DAR ES SALAAM
Na Dennis Luambano
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (68), hatimaye amefichua mambo yaliyomfanya asielewane na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli.
Membe ambaye ni mmoja wa mashushushu hodari nchini, amesema Rais Magufuli pamoja na mambo mengine, alimfitini hadi akakosa nafasi ya kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola. Jumuiya hiyo ni ya nchi 53 wanachama zilizokuwa makoloni ya Uingereza.
Katika mahojiano maalumu na JAMHURI yaliyofanyika nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita, Membe anasema hajui hasa kisa cha Magufuli kumfitini, lakini anadhani chanzo ni moyo aliokuwa nao kiongozi huyo. Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17, mwaka huu.
Membe ambaye amekuwa mbunge wa Mtama kuanzia mwaka 2000 hadi 2015, anasema baada ya Rais Magufuli kukataa kumuidhinisha kuwa katibu mkuu wa jumuiya hiyo ndipo mashambulizi yalipoanza dhidi yake, na anamtuhumu mtangazaji Cyprian Musiba, kama mmoja wa watu waliopewa kazi hiyo. Wiki iliyopita, Mahakama Kuu ilimpa ushindi Membe na kumtaka Musiba amlipe Sh bilioni 7 kama fidia kwa kumchafua.
“Musiba alikuwa anafanya hiyo kazi ya kunichafua na kunisingizia uongo wa uhaini kwa maelekezo. Jibu lake ni rahisi kabisa, uongozi wa juu wa nchi na uongozi wa juu wa chama, hapo kuna Dk. Bashiru Ally (aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM) na Humphrey Polepole (aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM).
“Wote huo ulikuwa ni wasiwasi tu wa uchaguzi wa urais wa mwaka 2020, walidhani kwamba kichwani mwao kabisa ikifika mwaka huo wa 2020 Membe angekuwa tishio la kuchukua urais,” anasema.
Membe anasema hakunuia kugombea urais mwaka jana kama ilivyodhaniwa, lakini akalazimika kufanya hivyo kutokana na yaliyojiri wakati huo.
“Sikuwa nimenuia kugombea urais, mbona mwaka 2015 sikuwa nimenuia? I was provoked, nilistaafu vizuri nikawa na shughuli zangu vizuri na nilikuwa niwe Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, ndiyo kazi niliyokuwa ninataka kuifanya tangu Novemba 2015, lakini yeye Magufuli akakataa. Kwa sababu ili upate nafasi hiyo lazima uidhinishwe na rais wa nchi yako, lakini alikataa tu,” anasema na kuongeza:
“Septemba 2015 tulikwenda UN (Umoja wa Mataifa) katika mkutano wa General Assembly. Tulipofika pale kikafanyika kikao cha Mawaziri wa Jumuiya ya Madola na moja ya ajenda ni kupendekeza kwa viongozi wakuu kuteua jina la kupendekeza la mtu atakayeshika nafasi ya ukatibu mkuu, kwa sababu aliyekuwapo alikuwa anamaliza muda wake wakati huo.
“Miongoni mwa mawaziri pale UN wakaamua kumchagua mtu aliyekuwa Mwenyekiti wa Commonwealth Ministiries Action Group (Kamati ya Kumchagua Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri) atakayeshughulikia migogoro yote ya Jumuiya ya Madola katika kipindi cha miaka miwili.
“Na huyo atatufaa, na mtu huyo alikuwa ni Bernard Kamillius Membe. Kikao kile kilifanyika nikiwa safarini kwenda India kumuangalia kaka yangu aliyekuwa mahututi wakati ule, alifariki dunia na kikao kile nilikikosa kwa wiki moja tu. Nilimuagiza Balozi Peter Kallaghe ahudhurie kwa niaba yangu, wakati huo ni balozi wetu pale Uingereza na kwa kuwa Jumuiya ya Madola inakutana na makao makuu yake ni London, Kallaghe akaenda kuniwakilisha wakinisubiri mimi.”
Anasema wakati huo hata Rais Jakaya Kikwete alitaarifiwa na akasema hana pingamizi na baada ya pale wakarudi nchini na wakaanza maandalizi, na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola ikaja kumuona na Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo wakati huo, Waziri Mkuu wa Malta, Josephat Muscat, akamuita kwenda kumuona kabla ya mkutano huo.
Membe anasema alipokwenda Malta kumuona akapewa baraka zote na wakamweleza kuwa anapaswa kuunda sera mpya, na hapa nchini wakatengeneza kamati iliyokuwa chini ya Balozi Liberata Mulamula wakati huo akiwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Mulamula ambaye kwa sasa ni waziri wa wizara hiyo, naye mapema mwaka huu, na Likwelile Servasius majina yao yalikatwa na Rais Magufuli wasigombee nafasi nyeti za kimataifa.
“Wakati kamati hiyo inafanya kazi yake, Magufuli tayari akawa ni Rais. Ndipo Mulamula akaitwa na Magufuli na kupigwa marufuku kuandaa hiyo kamati kwa ajili ya kunifanya mimi niwe Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo,” anasema.
Membe anasema si hilo tu, bali ili katibu mkuu achaguliwe anahitaji Rais wa nchi husika akamwelezee katika vikao vya viongozi wakuu wenzake.
