Mkurugenzi mkuu wa wa sensa ya watu na jamii Ephaim Kwesigabo

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa takwimu tunazopawa kuzitumia
kutafakari hatima yetu kama Taifa.
Sasa inakadililiwa kuwa idadi ya Watanzania ni milioni 54.2. Mwaka 2021
idadi hiyo itapaa hadi kufikia watu milioni 59. Hili ni ongezeko kubwa.
Lakini imebainishwa na NBS kuwa kati ya Watanzania 100, watu 92 ni
tegemezi! Hii ni hatari kwa watu na kwa Serikali yenyewe.
Hatuna budi kuzitumia takwimu hizi kutafakari hatima yetu kama taifa,
kwani endapo mwenendo huu tutauacha uendelee, basi kuna hatari kubwa
ya kuyumba na hata kupoteza kabisa mwelekeo.
Utegemezi huu unaotajwa na NBS si jambo la bahati mbaya! Haya ni
matokeo ya mifumo yetu ya kielimu na kiuchumi tuliyoijenga.
Kwenye uchumi tumeamua kuwa taifa la wachuuzi. Nguvu kazi kubwa sana
imezama kwenye uchuuzi na hilo kundi sasa linaitwa ‘wafanyabiashara’. Leo
kila anayeamka anakwenda mjini kuchuuza. Bahati mbaya, tunavyochuuza
vinatoka ng’ambo! Tunaimarisha soko la nje. Tumekubali nguvu kazi
kubwa ya vijana izame kwenye udereva wa pikipiki tukiamini kwa kufanya
hivyo watakombolewa kiuchumi. Hili lingeweza kuwa na tija kama hizo
pikipiki zingekuwa zinazalishwa hapa hapa nchini. Hatuzalishi pikipiki wala
kipuri chochote cha hizo pikipiki.
Nguvu kazi hii ingejielekeza kwenye sekta za uzalishaji kama kilimo,
naamini mabadiliko yangeonekana haraka. Bahati mbaya kwenye kilimo
nako ni shida. Sasa nasikia wakubwa wanang’ang’ana mafuta ya mawese

yaondolewe ushuru wa asilimia 10 ili yaingizwe nchini bure! Wamejipanga
kweli kweli bajeti ijayo ushuru huo ufutwe. Vijana wangapi wanaolima
alizeti wataumia? Hili nitalijadili matoleo yajayo.
Hapa kwenye ‘kujielekeza’ kwenye kilimo kunaleta hoja ya pili ya elimu.
Tukubali kuwa kama Taifa hatujawa na mpango mzuri wa kuwapa vijana
elimu ya kuwakomboa. Tunasomesha ‘watumishi’ ndiyo maana hata pale
zilipotangazwa nafasi 70 za ajira Idara ya Uhamiaji walijitokeza vijana
15,000 kufanyiwa usaili ndani ya Uwanja wa Taifa! Hapa pekee palitosha
kutuamsha ili kutafakari aina ya elimu tunayowapa vijana wetu na hatima
yao na taifa lao.
Nchi haiwezi kujengwa na wahitimu wa vyuo vikuu – tena ambao wengi
wao wanasoma masomo ya sanaa! Kijana amesoma sayansi ya siasa
anapohitimu anakwenda kufanya kazi gani? Vijana wangapi wataajiriwa
kufanya siasa? Leo ndiyo haya ya ‘ajira’ mpya ya kuhama chama hiki
kwenda chama kile. Hakuna upenzi wala nini wala nini; ni kusaka ujira tu.
Miaka ile ya mwanzo ya Uhuru hadi miaka ya 1980 somo la elimu ya
kujitegemea lilipewa umuhimu. Wazee wa wakati huo walijua hakuna
muujiza wa kuwafanya vijana wote wa nchi hii wapate elimu ya sekondari
na vyuo vikuu. Walijua hilo haliwezekani. Walitambua kuwa wengi
wangeishia shule za msingi na kwa maana hiyo wangehitaji kupata elimu ya
stadi za kazi yenye kuwawezesha kuyamudu maisha nje ya mfumo rasmi wa
ajira.
Lakini hata hii elimu inayotolewa sasa si elimu ya kumfanya kijana msomi
ajione anaweza kushiriki kazi kama wafanyavyo Watanzania wengine. Kwa
mfano, kijana aliyehitimu shahada ya kwanza au ya pili ni ‘aibu’ kwake
kuonekana akilima au akifanya kazi za ‘kuuchafua; mwili. Wahitimu wengi
ni wale wanaoamini kuwa kazi zinazowafaa ni za kuajiriwa, tena za ofisini!
Kijana wa chuo kikuu hawezi hata kufuga kuku nyumbani. Si kwamba
hawezi kwa bahati mbaya, bali hawezi kwa sababu hakuandaliwa kubuni na

