Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ningependa kuchangia hoja ya ubinafsishaji. Kama kuna eneo ambalo nchi hii imeuzwa, kama kuna mchakato ulifanywa wa kuuza taifa hili basi ni mchakato wa ubinafsishaji.
Watu wamezungumza maeneo mengi sana kuhusu hasara ambazo tumezipata kwenye ubinafsishaji, lakini mimi nitatoa mfano mmoja tu wa Mgodi wa Chumvi Uvinza.
Huu mgodi ni mgodi ambao nimekuwa nikiufuatilia hata kabla sijawa mbunge. Mgodi huu una uwezo wa kuzalisha chumvi kwa miaka zaidi ya 800 kwa utafiti uliofanywa na Kampuni ya Ujerumani mwaka 1927.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgodi huu ulijengwa kwa fedha za Wataliano miaka ya wakati wa Uhuru, lakini umekuja kuuzwa kwa Sh milioni 900. Mwekezaji kauziwa mgodi huu kwa Sh. milioni 900, akalipa asilimia 10, yaani Sh milioni 90.
Mwekezaji yule akabadilisha ‘plant’ moja, si kubadilisha, akang’oa mitambo ya ‘plant’ moja ambayo inazalisha chumvi kwa kutumia umeme, akauza nchini Iran kwa thamani ya Sh bilioni 4.5. Amenunua kwa milioni 900, akaomba alipe asilimia 10 kwanza, lakini bado mitambo aliyoing’oa ameiuza nchini Iran kwa Sh bilioni 4.5.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii haiwezekani. Haya ndiyo mambo yanayowafanya watu walalamike. Haya ndiyo mambo yanayoongeza hasira. Kwa wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi kwenye mgodi ule kwa miaka 30 hadi 40, kuna waliolipwa mafao ya Sh 200,000.
Unaweza ukadhani maigizo, lakini kuna watu wamefanya kazi katika mgodi ule miaka 20, miaka 30 lakini wamelipwa kuanzia Sh 200,000 hadi Sh 1,200,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo mambo yanayotufanya tukasirike. Naomba kukazia Azimio la Kamati ya POAC kuwa tunahitaji mchakato wa ubinafsishaji upitiwe upya. Ni muhimu mikataba yote iwekwe hadharani, wekeni kwenye mitandao watu wawe wanasoma tu. Kama mikataba mmekwishakuingia, kuna sababu gani ya kuendelea kuifanya kuwa siri?
Mimi nimekwenda Ofisi ya Bunge kuomba wanipatie mkataba huu wa Mgodi wa Chumvi. Wakauomba serikalini, ikachukua muda kupatikana. Lakini hata ulipopatikana, ninausoma chini ya ulinzi. Mbunge, nasoma mkataba chini ya ulinzi, duuh!
Mheshimiwa Naibu Spika, hii nchi ni ya akina nani? Mimi nilidhani sisi wabunge ndiyo waamuzi wa nchi. Sasa inawezekanaje mimi mbunge, kama mimi mbunge nasoma mkataba chini ya ulinzi, hivi raia wa kawaida akitaka kuuona huu mkataba unaohusu rasilimali za nchi yake itakuwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba jambo hili liweze kutazamwa vizuri. Nchi yetu ina uwezo, tatizo kubwa na ugonjwa mkubwa tulionao ni namna ya kusimamia hicho kidogo kinachopatikana.
Mbali ya kushindwa kusimamia namna ya kukusanya, lakini hata hicho kidogo kinachopatikana tunashindwa kukisimamia? Kuna matumizi mabaya mno. Kijana anaingia serikalini, anafanya kazi miaka mitatu anajenga ghorofa.
Mimi nashangaa, mimi mbunge mbona hata nyumba sina? Watu wanafanya kazi Mamlaka ya Mapato (TRA) pale, miaka mitatu miaka minne, ni matajiri wakubwa; hawakusanyi kodi.
