Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

MENEJA wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Ruvuma Yahya Mudhihiri amewaasa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuona umuhimu wa kuzingatia malezi mema kwa watoto na vijana kwani hivi sasa kumekuwa na matukio mengi ya ukatili na mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki kwenye mahafari ya darasa la saba katika shule ya msingi ya Skill Path (ENGLISH MEDIUM) yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Meneja wa mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Mkoa wa Ruvuma Bw.Yahya Mudhir ambaye ni mgeni rasmi kwenye mahafari ya darasa la Saba katika shule ya msingi ya skill path.

Amesema kuwa wazazi pamoja na walezi wanapaswa kujitahidi kuwa karibu na watoto kwenye malezi na kuwapa miongozo sahihi kwa ajili ya ustawi mzuri wa jamii kwa kuimarisha mila na desturi ya Mtanzania kwa kuwaepusha na makundi yasiyo sahihi ambayo yanaweza kusababisha kutotimiza ndoto zao.

Amewakumbusha wazazi na walezi kuzingatia lishe na chakula bora kwa watoto wao kama Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mara kwa mara imekuwa ikisisitiza jamii ya Watanzania kuzingatia zaidi lishe bora kwa watoto ili kuondoa na kutokomeza udumavu kwa watoto na kila mmoja anapaswa kufahamu lishe bora husaidia kwa kiasi kikubwa kumjenga mtoto katika ukuwaji mzuri na kuongeza uwelewa katika masomo yake.

‘’Napenda kuwashukuru kwa mara nyingine tena uongozi wa shule ya Skill Path kwa heshima waliyonipa ya kuwa mgeni rasmi katika sherehe hii ya mahafari najua heshima hii nimeipata kutokana na nafasi yangu niliyonayo katika taasisi ninayofanyia kazi ya Mfuko wa Taifa ya Hifadhi ya Jamii (NSSF) natoa shukrani za NSSF kwa uongozi wa shule ya Skill Path, “amesema Mudhihir.

Kaimu Mkurugenzi wa shule ya skill path Bw. Juma Mwanga akimkarisha mgeni rasmi kwenye mahafari ya darasa la Saba kwenye viwanja vya shule hiyo.

Meneja huyo amesisitiza kuona umuhimu kwa wazazi na walezi pamoja na wananchi wengine kujiunga na mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii kwa wale wote walioajiriwa katika sekta binafsi na Serikali .

Aidha meneja huyo ameahidi kutoa kompyuta 10, Scana 1 na Printer zenye thamani ya shilingi milioni 3 kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali katika shule hiyo.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Skill Path Rashid Nyenje amesema kuwa shule yao inakabiliwa na changamoto ya jamii kutowapeleka watoto wao kwa madai kuwa shule hiyo inaitikadi ya seminari jambo ambalo si la kweli bali inapokea wanafunzi wa dini zote kwa kuzingatia kanuni na taratibu za Wizara ya Elimu na si vinginevyo.

Naye kaimu meneja wa shule hiyo Juma Mwanga, amewashukuru wazazi pamoja na walezi wa wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi kwa kuiamini shule hiyo pamoja na uongozi kwa ujumla kwa malezi waliyoyapata tangu walipoanza shule ya awali hadi kumaliza elimu yao ya msingi na kwamba elimu waliyoipata kwa kipindi chote watafaulu vizuri zaidi mitihani yao ya mwisho alishukuru kwa ahadi ya vifaa iliyotolewa na mgeni rasmi ambaye ni meneja wa NSSF Mkoa wa Ruvuma.

Baadhi ya wanafunzi wahitimu wa darasa la Saba katika shule ya msingi ya skill path iliyopo manispaa ya Songea.