Na Mwandishi Wetu, WHMTH ar es Salaam
Mratibu Msaidizi wa Mfumo wa Anwani za Makazi, Arnold Mkude amewatoa hofu wananchi kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi NaPA kusomana na mifumo mingine akibainisha kwamba hilo ni jambo lililozingatiwa tangu awali na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati wa kuunda mfumo NaPA.
Amesema hadi sasa NaPA inasomana na mifumo mingine ya utambuzi ukiwemo wa TAUSI ulio chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI na ILMIS unaosimamiwa na Wizara ya Ardhi.
Mkude amesema hayo leo Julai 05, 2024 wakati akifafanua masuala mbalimbali kuhusu Mfumo wa NaPA, umuhimu wake kwa jamii na namna unavyofanya kazi kwenye kipindi cha Joto la Asubuhi kinachorushwa na kituo cha Radio cha EFM katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Viwanja vya Mwalimu Nyerere Kilwa Road jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa pamoja na mambo mengine lengo la mifumo hiyo kusomana ni kusaidia kuepusha uwezekano wa kutokea kwa migogoro ya Ardhi na kwamba hakuna Anwani ya Makazi inayotolewa kwenye eneo lenye mgogoro.
Mkude amewataka wananchi kupakua programu Tumizi ya NaPA inayopatikana katika Playstore na Appstore ili kupata na kutumia taarifa za Anwani za Makazi kirahisi , iwe ni nyumba ya kuishi, ofisi au Biashara pamoja na kupata maelekezo ya namna ya kufika eneo analokwenda.
“Ni muhimu kuwa na mfumo wa NaPA kwa sababu unarahisisha maisha hususan shughuli za utambuzi, na kutumia Mfumo huu ni muendelezo wa juhudi za pamoja za kutangaza na kulinda mifumo yetu ya ndani. Ni mfumo unaomsaidia mwananchi kujua namba ya nyumba yake, mtaa wake na Postikodi ya Kata yake, na hii inatuwezesha kutambuana kwa usahihi na hata ukimuelekeza mtu anafika mahali sahihi bila usumbufu wa aina yoyote,” amesisitiza Mkude.
Akifafanua kuhusu vigezo na masharti vinavyotumika kutoa majina ya mitaa, mmoja wa Maafisa kutoka Wizara hiyo, Innocent Jacob amesema majina yote ya mitaa yametolewa na Wananchi wenyewe kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa kwa kuzingatia Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi.