Sakata la mikopo ya wajasiriamali 4,200 katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, limechukua sura mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kumkamata na kumhoji Meneja Mkuu wa Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL), Elizabert Makwabe.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya mmoja wa wajasiriamali hao ambaye ni mwanachama wa Vicoba Endelevu mkoani Kilimanjaro, Vicent Mulamba, kutishia kuifikisha mahakamani benki hiyo kwa kile anachodai ilimdanganya kumpa mkopo wa Sh milioni 50.
Mikopo hiyo inayodaiwa kuwa ya Sh. 40 milioni hadi 60 milioni ilikuwa itolewe kwa vikundi 140 vya Vicoba kupitia Benki hiyo ya Ushirika, lakini kwa sharti la kila mwanachama wa vikundi hivyo kuwa na akaunti katika benki hiyo na pia kujiunga na NSSF.
Mkuu wa Takukuru mkoani Kilimanjaro, Alex Kuhanda, amekiri taasisi yake kumhoji meneja huyo, na kuongeza kuwa bado uchunguzi juu ya sakata hilo unaendelea, lakini hakuwa tayari kuingia kwa undani zaidi kutokana na kubanwa na kanuni zinazowakataza kuzungumzia masuala yaliyopo katika hatua ya uchunguzi.
Sakata hilo liliibuliwa na wana-Vicoba hao mwaka 2015 ambapo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala, alilazimika kufanya kikao cha pamoja baina ya uongozi wa KCBL na wajasiriamali hao.
Hata hivyo, Makala alilazimika kufanya mawasiliano na NSSF ambao ndiyo waliokuwa watoe fedha na kuipa KCBL ili nayo iwapatie wajasiriamali hao, lakini mpango huo uliyeyuka baada ya NSSF kudai haiwezi kutoa tena fedha kwa benki hiyo.
“Kwa vile suala hili sasa limefika mwisho na imebainika hakuna mikopo licha ya wanachama kusota kwa miezi 13, kuna tuhuma za rushwa ndani yake, hivyo naagiza vyombo vya usalama vifanye kazi yake,” alinukuliwa Makala.
Kwa upande wake, meneja huyo wa KCBL hakukubali wala kukanusha kuhojiwa na Takukuru kuhusiana na tuhuma hizo na badala yake alisema amepewa ushauri na watu (hakuwataja) kutozungumzia uchunguzi huo unaofanywa na Takukuru.
Taarifa zilizopatikana wiki iliyopita na kuthibitishwa na Takukuru wenyewe, zimedai kuwa meneja huyo amehojiwa kutokana na kuwapo na mazingira ya rushwa katika mchakato mzima wa kuwapatia mikopo wajasiriamali hao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KCBL, Reginald Hosea, pamoja na kukiri kuwapo kwa uchunguzi dhidi ya maofisa wa benki hiyo, amesema wanasubiri uchunguzi wa Takukuru na taarifa rasmi ya uchunguzi juu ya tuhuma hizo.
Amesema suala hilo lilitokea wakati wao wakiwa hawajaanza kazi rasmi licha ya kuchaguliwa na mkutano mkuu mwanzoni mwa mwaka jana, na kuongeza kuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ndiye aliyeagiza uchunguzi huo, hivyo wanatarajia kupata majibu ya uchunguzi huo kutoka vyombo sahihi.
Wakati meneja huyo akiangukia mikononi mwa Takukuru, mwanachama wa Vicoba Endelevu mkoani Kilimanjaro na mmoja wa wajasiriamali waliokuwa wanufaike na mikopo hiyo, Vicent Mulamba, ameshikilia msimamo wake wa kuiburuza mahakamani benki hiyo.
Vicent anadai kuwa benki hiyo ilimdanganya kuwa itampatia mkopo wa Sh milioni 50 ili aboreshe maisha yake, lakini kinyume cha hapo mkopo huo hadi leo umekuwa ni kitendawili kisichoteguliwa licha ya kutimiza masharti yote aliyopewa yeye na wajasiriamali wenzake likiwamo la kuwa na mchanganuo wa biashara.
Tayari mjasiriamali huyo ameipa barua benki hiyo ya kusudio lake la kuifikisha mahakamani na nakala za barua hiyo ya Machi 4 mwaka huu kutumwa kwa Mkurugenzi wa NSSF kupitia kwa Meneja wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anjela Mollel, ambaye ni mmoja wa viongozi wa Vicoba Endelevu na H. M. Associates, kampuni iliyohusika na michanganuo ya mikopo.
Inadaiwa kuwa mmoja wa maofisa wa Idara ya Mikopo katika benki hiyo, anatuhumiwa kupokea rushwa ya sh 100,000 kutoka kwa kila mwanachama wa Vicoba, fedha ambazo zilidaiwa ni za ‘kulainisha’ upatikanaji wa mikopo.
“Bila halali yoyote, mlinidanganya ya kwamba sina sifa za kukopesheka hadi pale nitakapojiunga na Vicoba Endelevu, niwe mwanachama wa NSSF, nifungue amana au niwe mteja wa Benki ya KCBL lakini pia niwe na mchanganuo wa biashara,” alisema na kuongeza:
“Bila halali yoyote mlinidanganya kwamba maendeleo yangu yataendelea kudorora ikiwa sitachukua uamuzi wa haraka wa kuchangamkia fursa ya mkopo mnono kwa kutii masharti katika muda mfupi.”
