Na Isri Mohamed, JamhuriMedia
Ni simanzi na huzuni zimetawala kwa wakazi wa Kigamboni, wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali na Taifa zima kwa ujumla kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dkt Faustine Ndugulile kilichotokea usiku wa kuamkia Novemba 27, akiwa nchini India akipatiwa matibabu.
Kifo chake kimekuja ikiwa ni miezi michache tu tangu ateuliwe kuwa Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.
Watu mashuhuri mbalimbali wameonesha kuguswa na msiba huu, sio tu wanasiasa wenzake, bali na wasanii, wadau wa mpira wa miguu na sekta mbalimbali, hii inaonesha wazi aliishi na watu wa kada zote vizuri, na ndio maana nikawiwa kuandika makala hii ili kwa wasiomfahamu basi wamfahamu vizuri.
KUZALIWA NA ELIMU
Jina lake kamili ni Faustine Engelbert Ndugulile, amezaliwa Machi 31, 1969, wilayani Mbulu mkoani Manyara.
Mwaka 1976 alianza masomo yake ya elimu ya msingi huko Harare nchini Zimbabwe katika shule ya Groombrige na kuhitimu mwaka 1982.
Baada ya kuhitimu msingi alijiunga na shule ya Prince Edward iliyoko huko huko Zimbabwe, mpaka alipomaliza mwaka 1986.
Baada ya kuhitimu sekondari alihamia rasmi nchini Tanzania na kuendelea na kidato cha tano katika shule ya Tambaza iliyopo jijini Dar es Salaam, na kuhitimu mwaka 1989.
Mwaka 1990 alianza kusoma shahada ya udaktari wa madawa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 1997.
Mwaka 2001 alipata shahada ya uzamili katika mikrobiolojia na chanjo katika chuo kikuu hicho hicho.
KAZI
Ndugulile alifanya kazi katika nyanja mbalimbali za tiba, afya ya umma, na siasa, alianza kama daktari wa afya ya umma na kupanda kwenye nafasi za uongozi.
Alifanya kazi kama Msaidizi Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi katika Wizara ya Afya, ambapo aliongoza juhudi za kuboresha huduma za damu na uchunguzi wa magonjwa, na kuwa na mchango mkubwa katika programu za afya za kitaifa.
Katika ngazi ya kimataifa, alifanya kazi kama Mshauri Mkazi nchini Afrika Kusini, akichangia katika usimamizi wa mifumo ya afya ya kanda na mipango ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
SIASA NA UONGOZI
Alianza siasa mwaka 2010 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Kigamboni nafasi aliyoitumikia mpaka umauti ulipomkuta.
Ndugulile aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Tanzania) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tano, hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Oktoba 2017.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020, tarehe 5 Desemba 2020, katika Baraza la Mawaziri la pili la Magufuli, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wizara mpya iliyozinduliwa.
NAFASI WHO
Mnamo Agosti 2024, Ndugulile aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO) aliheshimika sana kwa uongozi wake na maono yake katika sekta ya afya ya umma.
Uteuzi wake kama Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika ulikuwa ni mafanikio makubwa kwa Tanzania na Bara la Afrika.
Alipokea pongezi kutoka kwa viongozi, ikiwa ni pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, aliyempongeza kwa uwezo wake wa kushughulikia changamoto kubwa za afya zinazokabili Afrika.
Alikuwa anatarajiwa kuanza rasmi jukumu lake katika WHO mnamo Februari 2025, akichukua nafasi ya Dkt Matshidiso Moet wa nchini Botswana ambaye amemaliza muda wake.
KIFO
Ndugulile amefariki dunia Novemba 27, 2024, akiwa na umri wa miaka 55, wakati akipatiwa matibabu nchini India kwa ugonjwa ambao haukutajwa hadharani.