Nimewahi kuwaambia hapa wanatufanyia usanii kwamba wanaonyesha kwamba tunakadiria kukusanya kiasi hiki, halafu tumekusanya kiasi hiki, kwa hiyo tumezidi kwa asilimia hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba nchi hii haikusanyi kodi. Nimepata kuwaambia kwamba mwaka 2005 tulikuwa tunakusanya kwa mwezi Sh bilioni 260 wakati exchange rate ya dola kwa shilingi ya Tanzania ilikuwa Sh 1,000. Kwa sarafu iliyo imara kama dola, tafsiri yake ni kwamba mwaka 2005 tulikuwa tunakusanya dola milioni 260.
Lakini hadi sasa tunakusanya Sh bilioni 435, ukipeleka, ukiangalia kwa pesa za madafu utahisi kwamba tunakwenda mbele sana. Lakini ukipeleka kwenye sarafu iliyo imara kama dola unaona kwamba tulikusanya dola milioni 260 mwaka 2005, leo tunakusanya dola milioni 235 mwaka 2011/2012; kwa hiyo, bado kuna tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ningependa kuzungumzia suala zima la maana ya bajeti na Bunge. Bado Bunge hili, mchezo tunaoufanya wa kukaa hapa kujadili bajeti hauna maana yoyote.
Angalia mfano mmoja, Wizara ya Miundombinu (Ujenzi?) bajeti iliyopita – hii ambayo tunamalizia – walipitishiwa Sh trilioni 1.2. Hizi ni Sh bilioni 1,200 lakini hadi mwezi wa pili wamepewa Sh bilioni 380, na wakati wana madeni ya Sh bilioni 330.
Kwa hiyo, ni sawasawa na kwamba, hiyo bajeti yote haikufanya kazi yoyote isipokuwa ililipa deni tu. Sasa kuna maana gani ya kukutana kwa ajili ya kupanga bajeti kama mwenendo wa bajeti uko namna hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashauri kuwa ni muda mwafaka sasa tuanzishe Ofisi ya Bajeti ya Bunge. Bunge liwe na ‘Budget Office’ ambayo itamonitor. Isiwe kwamba tukishapitisha Mwaka wa Fedha, tunakuja kukutana tena mwaka mwingine wa fedha. Hii ni hasara kubwa. Kuna umuhimu wa kuwa na Ofisi ya Bajeti ikamonitor hatua kwa hatua kila siku… kila mwezi inakuwa inafanya ‘monitoring’ ya yale tuliyoyapitisha.
Inawezekana kabisa hapa tukifanya utafiti mdogo kwenye hizi wizara, ambazo tunakubaliana kwamba tulizipa fedha katika Mwaka wa Fedha uliopita, katika mwaka wa huu wa fedha ambao unakwenda kumalizika, kuna baadhi ya wizara utakuta zimepata asilimia 40, asilimia 30 nyingine asilimia 10, sasa maana ya kupanga ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha ipo. Hii nchi ina fedha. Haiwezekani nchi ambayo ni ya tatu kwa dhahabu katika Afrika, bado tujadili bajeti ya kasungura kadogo, haiwezekani.
Nchi ambayo ni ya 11 kwa mito mingi duniani, nchi ambayo kwa gesi inazidi kupaa, wanakadiria kwamba huenda miaka minane ijayo tukawa miongoni mwa nchi chache kabisa mbili au tatu kwa gesi nyingi duniani.
Inawezekanaje bado tunapanga bajeti za kimasikini? Hii ni nchi ambayo ilipaswa kuwa ‘a donor-country’ (nchi ya kufadhili nchi nyingine). Hii ni nchi ambayo tungekuwa tunatoa misaada kwa vinchi vidogo vidogo hivi ambavyo havina fedha.
Lakini leo kwa sababu ya uzembe wetu, leo kwa sababu ya kutokujali, Tanzania ni miongoni mwa nchi masikini sana duniani. Asilimia 45 leo ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wana uzito chini ya kiwango, wamedumaa kutokana na umasikini. Huu ni msiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna umuhimu kutazama upya nchi yetu. Hii ni nchi tajiri, bado ina nafasi ya kuwafanya hawa watu waishi maisha mazuri.