Nyota wa timu ya soka ya Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi pamoja na baba yake mzazi wamelipa euro milioni tano, sawa na dola milioni 6.6 za Marekani, baada ya kubainika na kosa la kukwepa kodi. Messi na mzazi wake huyo walidaiwa kukwepa kulipa kodi hiyo ya serikali kwa njia za ujanjaujanja.

Madai hayo ya kukwepa kodi yaliyowasilishwa mahakamani Juni, mwaka huu yalimpa wakati mgumu Messi ambaye alionekana kunyong’onyea kila mara ikilinganishwa alivyokuwa awali. Uamuzi ya jaji huko Gava, kwenye pwani ya bahari Mediterenian karibu na mji wa Barcelona, ulisema kuwa baba yake Messi, Jorge Messi, alilipa euro milioni 5.02 kwenye mahakama Agosti 14, mwaka huu kufidia kodi pamoja na riba.

 

Jaji huyo amepinga ombi la mwanasheria wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kutaka alipe kwa dhamana ya hisa kuhakikisha kuwa riba yoyote itakayosababishwa na kesi inalipwa. Jaji alisema haina haja kwa sababu ya uwezo aliyonao Lionel Andres Messi Cuccittini, akiongeza kuwa tayari kodi hiyo imeishalipwa.

 

Mashtaka dhidi ya Messi na baba yake huyo ni kuhusu kuiba kodi inayotokana na mapato ya biashara zinazotumia sura yake kuanzia mwaka 2006 hadi 2009. Inadaiwa kuwa Messi na baba yake huyo walijaribu kulihadaa taifa kwa kuhamisha hatimiliki za malipo hayo kwenye kampuni zilizo nje kama huko Belize na Uruguay ili wasilipe kodi nchini Hispania.

 

Wakili wa Messi, Juarez Veciana, alisema mteja wao anakubaliana na sheria za Hispania na yupo tayari kulipa kila fedha anayotakiwa kulipa. Ufanisi wa Messi uwanjani umemfanya kuwa moja ya sura zinazouzika duniani akiwa namba 10 kwenye orodha ya wanamichezo mashuhuri wenye mapato makubwa akikadiriwa kupokea dola milioni 21 kila mwaka kutokana na matangazo ya biashara peke yake.