Raia wa Uswisi au Switzerland, mwenye asili ya Italia, Gianni Infantino, mwishoni mwa wiki iliyopita ndiye aliyechaguliwa kuwa Rais mpya wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Amechukua nafasi ya Sepp Blatter, aliyedumu madarakani kwa miaka 17 akiongoza shirikisho hilo. Blatter ameondolewa kwa aibu, kwamba alihonga kuipa nafasi Qatar uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia, hapo 2022.
Kwa kawaida, binadamu haachi kujinasua panapotokea kashfa kama hiyo na Blatter naye amekana kutoa na kupokea rushwa katika kandarasi ya kuipa nafasi Qatar.
Blatter alishinda kiti hicho kwa mara ya tano mnamo Mei, mwaka jana, lakini akapigwa marufuku na Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo kujihusisha na soka kwa muda wa miaka minane baada ya uchunguzi wa awali kuelezwa kuwa alimlipa pauni milioni 1.3 Rais wa UEFA, Michel Platini. Platin naye amesimamishwa kazi kwa malipo hayo ya utata.
Yote kwa yote, nafasi ya Blatter sasa imechukuliwa na Infantino – Katibu Mkuu wa Fifa ambaye katika uchaguzi huo wa Ijumaa iliyopita, alipata kura 115 baada ya uchaguzi kufanyika kwa raundi mbili ikiwa ni kura 27 zaidi ya mpinzani, Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa- Rais wa Shirikisho la Soka la Asia.
Katika raundi ya kwanza, Infantino alizoa Kura 88 na Salman 85 na kulazimisha kufanyika kwa raundi ya pili ya upigaji kura kwa vile idadi inayotakiwa ya kuwa na Kura zaidi ya theluthi tatu haikufikiwa ambayo mshindi alitakiwa kuwa na kura zaidi ya 104. Katika raundi ya pili ya kura, Infantino alipata kura 115. Jumla ya mashirikisho na vyama vya soka 209 vilipiga kura.
Mwanamfalme Ali bin al-Hussein- makamu wa zamani wa rais wa FIFA kutoka Jordan alikuwa wa tatu akiwa na kura nne huku Mfaransa Jerome Champagne akishindwa kupata hata kura moja. Tokyo Sexwale wa Afrika Kusini alijiondoa kabla ya kura kuanza kupigwa mjini Zurich, Uswis.
Infantino (45) ambaye ataongoza shirikisho hilo hadi 2019, ni wakili kutoka eneo la Brig jimbo la Valais nchini Switzerland, ikiwa ni eneo lililopo chini ya maili sita kutoka nyumbani kwa Blatter.
Baada ya kutangazwa mshindi, Infantino aliwaambia wajumbe waliopiga kura hakujielezea vema kutokana na hisia alizokuwa nazo, ana akaongeza kusema: “Kwa pamoja tunaweza kuirudisha sura ya Fifa na heshima ya Fifa.”
Ilikuwa ni lazima Infantino kwani aliungwa mkono na Ulaya (UEFA) kwa kura 53, shirikisho la vyama vya kandanda Amerika ya kusini lenye kura 10, na wajumbe saba wa shirikisho la kandanda la America ya kati, ambalo ni sehemu ya kundi kubwa la kanda ya shirikisho la CONCACAF kwa ajili ya Amerika ya kaskazini na kati.
Kwa mujibu wa mtazamo huo, Infantino alikuwa na uhakika wa kupata kura asilimia 70. Sheikh Salman mwelekeo wake ulikuwa ni tofauti baada ya kuonekana anaungwa mkono na vyama kutoka Asia na Afrika ambavyo kwa jumla vina kura asilimia 20.
Infantino alizaliwa Machi 23, 1970, huko Brig, Switzerland. Wazazi wake alitokea, Calabria na Lombardy, Italia. Ni mtawala aliyekuwa Katibu Mkuu wa Fifa tangu mwaka 2009 hadi alipochaguliwa kuwa Rais wa Fifa, Februari 26, 2016.
Ni msomi wa sheria aliyepata shahada yake Chuo Kikuu cha Fribourg ambaye anazungumza vema lugha za Kilatini (Kitaliano), Kifaransa, Kijerumani, Kiingereza, Kihispaniola na Kiarabu.
Awali Infantino alifanya kazi ya Katibu Mkuu wa Kituo cha Michezo cha Kimataifa (CIES) katika Chuo Kukuu cha Neuchâtel.
Agosti mwaka 2000, Infantino alianza kutumikia UEFA kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa masuala ya Sheria na Leseni za klabu kuanzia Januari 2004.
Baadaye mwaka 2007 aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UEFA na miaka miwili baadaye, Oktoba 2009 akashika wadhifa kamili wa Katibu Mkuu wa UEFA.
Wakati akifanya kazi hiyo, UEFA ikamtambua na kumuongezea madaraka mengine ya kushughulikia usimamizi wa fedha na kusapoti vyama vichanga vya michzo.
Hapo akasimamia pia ongezeko la timu zinazoshiriki michuano ya Ulaya ‘Euro’ katika fainali za mwaka 2016. Timu zikafikia 24 kabla ya kutoa mchango wake wa kuboresha fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya na Uropa.
Mwaka jana, kulikuwa na tukio la kukatisha maendeleo ya soka huko Ugiriki baada ya Serikali kuanzisha sheria mpya za michezo za kubana wadaua wanaoleta vurugu uwanjani na viongozi wanaojihusisha na rushwa.
Infantino, kwa nafasi yake kama Katibu Mkuu wa UEFA, aliongoza timu ya wataalamu wa Ulaya kwend Ugiriki kuweka sawa hali ya mambo kwa makubaliano.
Aliwaambia wazi kabisa kuhusu kanuni na taratibu za Fifa na kwamba walikuwa wanaelekea kufungiwa kama wataamua kutumia sheria zao mpya hili Fifa ni chombo huru. Alifanikiwa kuishawishi Serikali ya Ugiriki na ikaondoa sheria zake.
Baada ya sakata la Blatter na mwenzake Platin, Infantino akafuatwa akishawishiwa kuwania nafasi hiyo jambo ambalo alilikubali mara moja na kuana taratibu huku sera yake ni kuwa soka lazima lipigwe.
Kwa mtazamo wake, timu 32 katika fainali za Kombe la Dunia ni chache na ni vema zikafika 40 ambako kwa Afrika sasa zinaweza kuongezeka kutoka tano za sasa hadi angalau timu nane.
Infantino ambaye ni shabiki mkubwa wa timu ya Inter Milan ya Italia, amemwoa Leena Al Ashqar, raia wa Lebanon. Ana watoto naye wanne.