Tot ADP
‘Female Circumciser Lays Down Her Tools’ Before downing her tools, this circumciser, Divinah Murkomen, aged 50 circumcised 500 of the 800 girls circumcised in Marakwet District in December 1999. She put down her tools – a knife and a razor blade — at the encouragement of NGOs like World Vision, who enlightened her on the myriad hazards associated with FGM.
Female circumcision is a deeply rooted cultural practice in Kenya. World Vision Kenya has developed an alternative initiation ceremony that maintains the important period of older women sharing their knowledge and advice with the young girl, without genital mutilation taking place. For twenty years, the women of the Tot region in Kenya have called on Divinah Murkomen to circumcise their daughters. Now Divinah has renounced her trade and insists her two younger daughters will not be circumcised.
Africa
color
horizontal

Watoto wa kike wanalazimishwa kuolewa

  • Sheria za kimila zinawabeba wanaume

 

NGORONGORO

NA ALEX KAZENGA

Kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika jamii ya Kimaasai kunachochea ukeketaji watoto wa kike katika jamii hiyo wilayani Ngorongoro, Arusha.

Chanzo cha kuota mizizi kwa mila hiyo kinatajwa kuwa ni mfumo dume unaotawala katika jamii hiyo.

Sheria za kimila za Wamaasai zimeruhusu mwanaume kuoa wanawake zaidi ya watatu kulingana na uwezo wa mali alizonazo.

Baadhi ya wazee huanza kuwachumbia watoto wa kike wakiwa na umri mdogo unaoanzia miaka 9 hadi 12, au pengine chini ya hapo.

Kutokana na sheria ya kimila kuwataka wanaume kutooa wanawake ambao hawajakeketwa, wazazi kulazimika kuwakeketa watoto ili iwe rahisi kupata  waume.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Kitengo cha Afya, katika Hospitali ya Wasso, Rashid Hussen, anasema vitendo hivyo huwanyanyasa watoto kwa kuwalazimisha kufanyiwa ukeketaji, kuchaguliwa wanaume na kuozeshwa kwa nguvu wakiwa wadogo.

Katika Kata ya Olorien wilayani humo, JAMHURI limeambiwa kuwa kwa miaka miwili iliyopita (2016 na 2017), wasichana 89 wenye umri kati ya miaka 13 hadi 17 walilazimishwa kuolewa.

Takwimu kutoka Hospitali ya Wasso zinaonesha kuwa kati ya hao, ni wasichana saba pekee waliolazimishwa kuolewa bila kukeketwa.

Wasichana 82 ambao ni sawa na asilimia 92.1, waliolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18 na wakiwa wameshakeketwa.

Hata hivyo, mila hizo zinapingwa kisheria kwa kuwa zinakiuka haki za watoto na haki za binadamu kwa ujumla.

Sheria zinazomlinda mtoto zinahesabu vitendo hivyo vya kimila kuwa kosa na zinatoa adhabu tofauti tofauti huku baadhi ya sheria zikionekana kutoa adhabu ndogo.

Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 kifungu Na. 13 kifungu kidogo Na. 1 inaeleza kuwa kitendo chochote cha kikatili kwa mtoto na kile kinachompunguzia utu wake, anayekutwa na kosa hilo kwa vitendo hivyo adhabu yake ni faini ya Sh milioni 5 au kwenda jela miezi isiyozidi sita; au adhabu zote kwa pamoja.

Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 imeainisha kuwa mwanaume anayejamiiana na binti mwenye umri chini ya miaka 18 anahesabika kutenda kosa la ubakaji ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.

Sheria hiyo pia imetaja kuwa ukeketaji ni kosa la jinai kwa sababu ni kitendo cha kikatili kinachomsababisha binti kukatwa sehemu za siri kinyume cha matakwa yake.

Ukatili huo adhabu yake ni kifungo jela miaka 15 na faini ya Sh 300,000; au vyote kwa pamoja kwa anayeweka mazingira ya mtoto wa kike kutendewa ukeketaji.

Wakili wa Kituo cha Sheria cha Moriah Law Chambers, Justine Kaleb, anafafanua kuwa sheria inapotoa adhabu tofauti mara nyingi adhabu iliyo juu zaidi ndiyo inayochukuliwa kumwadhibu aliyetenda kosa.

Anasema sheria huwa inatoa hukumu katika namna tatu – kulipa faini peke yake, kwenda jela, au vyote kwa pamoja kutegemeana na utetezi wa mshitakiwa.

Chini ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998, kulipa fedha kwa ajili ya kumpata mtoto kwa lengo la kufanya naye ngono imetajwa kuwa ni kosa la unyanyasaji wa kijinsia kwa mtoto wa kike.

Mkataba wa Afrika wa kulinda haki na ustawi wa mtoto ambao Tanzania imeuridhia mwaka 2003 unapiga vita mila na tamaduni potofu za Kiafrika zinazoathiri ustawi, utu na maendeleo ya mtoto.

Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Charles Mlaki, anasema baadhi ya jamii ya Wamaasai kutokana na kukosa elimu haioni kama vitendo hivyo ni makosa kisheria.

Anasema mfumo dume unachangia watoto wa kike kufanyiwa vitendo hivyo bila hatua zozote za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahusika kwa sababu wanaume hulindana, na wanawake hawapewi nafasi.