kuyakubali maisha ya ‘kutafuta’. Kwao, kazi za maana ni za ofisini. Hili si
kosa lao. Ni kosa la mfumo wetu wa elimu uliowaandaa kuwa hivyo
walivyo.
Tunao vijana wengi wanaohitimu masomo ya kilimo, ufugaji na hata uvuvi.
Je, ni wangapi walioajiri? Japo ni ukweli kuwa kujiajiri kunahitaji mtaji, bado
hii si hoja ya kuwafanya washindwe kujiajiri. Kitu muhimu kabisa ni
dhamira; na kinachofuata ni mbinu au malengo ya kufikia hiyo dhamira.
Kama kijana anakosa elimu ya kumsaidia kujitambua mapema kuwa kujiajiri
ndiyo suluhisho la maisha yake, huyo hata kama akipewa mtaji bado
atapenda aache – aende kuajiriwa.
Hapa ndipo Serikali inapopaswa kupatazama kwa jicho la kurekebisha.
Nilipata fursa ya kuzuru Misri. Kule nilikuta Serikali imeweka utaratibu wa
kuwahamasisha vijana kuingia kwenye kilimo. Ilichofanya ni kuandaa
mashamba kwa kurutubisha ardhi, kujenga nyumba na kuweka
miundombinu yote ya kilimo (maji). Kijana alikopeshwa idadi ya ekari
alizohitaji na akatakiwa azalishe kwa miaka 15 hadi 20 ndipo aanze
kurejesha mkopo wake bila riba! Mpango huo (sijui kama bado upo)
uliwavuta maelfu ya wahitimu wa vyuo vikuu kujiunga kwenye kilimo. Misri
ni mzalishaji na msindikaji mkuu wa matunda yanayouzwa Ulaya na
kwingineko duniani.
Hapa kwetu ni tofauti. Wanasiasa badala ya kuwaza na kutenda mambo
makubwa na mazuri ya aina hii kwa vijana wetu, wao wameona ukombozi
ni kuwapa bodaboda! Huwezi kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii
au taifa kwa kuwa na madereva wa bodaboda! Tusijidanganye.
Hapo hapo kwenye elimu kuna mahali tunakosea. Kama taifa
tumejiaminisha kuwa ni sifa kuwa na wahitimu wengi sana wa vyuo vikuu!
Tunashangilia tunaposikia Serikali imetenga shilingi zaidi ya bilioni 400 kwa
ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Sipingi kuwa na wahitimu

