Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Luis Bura

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Luis Bura, kwa kushirikiana na Ofisa Mifugo na Mtendaji wa Kata ya Kifula wilayani humo wanatuhumiwa kumtapeli mfugaji wilayani humo kiasi cha Sh milioni 12.

Mfugaji anayedai kutapeliwa anaitwa, Subi Gagi (56), ambaye ni mfugaji na mkazi wa Kijiji cha Ilunde, wilayani Kibondo, mkoani Kigoma.

Gagi ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba Machi 5, mwaka jana alikutana na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kifula (jina linahifadhiwa) ambaye alimweleza kuwa serikali imeruhusu wafugaji kuchungia mifugo yao kwenye Hifadhi ya Moyowosi.

Gagi anasema hakuamini maelezo hayo kutoka kwa mtendaji huyo, hivyo wakaongozana hadi kwa Ofisa Mifugo wa Wilaya, Dk. Gabriel Chitupila, ambaye alithibitisha kuwa suala hilo ni kweli na kwamba mkuu wa wilaya naye anathibitisha hilo.

“Baada ya kuonana na ofisa Mifugo, tukaongozana wote watatu hadi ofisini kwa Mkuu wa Wilaya, Bura, ambaye alithibitisha kuwa wafugaji tumeruhusiwa kuchunga mifugo yetu katika hifadhi hiyo kwa masharti mawili.

“Sharti la kwanza lilikuwa ni kulipia kiingilio cha Sh 30,000 kwa kila ng’ombe mmoja na kutaja majina yangu yote niliyokuwa nayatumia nikiwa katika Kijiji cha Ilunde kati ya mwaka 2005 hadi 2006,” amesema.

Mfugaji huyo amesema pamoja na masharti hayo, mkuu wa wilaya alimuuliza kama ana fedha zote za kulipia ng’ombe 400 ili waruhusiwe kuingia katika eneo hilo na ng’ombe wake kupigwa chapa.

Gagi amesema hakuwa na kiasi hicho cha fedha wakati huo, hivyo aliomba apunguziwe, ikiwa ni pamoja na nambari ya akaunti ili akalipe kupitia benki, lakini mkuu huyo wa wilaya alikataa kwa madai kwamba fedha hizo zinagawanywa kwa mkuu wa mkoa, wilaya, Idara ya Mifugo na kata.

“Aliniambia fedha hizo natakiwa kuzileta mwenyewe bila kupitia benki, nikiwa nimeambatana na ofisa mtendaji na ofisa Mifugo, ambao tulikuwa tumeongozana nao ofisini kwake ili kuthibitisha kauli hiyo ya serikali kuruhusu wafugaji kutumia eneo hilo.

“Kati ya Machi 8 na 10, mwaka jana niliuza ng’ombe wangu wakubwa 24 kwa bei ya Sh 500,000 kwa kila ng’ombe na kumpitia ofisa mtendaji na ofisa Mifugo, tukaongozana nao hadi kwa Mkuu wa Wilaya, Bura, ambaye nilimkabidhi Sh milioni 12 mbele ya wote hao.

“Nilimwomba mkuu wa wilaya anipe risiti ya malipo ya fedha hizo, akanieleza kuwa risiti zote zinatoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma baada ya kukamilisha zoezi la kupiga chapa na kwamba wenzangu wote waliokuwepo katika kijiji hicho nao hawajapewa risiti hizo.

“Niliuliza utaratibu wa kuingiza mifugo yangu baada ya kulipa ada hiyo kwa mkuu wa wilaya, Machi 16, mwaka jana nilipewa kibali na Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Kibondo,  Dk. Chitupila chenye namba 1523889,” amesema Gagi.

Mfugaji huyo amesema alipewa kibali cha kuingiza ng’ombe katika eneo la Ilunde, wilayani Kibondo kutoka wilayani Kasulu na kulipa Sh 600,000 kwa ng’ombe 400.

Gazeti la JAMHURI limekiona kibali hicho cha kuingiza ng’ombe ambacho kimemruhusu ‘Lugwisha Seni’ jina alilokuwa akilitumia Gagi alipokuwa anaishi katika Kijiji cha Asante Nyerere, wilayani Kasulu ambacho kimesainiwa na Ofisa Mifugo wa Wilaya hiyo, Sabinus Chaula, JAMHURI limemhoji Gagi sababu za kubadili jina, hakuwa na jibu isipokuwa kusema yote ni majina yake.