Mwanachama huyo anadai kuwa kutokana na ushawishi alioupata kutoka kwa maofisa wa benki hiyo, aliamua kuacha kazi zake zote ambazo zilikuwa zikimwingizia kipato na kuelekeza nguvu zake zote kwenye maelekezo aliyopewa na maofisa wa benki hiyo.
Miongoni mwa masharti anayodai alipewa na kuyatekeleza ni pamoja na kujiunga kwenye Vicoba Endelevu na kutoa kiingilio cha Sh 120,000, kugharamia uzinduzi wa Vicoba Endelevu kwa kutoa sh 20,000 pamoja na kununua fulana kwa kiasi cha sh 8,000 kwa ajili ya kuvaa wakati wa uzinduzi huo.
Masharti mengine anayodai alipewa na kuyatekeleza ili apatiwe mkopo huo, ni kujiunga na NSSF kwa kulipa ada ya miezi sita kwa kiwango cha Sh 20,000 kila mwezi ili kukidhi masharti ya mkopo na kufungua akaunti kwenye benki hiyo kwa kiasi cha Sh 30,000.
Pamoja na masharti hayo, pia wana-Vicoba wote waliohusika katika mchakato wa kupatiwa mkopo na benki hiyo, walipewa sharti la kuandikiwa mchanganuo wa biashara na kuelekezwa mchanganuo huo ufanywe na kampuni ya H. M. Associates ambako kila mwanachama alitozwa kiasi cha sh 250,000.
Amelalamika kuwa pamoja na kukamilisha masharti aliyopewa na benki hiyo ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti katika benki hiyo, uongozi wa benki hiyo umekataa kumkopesha kiasi cha Sh milioni 50.
“Mtandao wenu wa kunilaghai umeniathiri, kwa sababu hiyo ninataka mnilipe fidia ya madhara ya kiasi cha Sh milioni 30 ili akili yangu itulie na kufanya biashara mliyonichochea kuifanya,” inasema barua hiyo.
Benki ya KCBL inakusudiwa kushitakiwa mahakamani kujibu tuhuma za kumdanganya mwanachama wa Benki ya Kijamii Vijijini (Vicoba) kuwa benki hiyo ingempatia mkopo wa Sh milioni 50.
Mwanachama huyo, Vicent Mulamba, ameipa KCBL hati ya kusudio la kuifikisha mahakamani kwa kile anachodai ilimdanganya mkopo licha ya kutimiza masharti.
Nakala ya barua hiyo ya Machi 4, mwaka huu, ambayo JAMHURI ina nakala yake imepelekwa kwa Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupitia kwa Meneja wake Mkoa wa Kilimanjaro, Angela Mollel.
Mollel ni mmoja wa viongozi wa Vicoba Endelevu; pamoja na Kampuni ya H. M. Associates iliyojihusisha na michanganuo ya mikopo.
Meneja wa KCBL, Elizabeth Makwabe, amekiri kupokea hati hiyo ya kusudio la kufikishwa mahakamani, lakini akagoma kuingia kwenye undani wa suala hilo.
Sakata latinga Takukuru
Takukuru imeamua kuingilia kati mgogoro wa mikopo kwa wanachama zaidi ya 4,000 wa Vicoba katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Taasisi hiyo inachunguza majalada 56 yanayotokana na tuhuma 126 zilizofikishwa katika ofisi hiyo mkoani Kilimanjaro. Taarifa za awali zinasema Takukuru imejiridhisha majalada hayo yameiwezesha kuwa na msingi wa uchunguzi.
Miongoni mwa tuhuma zinazochunguzwa zinagusa ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka katika kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Alexander Kuhanda, amesema tuhuma 126 zilipokewa na kuzipitia, ofisi yake imefungua majalada 56 huku maeneo yaliyoonekana kulalamikiwa zaidi ni rushwa katika vyama vya ushirika vya msingi.
Maeneo mengine ni idara za ununuzi katika ofisi mbalimbali za Serikali na mfumo unaosimamia Vicoba katika Mkoa wa Kilimanjaro. Amesema wana-Vicoba zaidi ya 4,000 wanahangaikia mikopo katika KCBL.
Maofisa watatu wa benki hiyo wamehojiwa kuhusu mikopo ya wanachama wa Vicoba Endelevu.
Baadhi ya watumishi wa umma wameshafikishwa mahakamani wakituhumiwa kufuja mali za umma, kughushi na matumizi mabaya ya madaraka.
Takukuru imesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, imeokoa Sh milioni 33 kutoka kwa mfanyabiashara mmoja aliyekuwa anakwepa kodi kwa kutumia namba feki ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN). Jina lake halikutajwa.
Takukuru imesema mafanikio iliyopata katika kipindi cha miezi mitatu, yametokana na mwitikio wa jamii katika kutoa taarifa na utayari wa kuipa taasisi yake ushirikiano.