Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MFUKO wa SELF (SELF Microfinance Fund), umeandaa mikakati ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo ili kuwawezesha kupata huduma za kifedha kwa ajili ya kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Hayo yamebainishwa leo Machi 11, 2024 na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Mfuko wa SELF Bw. Petro Mataba wakati akizungumza katika kikao kazi kati ya Jukwaa la Wahariri Tanzani (TEF) kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa hadi kufikia Desemba 31, 2023 tayari wametoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 324.51 ikiwa na kiwango cha mikopo chechefu chini ya asilimia 10 na kujiendesha kwa faida.
Mataba amesema kuwa mikopo iliyotolewa iliwafikia wanufaika laki 314,000 ambapo kati yao wanawake ni laki 166,000 wanaume laki 147,000 ambao walitoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Amesema mfuko wa SELF unafanya kazi inchi nzima kupitia matawi 12 na hadi sasa wanazaidi ya taasisi 200 ambazo wanazikopesha.
“Mfuko umetengeneza ajira 37,000 kutokana na wanufaika wanaochukua mikopo sanjari na kutoa elimu ya fedha kwa wanufaika 1517.
“Hadi kufikia Desemba 31, 2023 tumetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 324.51 ikiwa na kiwango cha mikopo chechefu chini ya asilimia 10 huku wakiweza kujiendesha kwa faida” amesema.
Amesema kuwa, mikopo hiyo imechangia upatikanaji wa huduma za mikopo kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kati nchini
Tawi la pili, Cheyo amesema ni la Zanzibar ambalo linahudumia Unguja na Pemba huku tawi la Kahama likihudumia mikoa ya Shinyanga, Tabora na Katavi.
“Na tawi la Morogoro linahudumia mkoa huo ambapo lile la Arusha linahudumia mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Tawi la Geita linahudumia mikoa ya Geita na Kagera huku Mtwara lilikihudumia mikoa ya Mtwara na Lindi.”
Kwa upande wa tawi la Mwanza linahudumia mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu ambapo lile la Iringa linahudumia Mkoa wa Iringa, Ruvuma na Njombe huku Tanga ikihudumia Mkoa wa Tanga. Aidha, tawi la Mbeya linahudumia mikoa ya Mbeya, Rukwa na Songwe. Huku lile la Dodoma likihudumia Dodoma yenyewe na Shinyanga.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa mfuko huo, Mudith Cheyo amesema Mfuko wa SELF (SELF Microfinance Fund) ni zao la mradi wa Serikali ambao ulijulikana kama Small Entrepreneurs Loan Facility (SELF) ulioanzishwa mwaka 1999 ikiwa chini ya Wizara ya Fedha pia ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
TR ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.
Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile, Mjumbe wa Kamati Tendaji wa jukwaa hilo, Salim Salim amesema kuwa, mfuko huo una nafasi kubwa ya kuweza kuboresha ustawi wa biashara za wananchi wenye kipato cha chini na cha kati.
Amesema kuwa, ili mfuko uweze kuhudumia idadi kubwa ya watu ni jambo jema kuendelea kujitangaza na kutoa elimu kuhusu masuala yahusuyo fedha kwa wananchi hapa nchi waweze kutumia fursa zilizopo katika mfuko kujiendeleza.