Pamoja na kuruhusiwa kuingiza mifugo yake katika Wilaya ya Kibondo, Dk. Chitupila alimtaka Seni (Gagi) kupeleka mifugo yake katika eneo la kupigia chapa lililopo kwenye mpaka Kata ya Busagara katika halmashauri ya wilaya hiyo.

“Katika kutekeleza zoezi la chapa kitaifa, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo iliendesha zoezi hilo katika eneo la Ilunde ambalo liko katika mipaka ya Halmashauri ya Kibondo Januari 4 hadi Machi 12, 2018,” imeeleza sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Dk. Chitupila.

Barua hiyo imeeleza kuwa wakati wa uendeshaji wa zoezi hilo, ilitokea operesheni ya watu wa Pori la Moyowosi na kusababisha baadhi ya wafugaji kutoroka na mifugo yao kwa hofu ya kukamatwa.

Dk. Chitupila katika barua yake amesema: “Miongoni mwa watu ambao walitorosha mifugo yao ni pamoja na Seni ambaye alitoroshea mifugo yake katika eneo la upande wa Kasulu linalopakana na Wilaya ya Uvinza ili kunusuru mifugo yake isikamatwe.”

Gagi amesema baada kupiga chapa mifugo yake aliendelea kuchunga mifugo yake katika Pori la Moyowosi kama alivyokuwa ameelekezwa na kupewa kibali, kwa kipindi cha miezi mitano akiwa amewaacha vijana wake wawili, Jilala Seni na Bikolimana Musa.

Amesema Septemba Mosi mwaka jana, maofisa wa maliasili kwa kushirikiana na askari polisi waliingia katika eneo hilo ambalo alielekezwa na viongozi hao wa wilaya achungie ng’ombe wake na kukamata ng’ombe wote 441 pamoja na vijana hao.

Baada ya kukamatwa, vijana wake walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kibondo na kufunguliwa kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2018, kwa kuingia kinyume cha sheria katika eneo la hifadhi, kinyume cha Kifungu cha 15 (1)&(2) cha Sheria ya maeneo ya hifadhi namba 5 ya mwaka 2009.

Kesi hiyo iliendeshwa kwa muda wa siku nne tu na Septemba 21, mwaka jana Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibondo, Kamuntu, alitoa hukumu iliyowataka washtakiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh 300,000 kila mmoja.

“Nililipa faini na Oktoba 4, mwaka jana niliamua kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma ili kuokoa mifugo yangu iliyotangazwa kutaifishwa na kuuzwa kwa njia ya mnada na mkuu wa wilaya.

“Rufani yangu ilipewa namba 188 ya 2018 na kupangwa kusikilizwa Oktoba 10, mwaka jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Salvatory Bongole, alitoa zuio la kuuzwa kwa ng’ombe hao 441.

“Wakati kuna zuio la mahakama, Oktoba 10, mwaka jana, mkuu wa wilaya aliagiza ng’ombe wangu wauzwe kwa mnada ambao ulifanyika Oktoba 11, mwaka jana,” amesema.

Gagi ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa baada ya ng’ombe wake kuuzwa alikwenda kuonana na mkuu wa wilaya aliyempa kibali cha kuchunga mifugo katika eneo hilo ili amsaidie kunusuru mifugo hiyo isipigwe mnada lakini akamtaka alipe faini ya Sh milioni 20.

Amesema hakuwa na kiasi hicho cha fedha alichotakiwa kulipa kama faini na kuelezwa kuwa aliruhusiwa kuingiza mifugo hiyo katika eneo hilo kwa ajili ya kupiga chapa tu na kuondoka nayo.

“Mkuu wa wilaya akanieleza kwamba nikizidi kumfuata fuata atanifanyia kitu kibaya zaidi na kwamba nifanye lolote lile lazima ng’ombe wangu wauzwe,” amesema Gagi.

Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Kasulu aliyesaini kibali cha kusafirishwa kwa mifugo hiyo kutoka wilayani humo hadi Ilunde, wilayani Kibondo, Sabinus Chaula, ameliambia JAMHURI kuwa suala hilo bado liko kwenye uchunguzi na malalamiko ya mfugaji huyo yalifikishwa katika Ofisi ya Rais.

“Mlalamikaji ana haki ya kulalamika iwapo amedhulumiwa haki yake, na kwamba nani amemchukulia fedha zake na kutoa kibali mifugo yake irudishwe katika eneo hilo?

“Siwezi kulielezea suala hili kwani liko katika hatua za uchunguzi, naomba uwatafute waliompa kibali mfugaji huyo kuingiza mifugo yake tena katika eneo hilo la hifadhi,” amesema Chaula.

Waliotoa kibali

JAMHURI limemhoji Dk. Chitupila ambaye ni miongoni mwa watu wanaotuhumiwa kumruhusu Gagi kuingiza mifugo katika eneo hilo na baadaye kuikamata na kuiuza kwa mnada, amesema hana uhakika kuwa linakuwaje jambo hilo linahojiwa.

“Naomba tuache uchunguzi ufanyike, lazima haki itendeke kwa pande zote tangu hapa wilayani hadi taifa na kitakachotokea kitajulikana,” amesema Chitupila.

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Luis Bura, amekana kutomfahamu mfugaji huyo anayedai kumpatia Sh milioni 12 ili kuingiza ng’ombe katika eneo hilo.

Bura amesema Machi 5, mwaka jana siku ambayo mlalamikaji anasema alikwenda ofisini kwake akiwa ameongozana na Dk. Chitupila na Msanzugwimo ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Kifula hakuwepo ofisini kwake.

“Machi 5 na 6, mwaka jana nilikuwa Dodoma kuonana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo na shughuli zangu nyingine.

“Nilirudi Machi 11, mwaka jana kutoka Dodoma, mimi ni DC ninatoka ofisini kwangu kwa kibali na muda wa kuingia na kutoka lazima niandike kwenye kitabu.

“Pia Machi 14, mwaka jana sikuwepo ofisini kwangu, nilikwenda kumpokea Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Humphrey Polepole na kurudi nyumbani saa moja usiku,” anakumbuka Bura.

Bura ameongeza kuwa Machi 15, mwaka jana hakuwepo ofisini kwake, alikuwa ameongozana na Polepole hadi mpakani mwa Wilaya ya Kibondo na Kasulu na kumkabidhi kwa mkuu wa wilaya hiyo.

 Amesema Machi 18, mwaka jana ndipo aliporudi ofisini kwake na kwamba hamfahamu mwananchi huyo anayedai kuwa Machi 16, mwaka jana alimpelekea fedha kwa ajili ya malipo ya kibali cha kuingiza mifugo yake katika eneo la Ilunde.

Amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) walikwisha kumhoji na vielelezo vyote aliwapa na kusisitiza kwamba hakuwahi kukutana na mlalamikaji huyo kwa tarehe hizo.

“Vielelezo vyote na kwenye Hifadhi ya Ilunde hakuna mifugo yoyote kwa sasa, hivyo awatafute watu aliowapa hizo fedha na wakamtapeli, hizi ni tuhuma nzito sana.

“Sijawahi kuonana na Gagi ana kwa ana, lakini alinipigia simu na kunijulisha kuwa watu wa hifadhi wamekamata ng’ombe wake, akaomba nimsaidie,” anakumbuka Bura.

Gagi amesema wahusika wanafahamu kuwa hajui kusoma na kuandika, hivyo wanatumia nafasi hiyo kukwepa tuhuma hizo ambazo wanahusika nazo moja kwa moja.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa wizara yake haielewi kuuzwa kwa ng’ombe hao, wala haijaanza kufanya uchunguzi kama wahusika wanavyodai.

“Bado sijafika Ilunde na malalamiko ya mfugaji huyo hayajanifikia rasmi, hivyo nasubiri aniletee vielelezo vyake ili nielewe tatizo hilo liko wapi.

“Mimi niko kwa ajili ya kuwatetea wafugaji, siwezi kuwaletea manyanyaso kama haya, waliouza mifugo hiyo ni watu wa maliasili,” amesema Mpina.