“Mwanamke akishitaki kwenye vyombo vya dola, wazee wa kimila watamtenga, na hivyo kuonekana kama hana heshima,” anasema Mlaki.

Daniel Killel, Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la kupinga ukeketaji wilayani humo (KIDUPO), anasema wanaume wanachangia ukeketaji kuendelea kwa sababu hawataki kuoa wanawake ambao hawajakeketwa.

“Haipo namna mwanamke anaweza kujikwamua katika utaratibu huo, hata akijitoa muhanga na kwenda kushitaki nje ya vikao vya kimila anaweza kutengwa ama kutozwa faini,” anasema Killel.

Kwa upande mwingine, wanaume ndiyo wanaoongoza kuwasema vibaya wasichana ambao bado hawajakeketwa kwamba ni wachafu na wananuka.

Kutokana na hali hiyo, wasichana wengi wamejikuta wakilazimika kufanyiwa ukeketaji ili kuondoa dhana hiyo ya uchafu na kunuka.

Mkazi wa Kijiji cha Oldonyo- was [jina kamili tunalihifadhi], ambaye amekeketwa anasema, “Morani wanaokaa katika boma la manyata wanaongoza kwa kuwachukia wasichana ambao hawajakeketwa wakiamini kuwa ni wachafu.”

Manyata ni boma wanalokaa vijana baada ya kutoka jandoni kwa ajili ya kufundishwa mila na utamaduni wa Kimaasai.

Kutokana na hali hiyo, wasichana hulazimika kukeketwa ili kupunguza chuki na dharau wanayokumbana nayo kutoka kwa morani.

Mkazi wa Wasso, Steve Laizer ambaye ni morani, anasema kuwadharau wasichana ambao hawajakeketwa ni kasumba waliyorithi kwa wakubwa wao, na pia ni ukosefu wa elimu ya maumbile ya mwanamke.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Olorien, William Palapala, anasema wanasiasa wanapaswa kushiriki kukomesha ukeketaji.

Anawashutumu kwa kujipendekeza na kuwasaliti kwa wananchi watu walio mbele kupinga ukeketaji, na hivyo kusababisha chuki kwenye jamii.

Naye, Gagi Didiah, ambaye ni Ofisa Mtendaji Kata ya Olorien, anasema wameanzisha utaratibu wa kuwakagua watoto wa kike hasa kipindi cha kufunga shule na wakati wa kufungua shule ili kubaini waliokeketwa wakati wa likizo.

“Tumedhamiria kutokomeza vitendo vya ukeketaji, wasichana watakaobainika kukubali kukeketwa kipindi cha likizo wazazi wao tutawapeleka kwenye vyombo vya sheria,” anasema Didiah.

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Arusha, Ramadhan Ng’azi, anasema tangu mwaka jana hakuna kesi au tuhuma za ukeketaji zilizofikishwa Kituo cha Polisi Loliondo.

Anasema licha ya ukeketaji kufanywa kwa siri, polisi wamejipanga kuwabaini wataribu wa vitendo hivyo.

Anawaomba wasamaria wema kujitokeza kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini wahusika.

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ngorongoro, Rashid Mfaume, anasema wa kuelimishwa kwa undani zaidi ni wanaume kwani ndiyo waamuzi wakuu katika ngazi ya familia.

Anasema ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya mila ya ukeketaji unachangia vitendo hivyo.

 

Muuguzi Mkuu anena

Muuguzi wa Hospitali ya Wasso, Joyce Sinodiya, anasema ukeketaji una madhara makubwa kwa mtoto wa kike kwani huharibu mfumo wa fahamu.

Anasema wasichana wengi wanaojifungulia hospitalini hapo huugua kichaa cha mimba, hali anayodhani husababishwa na kupata mimba wakiwa wadogo na pia kukeketwa.

Madhara mengine ya ukeketaji anasema ni wanawake kuchanika sehemu za siri wakati wa kujifungua.

“Hali hii humfanya mjamzito aliyekeketwa kutokwa na damu nyingi na tunalazimika kumuongezea nyingine, na baadhi yao hupoteza maisha pale huduma stahiki zinapokosekana,” anasema Sinodiya.

Anasema hakuna vifo vinavyotokea Wasso, isipokuwa kwa wanaofika wakiwa wamecheleweshwa.

Anasema wanawake wengi wakikeketwa hupoteza uwezo wa kujiamini wanapokuwa na wanawake wenzao wasiokeketwa kwa kudhani wamezaliwa tofauti na wenzao.

“Hali hii inaweza kumfanya mtoto wa kike aliyeko shuleni kufanya vibaya katika mitihani kutokana na kutumia muda mwingi [mrefu] kufikiria maumbile yake,” anasema Sinodiya.

Pia waliokeketwa hupoteza hamu ya tendo la ndoa, na wakati mwingine hulazimika kutafuta wanaume tofauti kwa kudhani watatimiziwa mahitaji yao ya kimwili.

Anasema ili jamii ya Kimaasai ibadilike, wanaume wanatakiwa kubadilishwa mitazamo yao kwa kupewa elimu. Kwa hali ilivyo sasa, mashirika ya kiserikali mengi yamejielekeza kuwaelimisha wanawake na watoto wa kike pekee.

Makala hii imeandaliwa na Gazeti la JAMHURI kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la Internews, linalojishughulisha na kupinga vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike na wanawake pamoja na unyanyasaji wa kijinsia.