Kutokana na hali ya Yanga kuwa katika kipindi cha mpito hivi sasa, imeelezwa kuwa Katibu wa Baraza la Wazee ndani ya klabu hiyo, Ibrahim Akilimali, amepanga kufika Ikulu kwa Rais John Pombe Magufuli.

Taarifa imeeleza kuwa Akilimali amefunguka na kusema njia pekee ya Yanga kuepukana na hali iliyonayo kwa sasa ni kupata msaada wa Rais Magufuli ili kuikomboa iweze kurejea kama ilivyokuwa zamani.

Akilimali ameeleza kuwa Yanga haijaanza leo kuwa na migogoro bali tangu kipindi cha utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hivyo si kitu kigeni kinachotokea hivi sasa.

Aidha, Katibu huyo amesema alikuwa mtu pekee aliyepinga klabu hiyo kukodishwa na akieleza chanzo cha migogoro ndani ya timu hiyo kuanza kushika kasi kilianza kipindi hicho.

Mzee huyo amesema kwa sasa anafanya namna ya kuweza kukutana na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ili aweze kumfanyia mpango wa kukutana na Magufuli ambaye anaamini anaweza akawa msaada mkubwa kuisaidia Yanga.