DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Mambo huwa yanakwenda na kufika mwisho. Nimewahi kuuona mwisho wa Steven Gerrard na Liverpool. Nikawahi kuuona mwisho wa Sergio Ramos na Real Madrid. Hivi sasa ninauona mwisho wa Lionel Messi na Barcelona. Haishitui sana.
Hivi sasa Messi ni mshindi wa taji la Copa America, lakini ni mchezaji huru.
Mwishoni mwa wiki gwiji huyu wa soka wa Argentina ameliongoza taifa lake kuifunga Brazil bao 1-0 na kushinda ubingwa wa Copa America.
Anamaliza muda wake wa soka kwa heshima huku mpinzani wake wa miaka mingi, Ronaldo, akijikuta akiishia robo fainali ya UERO 2020.
Ni mara ya kwanza kwake kuchukua taji hilo kubwa baada ya kuingia na kucheza fainali nne za Copa America.
Kwa upande mwingine, katika soka ngazi ya klabu, mkataba wake na Barcelona umekata roho siku kadhaa huko nyuma. Yuko sokoni na ukiweka dau analolitaka na meneja wake unamsajili bila shida.
Umewaza kwa nini Messi amecheza mpaka mkataba wake umemalizika kabisa na mabosi hawakimbizani naye tena? Jibu ni dogo na jepesi tu. Hana maajabu na umri wake umesogea kiasi kikubwa. Ana miaka 34.
Messi wa sasa hakimbii tena kilomita nyingi kiwanjani. Akili yake inataka kufanya kitu, mwili wake unamsaliti. Mwisho kabisa kuwa na Messi katika timu yako ni gharama kubwa.
Njia pekee ya kumfanya Messi apewe mkataba mpya na Barcelona ni kupunguza mshahara mnono aliokuwa anauchukua katika mkataba uliopita. Sidhani kama Messi atakubali kufanyiwa hivi. Ngoja tuone mwisho wa sinema hii.
Messi wa miaka kumi iliyopita mkataba wake usingefikia hivi. Angekuwa na mkataba wa miaka mitatu, bado angeongezwa miaka mingine miwili. Timu kubwa za Ulaya huwa zinaishi hivi na mastaa wao wakiwa katika kiwango bora na wakiwa na umri mdogo.
Ukiwa katika ‘peak’ watu hawatazami sana mkataba wako mnono na mkwanja unaochukua. Lakini umri wako ukisogea unaandaliwa mikataba ya kubanwa ambayo mara nyingi wachezaji hukataa kuisaini.
Mwisho wa siku huwa wanaondoka. Ni kama ilivyotokea kwa Ramos na Madrid. Kabla ya Ramos kuachana na Madrid alianza kuvutana na mabosi wake. Alitaka apewe mkataba wa miaka miwili, Madrid wakakataa wakasema watampa mwaka mmoja.
Ramos akasema ngoja akafikirie. Alipokwenda kushauriana na wakala wake wakaukubali huo mwaka. Alipokwenda kuwaambia mabosi wa Madrid kuwa amekubali kusaini mwaka mmoja akajibiwa muda huo haupo tena na anaweza kuondoka kwenda kutafuta changamoto nyingine.
Ramos aliyekuwa mwamba wa kufanya kazi mbili kiwanjani kwa wakati mmoja, inakuwaje mkataba wake unafikiriwa mara mbili mbili na mabosi wa Madrid? Ramos wa leo hana tena maajabu miguuni mwake. Mambo hufika mwisho.
Nampenda sana Messi, lakini mwisho wake umekaribia. Kama si leo ni kesho, kama si kesho ni keshokutwa. Hakuna namna. MERCII MESSI.