*Aingia Selous kuua wanyamapori
Raia wa Ugiriki, Pano Calavrias, aliyeghushi uraia wa Tanzania na kisha kuhukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, mwaka 2010 kwa kosa la kukutwa na hati ya kusafiria ya Tanzania kinyume cha sheria, yupo nchini akiendelea na uwindaji wa kitalii.
Pano anahifadhiwa na jamaa zake wa karibu, mmoja akiwa ni mfanyabiashara Ahmed Huwel mwenye biashara nyingi katika Jiji la Dar es Salaam na Iringa.
Mgiriki huyo amepata nguvu kubwa baada ya maofisa kadhaa wa Idara ya Uhamiaji kumlinda, kwa madai kwamba anaandamwa kutokana na mgongano wa kimaslahi na wafanyabiashara wengine.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Pano, aliyenyimwa kibali cha uwindaji wa kitalii kutokana na utata wake, kwa sasa anatumika kuwinda katika Pori la Akiba la Selous ndani ya vitalu M1, R1 na K4. Anatumiwa na kampuni ya Mkwawa Hunting Safaris.
Chanzo cha habari kimesema; “Anaingia Selous kama observer (mwangalizi), hana leseni ya Professional Hunter (PH). Ukiingia porini kwa kibali cha observer unalipa dola 100 kwa siku.
Ukiwa na leseni ya PH wa kigeni unalipa dola 5,000 kwa mwaka. PH wa Kitanzania analipa dola 1,000 kwa muda huo. Pia kuna shaka kama analipa hata hiyo dola mia moja kama observer kila anapoingia porini. Imebainika kuwa mara zote amekuwa akilipa dola hizo na anawinda kwa siku 21,” kimesema chanzo chetu.
Aidha, imebainika kuwa kampuni nyingi, zikiwamo anazojishughulisha Pano, hukata kibali cha wageni cha siku 21, na wageni huweza kuwinda na kumaliza shughuli zao ndani ya siku tatu au nne.
“Kibali kwa siku 21 ni dola 5,000. Kila mgeni kwa siku analipa dola 1,800 hadi dola 2,500. Hii inatakiwa kila mgeni au wageni wanapoingia walipiwe kibali cha 21 na hivyo kuingiza dola 5,000 serikalini; lakini kinachofanyika hapa ni kwa kibali hicho hicho kimoja cha siku 21 kutumika kuwindisha wageni hata kama watakuwa tofauti wanne ndani ya siku 21. Hii ina maana kwamba kama wageni wa safari nne ndani ya siku 21 wangelilipiwa kihalali, wangelipa dola 20,000; lakini kwa mchezo unaofanywa sasa ni kwamba kinacholipwa ni dola 5,000 tu,” kimesema chanzo chetu.
Katika Pori la Selous, Pano anajulikana, lakini amekuwa na ushirika wa karibu na askari wa wanyamapori.
Mmoja wa askari wanyamapori amezungumza na JAMHURI na kusema; “Wanaua sana wanyamapori. Anaweza kuja na wageni wenye kibali cha kuua pofu, nyati, na akawaua na asijaze. Keshokutwa anakuja na wageni wengine akaua pofu na nyati na akaandika ameua nyati. Impala wanaouawa ndiyo hawana idadi! Wenzangu (askari wanapewa hela), sifichi, hata mimi huwa napata.”
Pano, ambaye amekuwa akilindwa na viongozi kadhaa wakubwa nchini, anaishi jijini Dar es Salaam katika moja ya nyumba za Huwel iliyopo Masaki.
Kwa upande wake, Huwel ametafutwa mara kadhaa na JAMHURI kupitia simu yake ya mkononi yenye namba 0685 010101 lakini amekuwa hapokei simu wala kujibu ujumbe mfupi wa maandishi. Pano naye kupitia namba yake 0756 487318 amekuwa hapatikani. Baada ya hukumu ya mahakama, Pano aliuza baadhi ya kampuni na mali zake na kukimbilia Malawi.
Pamoja na kukosa sifa za uraia na kuendesha shughuli zake nchini, kwenye tovuti yake ya www.liontarihunters.com amekuwa akijinasibu kama ni Mtanzania halisi aliyezaliwa, kukulia na kuishi hapa hapa Tanzania kwa muda wote, na kwamba anamiliki kampuni ya Kiboko Hunting Safaris.
Hata hivyo, taarifa zilizopo ni kwamba alikwishaiuza kampuni hiyo na baadaye akaikimbia nchi. Anasema amekuwa PH kwa miaka zaidi ya 12 na kwamba aliwinda na kuua simba wakati akiwa na umri wa miaka 14.
Anatamba kuwa akiwa na umri wa miaka 19 aliweza kuua ndovu; anajitangaza kuwa mmiliki na mwendeshaji wa kampuni nyingine ya Liontari Hunters Co. Ltd inayoendesha shughuli za uwindaji wa kitalii katika nchi za Tanzania, Malawi na Zambia.
Pano ana historia ya kufungua kampuni na kuziuza. Kabla ya kuanzisha Kiboko Hunting Safaris alikuwa akimiliki kampuni iliyoitwa Voucher. Wakati huo Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori alikuwa Muhidin Ndolanga. Alipouza Kiboko alifungua kampuni nyingine ya Ndorobo ambayo nayo pia aliiuza. Baadaye alimiliki Liontari Hunters Co. Ltd.