Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mpwapwa
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mha.Felchesmi Mramba amesema kuwa tatizo la mgao wa umeme litakwisha ifikapo Januari mwaka 2024 baada ya mtambo mmoja wa kuzalisha umeme kutoka bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) kuanza majaribio ya kuzalisha umeme utakaoingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Mhandisi Mramba ameyasema hayo leo Desemba 20,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua kiwango cha maji katika chanzo cha kuzalisha umeme cha bwawa la Mtera lililopo Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma
Anasema kuwa Umeme utakaoingizwa ni megawati 235 ambazo zitasaidia kupunguza makali ya mgao kwani upungufu uliopo nchini ni kati ya megawati 250 hadi 300.
” Pamoja na kina cha maji cha bwawa la Mtera kutofikia kiwango kinachotakiwa cha mita 691 kwa ajili ya kuzalisha umeme lakini kiwango cha maji cha mita 690.4 kina uwezo wa kuzalisha umeme megawati 40 ambayo ni nusu ya uzalishaji unaotakiwa wa megawati 80″ amesema Mhandisi Mramba.
Mhandisi Mramba amesema kuwa wanategemea kina cha maji katika bwawa hilo kitaongezeka kuanzia Desemba 25 hadi 26 mwaka huu baada ya Mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA) kuwaathibitishia kutakuwa na mvua za kutosha kwenye Mikoa ya Iringa na Mbeya ambayo maji yake yanaingia kwenye bwawa hilo.
“Niwatoe hofu wananchi kuhusu mgao wa umeme kuwa utaisha ndani ya wiki tatu za kwanza za mwezi Januari mwaka 2024 kwa sababu pamoja na mvua kunyesha kwenye Mikoa hiyo lakini pia tutaingiza megawati 235 kwa majaribio ya mtambo mmoja kutoka bwawa la Mwalimu Julius Nyerere kwenye gridi ya Taifa,” amesisitiza Mhandisi Mramba
Aidha, Katibu Mkuu amesema kuwa upungufu wa umeme nchini utakuwa historia kwani mwezi machi mwakani tena zitaingizwa tena megawati 235 na kufanya jumla ya megawati 470 baada ya mtambo wa pili kuanza kufanya kazi na hivyo kuondoa uhitaji wa megawati 300 ambazo ndizo upungufu uliopo kwa sasa.
Pia Mhandisi Mramba amesema kuwa megawati 470 ambazo zitaingia kwenye gridi ya Taifa kutoka bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ni nyingi na zitamaliza mgao wa umeme na kuwa historia nchini kwani mkoa wa Dodoma peke yake unahitaji megawati 60 pekee.
Aidha amewaomba wananchi wawe wa uvumilivu wakati serikali ikijitahidi kuboresha huduma ya umeme na kwamba kila eneo litapata umeme kwa ratiba iliyopangwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Mhandisi. Gisima Nyamo-Hanga amesema kina cha maji kwenye bwawa la Mtera kimeongezeka kutokana na mvua zilizonyesha kwenye Mkoa wa Tabora na kuongeza ujazo wa maji kutoka mita 689.38 hadi mita 690.4 na mategemeo yao ni maji kuongezeka mvua zitakapoanza kunyesha kwenye Mikoa ya Iringa na Mbeya inayomwaga maji yake kwenye bwawa hilo.
Mhandisi Nyamo-Hanga amesema kuwa kina hicho cha maji kiliongezeka Desemba 2 mwaka huu na kuliwezesha bwawa hilo kuzalisha umeme megawati 40 ambayo ni nusu ya uzalishaji wake wa megawati 80 huku Kidatu likizalisha megawati 60 kutoka megawati 120.
Amesema kuwa bado wana matumaini kuwa mvua zikianza kunyesha kwenye Mikoa ya nyanda za juu kusini zitasaidia kujaza bwawa letu na hivyo tutamaliza kabisa mgao wa umeme nchini.
” Mvua za Pwani zinapeleka maji Bahari ya Hindi na vituo vya Mtera na Kidatu vinategemea mvua ambazo zinazonyesha Mikoa ya Iringa na Mbeya inayojaza Miti ya Ruaha Mkubwa na Ruaha Mdogo wakati Mto wa Kizigo unajanzwa na mvua za Tabora, Singida ba Dodoma.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa TANESCO , Aloyce Simon amesema kwa sasa Bwawa la Mtera linazalisha megawati 40 chini ya uwezo wake wa kuzalisha megawati 80.
” Maji haya yakisalisha umeme hapa yanaenda kuzalisha umeme katika kituo chetu cha Kidatu, hivyo kutokana na hali ya maji kuwa kina cha chini linazalisha megawati 40 yanaenda Kidatu na kuzalisha megawati 60 chini ya uwezo wa kituo hicho ya kuzalisha megawati 200.”
Awali, Kaimu Meneja wa Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera, Moses Holela amesema baada ya mvua kidogo kunyenya Kanda ya kati Bwawa limefikia kina cha chini cha mita za ujazo 690.4 juu ya usawa wa bahari ambapo kiwango cha wastani ni mita za ujazo 698.5 juu ya usawa wa bahari.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi.Felchesmi Mramba,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari leo Desemba 20,2023 mara baada ya kukagua kiwango cha maji katika chanzo cha kuzalisha umeme cha bwawa la Mtera lililopo Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi.Felchesmi Mramba ,akiwaonyesha waandishi wa habari hali ilivyo katika Bwawa la Mtera wakati wa ziara ya kukagua kiwango cha maji katika chanzo cha kuzalisha umeme cha bwawa la Mtera lililopo Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi.Felchesmi Mramba,akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Mhandisi. Gisima Nyamo-Hanga wakati akitoa maelezo kwa waandishi wa habari wakati wa ziara ya kukagua kiwango cha maji katika chanzo cha kuzalisha umeme cha bwawa la Mtera lililopo Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Mhandisi. Gisima Nyamo-Hanga,akiwaeleza waandishi wa habari mikakati ya TANESCO wakati wa ziara ya kukagua kiwango cha maji katika chanzo cha kuzalisha umeme cha bwawa la Mtera lililopo Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Kaimu Meneja wa Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera, Moses Holela,akielezea hali ya uzalisha katika Bwawa la Mtera baada ya ukaguzi wa kiwango cha maji katika chanzo cha kuzalisha umeme cha Bwawa la Mtera ukaguzi uliofanywa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati,Mhandisi Felchesmi Mramba na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),Gissima Nyamo-HangaDisemba 20,2023.
Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa TANESCO , Aloyce Simon, ,akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 20,2023 mara baada ya ukaguzi katika chanzo cha kuzalisha umeme cha bwawa la Mtera lililopo Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Muonekano wa Bwawa la Mtera