Ujumbe wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) ukiongozwa na Mkurugenzi Mwakilishi – Afrika Bwana Linden Morrison umetembelea MSD kwa lengo la kupata mrejesho wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo Global fund inasaidia kwa lengo la kuboresha mifumo ya afya nchini. Miradi inayofadhiliwa na mfuko huo ni pamoja na Mradi wa Dawa za UKIMWI na Kifua Kikuu, Malaria, Ununuzi wa vifaa vya maghala mapya yanayojengwa na MSD pia miradi ya mifumo mbalimbali ya uendeshaji wa MSD
Akizungumza kwenye Mkutano huo Mkurugenzi Mwakilishi – Afrika Bwana Linden Morrison amesema Global fund inafurahishwa na namna MSD inavyosimamia na kutekeleza miradi inayofadhiliwa na Mfuko huo kwani inaonesha namna fedha zinazotolewa na Global Fund zinavyotumika vizuri na kwa manufaa ya nchi. “Tuendelee na utekelezaji huu mzuri pale ambapo panachangamoto msisite kukaa nasisi kuweza kutatua kwa pamoja” Aliongeza Morrison.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai ameushukuru ujumbe wa Global Fund kwa kutembelea MSD na amewahakikishia kuwa fedha zinazotolewa na Global Fund zitaendelea kusimamiwa vizuri na kuelekezwa kwenye miradi iliyokusudiwa yenye lengo la kuboresha mnyororo wa ugavi wa nchi.
Hata hivyo Mavere ameomba kuendeleza ushirikiano baina ya MSD na Global Fund katika utekelezaji wa miradi mingine mbalimbali yenye lengo la kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi katika mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.


