*Chadema waanza kuzunguka mikoani kufanya mikutano ya kuinadi ‘No Reforms, No Election’
*Butiku asema serikali haiwezi kuacha kufanya Uchaguzi Mkuu kwa sababu ya Chadema
*Ananilea asema muda unatosha wa kufanya mabadiliko madogo ya Katiba
Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Msimamo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi (No Reforms, No Election) umekuwa kama mfupa mgumu na unaibua mawazo mseto.
Ugumu wa msimamo huo unatokana na wasiwasi kwamba inawezekana madai yao yasitekelezwe kutokana na kile kinachokipiganiwa na chama hicho ikiwa imebaki miezi michache kabla Uchaguzi Mkuu haujafanyika Oktoba, mwaka huu.
Miongoni mwa madai yaliyosababisha chama hicho kuwa na msimamo huo ni kupinga mfumo wa uchaguzi kudhibitiwa na Rais, uharibifu katika mfumo wa majimbo ya uchaguzi kutokana na upendeleo na ukosefu wa haki ya kupiga kura.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, amesema serikali haiwezi kuacha hitaji la msingi la Watanzania la kufanya uchaguzi kwa sababu ya madai ya chama hicho.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na JAMHURI Dar es Salaam hivi karibuni, Butiku amesema madai ya Chadema kwa sasa hayana maana kwa sababu uchaguzi ni suala la kikatiba.
“Madai haya si issue, serikali yetu inatoka madarakani kwa hiari ya uchaguzi mkuu, reform ni hitaji la muda. Ukiwa na watoto wengi lazima ukubali lugha zao mbalimbali. No election maana yake nini?” Amehoji na kuongeza:
“Yaani tukae hatuna serikali au tukae na serikali ambayo yenyewe iko tayari kutoka, tungeweza kuwa na serikali haiwezi kutoka madarakani. Serikali yenye na majeshi yake inasema mimi tayari kutoka mwaka 2025. Wewe mwenye mashaka una sababu zako unadhani kuna rushwa kuna nini?
“Labda tutachagua serikali si nzuri ndiyo tunazungumza hivyo, lakini lazima tuwe nayo itakayosimamia reform. Huu ni utani kuzungumzia mabadiliko hayo wakati tuna miezi michache maana yake wanachosema serikali hii ibaki au kuna watu wana mawazo kwamba kuna utaratibu mwingine wa kuiondoa?”

Amesema mabadiliko ni hitaji la muda: “Mnaona lipo hitaji mnazungumza mnafanya, lakini haiwezi ikafanya mkavunja utaratibu wa msingi. Uchaguzi ni kitendo cha msingi, tunawapa watu nafasi ya kuchagua rais wao, sasa mashaka mashaka ndiyo tunayoyazungumza, Rais wetu amesema yasiwapo sababu zake zisiwepo tutii pamoja na ndani ya CCM, tutii wote lakini sasa isije tena ikawa tunaanza kuwa na mfumo ambao unavunja mambo makubwa.”
Vilevile amesema wananchi wapewe nafasi ya kuchagua viongozi wao na kama kuna matatizo yanatakiwa kuzungumzwa.
“Nadhani yapo matatizo ya kutosha lakini kuzungumza kutofanya uchaguzi, mimi maoni yangu kama mzee kabisa kabisa sijawahi kuona mna tatizo halafu mnataka liendelee, wale wanaodhani serikali haisikii, si tukubaliane safari hii muache madhambi hayo tuchague serikali halafu sasa tunaona tuna miaka mitano ya kuzungumza kwa sababu nchi haijengwi siku moja.
“Uchaguzi mkuu ni jambo la taifa, jambo la katiba na kisheria huwezi kuukataa kwa lugha nyepesi hivi, Watanzania tunajua uchaguzi upo tunajua tunakwenda kufanya uchaguzi,” amesema.
Pia amesema Watanzania wanajua hata ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuna kasoro kubwa na mengine yanataka lugha ya mabadiliko.
“Hata mama katika zile 4R imo ya kuvumiliana, tuchague halafu tutazama yale tunayotaka kusahihisha,” amesema.
Katika hatua nyingine, amesema kuna vyombo vya kusimamia masuala hayo na kamwe Watanzania hawawezi kwenda katika mabadiliko wakati kuna serikali isiyo halali.
“Serikali yetu inafikisha mwisho wake wa kutoka na lazima tuchague nyingine, tuchague kwa haki na ukweli tusisahau tulikotoka na misingi aliyotuwekea Mwalimu Julius Nyerere, tuache yale yote yaliyotuletea kasoro moja kubwa rushwa na kuibiana kura tuachane hayo na Rais wetu anasema tuache.
“Ndivyo nilivyokuwa nasema hivyo, kama una kiongozi mkubwa namna hiyo na sisi tunamsifu kabisa kwa dhati anasema jambo kubwa namna hiyo la maadili kama husikilizi wewe si mjukuu wake, kama unafanya mambo ya ovyo na yeye unajua anatujua,” amesema.
Amesema si wote wanamsifu Rais Samia Suluhu Hassan ni wala rushwa lakini umefika wakati wa kumpa muda wa kufanya kazi.
“Rais wetu unaweza kumtania hivi hivi katika mema usijaribu hata siku moja kumfanya mtani wako katika mambo ambayo hataki na wakati wote anasema msitende, safari hii tunataka kuona katika uchaguzi huu kuona ushahidi kuwa tumemsikiliza,” amesema.

Kwa upande wake, Mbunge wa zamani wa Busega, Dk. Raphael Chegeni, ameiambia JAMHURI kwamba msimamo wa Chadema ni sawa na ndoto kwa sababu haina tija.
