Kabla ya kuzungumzia mada ya leo, ninapenda kuwashukuru wasomaji wote wa Safu hii walionipigia simu, kunitumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) na e-mail, baadhi wakinipongeza, kunishauri na wengine wakinikosoa kuhusu makala niliyoandika wiki iliyopita, iliyobebwa na kichwa cha habari, “Watanzania na imani potofu ziara ya Obama.” Nimejifunza mengi kutoka kwao.
Lakini pia ninawapa pole watu wote waliokwazwa na kubughudhiwa kwa namna mbalimbali wakati wa maandalizi na utekelezaji wa ratiba ya ziara ya Rais Barack Obama wa Marekani, jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.
Ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya ombaomba na wamachinga wanaojitafutia riziki kandokando ya barabara jijini, hawakufurahia ujio wa Rais Obama kwani umewakosesha kipato baada ya vyombo vya dola kuwaondoa katika maeneo hayo wakati wote wa ziara hiyo. Tuachane na hayo.
Leo nafsi imenisukuma kuzungumzia juhudi mbalimbali zinazofanywa na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, kutafuta ufumbuzi wa umaskini unaoendelea kuwanyima Watanzania wengi maendeleo na maisha bora.
Nilipata kusema, na ninaendelea kusisitiza kuwa Dk. Mengi ni mtu anayedhihirisha kwa vitendo uzalendo wake kwa nchi yetu, lakini pia anayetamani kuona mafanikio ya kiuchumi na maisha bora kwa kila Mtanzania.
Itakumbukwa kwamba katika siku za karibuni, Dk. Mengi amekazania kusaka ufumbuzi wa matatizo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yanayoikabili Tanzania. Amefanya jitihada hizo kwa nyakati tofauti kupitia kwa mabalozi wa nchi mbalimbali hapa nchini.
Tayati katika kipindi cha miezi minne iliyopita, Dk. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), ameweza kukutana na Balozi Sinikka Antila wa Finland, Chung Il (Korea Kusini), Debnath Shaw (India) na Lennarth Hjelmaket wa Sweden.
Mazungumzo ya Dk. Mengi na mabalozi hao yamekuwa yakijikita zaidi katika hoja za kuboresha uchumi, elimu, afya (miongoni mwa huduma nyingine za kijamii), amani, kuongeza ajira kwa vijana, matumizi sahihi ya rasilimali za nchi na udhibiti wa rushwa na bidhaa bandia hapa nchini.
Matarajio ni kwamba ahadi chanya zilizotolewa na mabalozi hao kwa Dk. Mengi, zitatekelezwa kwa vitendo kupunguza umaskini miongoni mwa Watanzania.
Kama hiyo haitoshi, Mei mwaka huu, mfanyabiashara huyo ameanzisha shindano la mawazo mapya yanayoweza kusaidia kutokomeza umaskini Tanzania. Shindano hilo litadumu kwa mwaka mmoja. Ametenga zawadi ya Sh milioni 1.8 kwa washindi kila mwezi.
Kwa mfano, Mei mwaka huu, washindi watatu wa shindano hilo walitangazwa na kuzawadiwa fedha taslimu.
Mshindi wa kwanza, Jill Kiomo, alizawadiwa Sh milioni moja. Wazo lililomwezesha kutwaa nafasi hiyo linasema, “Tuwe na utamaduni wa kupenda kile tukifanyacho, kukifanya kwa moyo, uadilifu, heshima na kujali muda, hata kama it’s self employed.”
Peter Ngululu alishika nafasi ya pili katika shindano hilo na kuzawadiwa Sh 500,000. Alibebwa na wazo lake linalosema, “Kuweka mfuko wa mikopo kwa vijana wanaowekeza kwenye kilimo na kukuza sekta za kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja.”
Naye Ludovick Angelino alitangazwa mshindi wa tatu na kukabidhiwa zawadi ya Sh 300,000 kufuatia wazo lake linalosema, “Uoga ndiyo chanzo cha umaskini, tunachekea ufisadi, tunashindwa kuchagua na kuteua watu sahihi wa kutuongoza.”
Pia washindi wa Juni mwaka huu wameshatangazwa na kukabidhiwa zawadi zao na Dk. Mengi jijini Dar es Salaam. Mshindi wa kwanza ni Emmanuel Kombe akifuatiwa na Ndavukai Mollel na Wilfred Tarimo. Mawazo yaliyowapatia vijana hao ushindi huo ni kama ifuatavyo:
Emmanuel Kombe: Ili kufanikiwa kiuchumi katika mazingira yoyote unahitaji maandalizi. Kama serikali haijakuandalia, usiendelee kusubiri. Jiandalie.
Ndavukai Mollel: Nina idea ambayo ninaamini itasaidia kiasi kikubwa sekta ya elimu na jamii….unaonaje mkianzisha students volunteer programs.
Wilfred Tarimo: Shida ya vijana wengi wanapenda kazi zinazowapa hadhi ya juu katika jamii, badala ya kukubali vidogo ili makubwa yaje.
Mwenyekiti huyo wa IPP amefafanua kuwa ameanzisha shindano hilo, baada ya kukerwa na tatizo la umaskini linaloendelea kushika hatamu miongoni mwa Watanzania, licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali.
Mwenyewe anasema; “Hata baada ya miaka 50 ya Uhuru, umaskini umewaganda Watanzania kwa namna ya ajabu na inayotia aibu. Hili linaonekana mpaka kwenye mahitaji ya msingi kama vile chakula. Watanzania wengi ni maskini mno kiasi cha kutoweza kula milo miwili kwa siku, achilia mbali chakula kilichokamilika chenye lishe bora.
“Umaskini huo upo katika nchi yenye utajiri mkubwa wa rasilimali. Kama Tanzania inataka kuondokana na mzizi wa umaskini huo lazima iwepo mikakati mipya yenye majibu sahihi kuhusu nini kifanyike kuuzika.
“Ni dhahiri mafanikio hayo yatawezeshwa na fikra, mawazo na ushauri kutoka kwa Watanzania wenyewe na marafiki zao juu ya nini kifanyike ili kupambana na kuuzika umaskini.”
Matarajio ni kwamba shindano hilo lililoanzishwa na Dk. Mengi litaibua mawazo mapya yanayoelekeza mbinu zinazofaa kutumiwa kukabili na hatimaye kutokomeza umaskini hapa Tanzania.
Yeyote anayehitaji kushiriki shindano hilo lazima ajisajili kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kutafuta neno @regmengi kwa ajili ya kutuma wazo lake.
Kwa hakika juhudi hizo za Dk. Mengi zinadhihirisha dhamira yake ya kweli katika kuisaidia serikali na Watanzania kwa jumla kutafuta mbinu zinazofaa kufuta umaskini hapa nchini. Ni mfano mzuri unaostahili kuigwa na watu wengine katika jamii.