wengi wa vyuo vikuu. Ninachokosoa ni kuamini kuwa hawa ndio
wakombozi wa uchumi wa taifa letu. Hili ni kosa kubwa.
Nguvu hii inayoelekezwa vyuo vikuu inapaswa ielekezwe kwenye vyuo vya
ufundi stadi (VETA) nchini kote. Tunapaswa kuzalisha mafundi mchundo
wengi kuliko wahandisi. Barabara yenye urafu wa kilometa 100 inaweza
kusimamiwa na wahandisi watatu, lakini mafundi mchundo wanaweza
kuwa zaidi ya 500! Hii ni kada muhimu.
Mataifa ya Asia kama vile Korea, Japan, China, Malaysia, Indonesia na
mengine mengi, yameendelea kwa sababu ya kuitambua na kuithamini kada
hii. Nchi haiwezi kupiga hatua kwa kupuuza au kutoipa kipaumbele kada ya
VETA. Hapo ndipo wanapopatikana mafundi na wabunifu wengi
wanaotakiwa kubuni na kutengeneza vifaa mbalimbali kwa mahitaji ya
binadamu ya kila siku.
Serikali ikiwekeza kwenye utafiti katika kada hii itakuwa imefanya jambo
lenye manufaa makubwa mno kwa jamii na kwa taifa zima.
Napendekeza tuwe na mjadala mpana wa kitaifa wa aina ya mfumo wa
elimu unaoifaa Tanzania ya leo na ijayo. Mfumo wa elimu usitokane na
utashi wa waziri au viongozi wa awamu fulani. Tunakosea kuona leo waziri
huyu anasema tufute michezo, kesho anakuja mwingine anafuta masomo ya
biashara, n.k. Hatuwezi kuendelea kwa staili hiyo.
Watanzania kwa umoja wetu tujadiliane na mwishowe tupate jawabu
linalotokana na uamuzi wa wengi la aina ya elimu inayolifaa taifa letu.
Tujadili kwa kupima umuhimu wa elimu – ya VETA au ya vyuo vikuu na
ikiwezekana tuamue uwiano wa mikopo kwa wasomi wa ngazi zote hizo.
Ninachojadili hapa ni kama jeshini. Jeshi la ushindi ni lile lililo na askari wa
kawaida na maofisa wa chini na wa kati wa kutosha. Huwezi kuwa na jeshi
ambalo idadi kubwa ya wanajeshi wake ni majenerali halafu ukatarajia
ushindi.

Wala huwezi kuwa na vyuo vingi kwa ajili ya kufundisha maofisa, lakini
ukapuuza kuwa na vyuo vya aina hiyo kwa ajili ya kuwaandaa wapiganaji ili
wapate mbinu na weledi wa kumshinda adui.
Vivyo hivyo, huwezi kuwa na wahandisi wengi, lakini ukapuuza kuwa na
mafundi mchundo. Kwa maana hiyo nawaomba watunga sera watazame
namna ya kuwekeza zaidi VETA. Huko ndiko waliko vijana wengi ambao
kwa ujuzi watakaopata wataweza kuyabadili haraka kabisa maendeleo ya
nchi yetu.
Tuwe na mitaala ya elimu –kuanzia shule za awali/msingi- yenye
kuwajengea watoto ari ya kujiajiri wakingali wadogo. Wajengewe jeuri ya
uthubutu. Tuwajenge kiakili waamini na wajione kuwa wajibu wao
wakishahitimu masomo ni ‘kutengeneza’, na si ‘kutengenezewa ajira’.
Katika mjadala huu, yooote haya tunayoyajadili hapa hayatakuwa na tija
endapo suala la uzazi wa mpango halitazingatiwa. Wachumi wanaamini
wingi wa watu ni moja ya nyenzo njema katika kujiletea maendeleo. Hata
hivyo, idadi ya watu isiyoshabihiana na ukuaji uchumi wa familia, jamii na
taifa lolote; ni janga. Ni kama kujenga paa zito la vigae juu msingi
ulioshikwa kwa mabua! Hilo jengo litaporomoka tu.
Ongezeko la idadi ya watu halina budi liwe na uwiano na ukuaji uchumi.
Ilivyo leo ni kwamba Watanzania tunazaliana tu bila kuwa na mipango ya
kuhudumia hao wanaozaliwa.
Nawapongeza NBS kwa kutukumbusha sababu za ‘mkwamo wetu’. Utafiti
wao utusaidie kujipanga vizuri kukabiliana na hali inayotukabili sasa na kwa
miaka ijayo. Muhimu ni kuwa tunahitaji mapinduzi makubwa kuanzia
kwenye fikra zetu (mindset) na kwa hakika tunapaswa kuwa na mjadala wa
pamoja wa aina ya elimu tunayopaswa kuwapa watoto wetu ili kuondokana
na huu mzigo wa watu 8 kuhudumia watu 92! Kwa pamoja tutashinda.