“Changamoto zilizopo za kisiasa ni kawaida kwa sababu 4R za Rais Samia kuna watu wengine hawazielewi lakini ukifuatana na kuzingalia vizuri ndiyo maridhiano makubwa kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu. Hata wenzetu wa upinzani wana haki kwa sababu siku zote ni mtu ambaye haungi mkono kitu kilichofanywa na serikali iliyoko madarakani.
“Atakosa ajenda ya kuweza kufanya au kuwaambia wanachama wake kwa hiyo ajenda yao kubwa ni kupinga na kuonyesha kinachofanyika si sahihi, kwa maana hiyo tunasema kupitia 4R zikisimamia vizuri hakutakuwa na shida,” amesema.
Amesema msimamo wa Chadema unaonyesha wanataka kwenda kidikteta kuliko kidemokrasia hapa nchini.
“Tunaamini katika hatua za kukaa na kujadiliana, hoja walizonazo ziwe za msingi au laa ni kukaa na kuona kwa kipindi hiki kipi tukifanye tuweze kuendelea kwa sababu mazungumzo hayaishi leo au kesho mabadiliko hayaji siku zote Katiba au sheria huwa zinabadilika kila wakati kulingana na wakati uliopo.
“Nawashauri badala ya kupambana na kutokwa mapovu na no reform no election wangesema tukae tutengeneze mustakabali wa kitaifa tukubaliane tunatokaje hapo tulipo na waendelee kuzisoma na kuzielewa zile 4R na wakizielewa vizuri sioni kama kuna shida yoyote,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Dk. Ananilea Nkya, amewashangaa wanaosema msimamo wa Chadema hayatekelezeki kwa sababu muda uliobaki ni mfupi.
Akizungumza na JAMHURI wiki iliyopita, amesema Uchaguzi Mkuu ni shughuli ya Watanzania na lazima wakubali unavyoendeshwa huku akisisitiza kwamba suala la muda si jambo la msingi.
“Yapo matukio nchi inaweza kusogeza mbele uchaguzi kwa manufaa ya taifa. Wanaosema hivyo hawaitakii nchi mema. Lakini hakuna kusema eti muda hautoshi kama uchaguzi unafanyika Oktoba.
“Tunaojua thamani ya uchauzi tunaungana na Chadema na wote wanaoitakia mema Tanzania. Hakuna sababu yoyote kwa nchi kuendelea na uchaguzi wenye kasoro na wizi wa uongozi rasilimali unaopatikana kupitia sanduku la kura na hilo tumeshuhudia kwa miaka ya karibuni,” amesema.
Kwa sasa, amesema kinachotakiwa kufanywa ni mabadiliko madogo ya Katiba ili madai ya Chadema yaweze kutekelezwa.
“Kitu hicho kimesisitizwa na wadau mbalimbali wakati wa marekebisho ya zile sheria tatu mwaka jana. Muda uliopo unatosha endapo serikali ikikubali na muswada unapelekwa bungeni na madai hayo yatafanyika ikiwamo tume huru ya uchaguzi,” amesema.
Watinga kwa Msajili
Wiki iliyopita, Chadema imefika Ofisa za Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kumueleza msimamo wa madai yao unaokusudia kushinikiza mageuzi ya mifumo ya uchaguzi yasipotekelezwa wanapanga kuzuia uchaguzi usifanyike.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, amesema wamelazimika kwenda Ofisi ya Msajili kutokana na wito walioupokea hivi karibuni uliowataka kueleza wanamaanisha nini wanaposema ‘No Reform, No Election’?
Kupitia kikao hicho, amesema wameieleza ofisi hiyo kuwa kauli hiyo hawajaitoa kwa bahati mbaya kwa sababu kwa muda mrefu kumeshuhudiwa uchaguzi usiokuwa huru na haki na usioheshimu maoni ya wananchi wanayotoa kupitia masanduku ya kura.
Amesema mwarobaini wa yote hayo ni kufanyika mageuzi ya mifumo ya uchaguzi ikiwemo kupatikana na Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi lakini serikali haitaki kutekeleza.
“Chadema tunaamini baada ya kutuita na kuitikia wito wao, sasa Msajili anapaswa kuyachukulia kwa uzito ili na wao wawe na mchango kama wadau wengine tuliokutana nao, wa kuwezesha kufanyika kwa mageuzi na mabadiliko kabla ya uchaguzi mkuu. Tunaamini jambo hili linapaswa kukubalika na wadau wote,” amesema.
Pia amesema baada ya kikao hicho wanatarajia kukutana tena hivi karibuni kwa mazungumzo mengine lakini msimamo wao uko palepale na hautabadilika na wataanza kuzunguka kwenye maeneo mbalimbali ya nchini kuwaeleza wananchi kuhusiana na hilo ikiwamo kufanya vikao na mikutano ya hadhara.
Katika kikao hicho, Mnyika aliambatana na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Amani Golugwa, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) Wakili Ally Ibrahim, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Dk. Rugemeleza Nshala na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupi.
Wakati huohuo, Chadema Kanda ya Nyasa imetangaza kuanza kwa mikutano ya hadhara katika mikoa ya kanda hiyo kuanzia Machi 23, mwaka huu kwa lengo la kuwaeleza wananchi msimamo wa chama hicho.
Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, amesema mikutano hiyo itazinduliwa na Mwenyekiti wao Taifa, Tundu Lissu.
Amesema Lissu ataongoza mikutano ya hadhara na vikao vya ndani katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa huku Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche, ataanza mikutano hiyo Mbeya kisha Njombe na hatimaye kufunga Iringa kabla ya kuelekea kanda nyingine.
Katika mikutano hiyo, ajenda kuu itakuwa kuwaeleza wananchi umuhimu wa mabadiliko ya mifumo na sheria za uchaguzi ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unafanyika kwa haki, uhuru na amani.