa na kuendeleza vita dhidi ya vishoka wa aina zote.
Nyingine anasema atashinikiza mabadiliko ya sheria zinazowanyima mawakili kazi na kuhakikisha suala la “local content” kwa kazi za sheria linazingatiwa katika mikataba yote ya uwekezaji, kutungwa kwa sera ya jinsia itakayotoa dira katika ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika uongozi wa TLS na nafasi za ajira na kuilinda na kuitetea taaluma hiyo na kuhakikisha inakuwa msemaji wa mawakili.