“Wanakwenda huko wanakaa siku nzima na moja kati ya shughuli wanazozifanya ni kuteua Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola. Kwa hiyo rais wangu alitakiwa aende pale akasome CV (wasifu) yangu na kuwaambia wenzake waniunge mkono,” anasema na kuongeza:
“Hadi wanakwenda Commonwealth nilikuwa na nchi 32 zinaniunga mkono kati ya 53, na hata kabla ya kule nilikuwa nimeshavuka asilimia 50. Wakati Magufuli akiwa hapa akakataa kwenda Malta; na rais wako asipokwenda, basi kazi imekwisha. Akakataa kwenda kwa maelezo yuko ‘bize’ kutengeneza baraza lake la mawaziri – kama mnakumbuka ilimchukua zaidi ya mwezi mmoja kutengeneza baraza.
“Akakataa, kwa hiyo aliua Kamati ya Jumuiya ya Madola pia akakataa kwenda Malta. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alinipigia, akaniambia nimeongea na Abdulrahman Kinana (wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa CCM) na naongea na wewe – kama rais wako haendi anitume mimi kwa sababu mimi ni Mwenyekiti wa EAC (Jumuiya ya Afrika Mashariki) nikazungumze kwa niaba yake. Rais wetu akakataa, sasa unataka ushahidi gani zaidi wa kuonyesha Rais alikataa?”
Membe anasema Kinana akasaidia kwa kumfuata Rais Magufuli na kumwambia kama haendi amruhusu Kenyatta aende kwa sababu kule kuna fedha nyingi.
“Kule Commonwealth kuna fedha, wewe fikiria nilikuwa ninakabidhiwa Paundi bilioni saba za Commonwealth Fund. Sekretarieti ilipokuja hapa kuni-brief.
“Nilikuwa ninakabadhiwa fedha hizo kwa ajili ya technical fund kwa ajili ya kusomesha watu nje ya nchi, fedha za maafa, kuwawezesha wanawake, kupambana na magonjwa, tukakiacha kiti kikaenda Trinidad na Tobago, ujinga mkubwa,” anasema.
Membe anasema baada ya hayo kutokea hakuzungumza na Magufuli na hakupenda kabisa kumuona.
“Sasa after the facts iweje? Na alishaonyesha wazi mimi kutopata nafasi hiyo, wala sikumtafuta na sikutaka kujidogosha kiasi hicho. Wakati huo sikufanya ubaya wowote ndani ya chama (CCM) kwa sababu tuliteuliwa watu watano yeye akapita tatu bora na nilishiriki kwa Mkoa wangu wa Lindi kumfanyia kampeni huku nikibembeleza nikijua kuna Commonwealth position,” anasema na kuongeza:
“Tulikwenda vizuri hadi Novemba alipovunja ile kamati ya Commonwealth, akakataa kwenda Malta, akakataa kumruhusu Kenyatta, common sense inasema ni ushindani wa nafasi ya urais ndani ya chama. Sasa baada ya hapo yakaanza mashambulizi from no where katika vyombo vya habari ndipo akazuka Musiba.”
Anasema baada ya ushindi wa Magufuli yeye Membe alihojiwa na gazeti moja la kila siku na akaulizwa ushauri wake kwa rais kujenga uhusiano na dunia.
Membe anasema akajibu haiwezekani kutosafiri kwa sababu rais lazima aende nje, kwa kuwa Tanzania haiwezi kujitenga, pia akienda nje atajenga uhusiano.
“Kupitia vyanzo vyangu, nikasikia anasema unaona, mimi nimesema siendi nje huyu ananipinga. Mara sasa ikaanza katika gazeti inatoka mara huyu ni mhujumu, mara anafanya hivi, nikajiuliza hiki kitu kinatoka wapi?”
“Inakwenda… inakua na wala mimi sikujibu, inakua inakua hadi likatengenezwa gazeti mahususi kwa ajili ya kunishambulia, kila toleo lilikuwa linanishambulia, picha yangu inakuwa kubwa hata kama tuko wanne, Membe ni mtu hatari katika nchi hii, Membe apagawa, Membe kumhujumu Rais, ala fedha za Libya.
“Sasa mimi nimetoka katika intelligence, nina network, there is no doubt at all kwamba Magufuli, Bashiru na Polepole ndio walikuwa wanahusika. Kwa hiyo nikavumilia, lakini kilichoniuma ni pale Bashiru alipojitokeza rasmi kumuunga mkono Musiba na kunipiga vita mimi. Nikiwa Zimbabwe katika uchaguzi nikasema kumbe ndiyo tumefikia katika pointi hiyo.
“Chama nilichotegemea kingemuita Musiba pamoja na mimi ndani ya ofisi kimyakimya na kutuuliza kulikoni watu nyinyi, lakini Bashiru anakwenda public na anasema kabisa huyu bwana ana shutuma mbalimbali zinamkabili aje ofisini kwangu muda wowote atakaporejea anione.
“Mimi nikasema sawa katibu mkuu, utaratibu uliotumia kuniita si ethical ndani ya chama chetu na kwa sababu wewe ni mgeni katika hiki chama nitakuja, pia ninataka uniite na huyo anayezusha hayo masuala dhidi yangu. Muite na aje athibitishe kweli ndipo utakapolimaza tatizo kati yangu na Musiba.
“Bashiru akajibu kabla sijarudi kwamba sina haki ya kumpangia yeye nini cha kufanya, kwa hiyo ninayeitwa ni mimi tu na si Musiba, nikarudi hapa nikamwandikia barua ya kumuomba siku na tarehe ya kukutana naye, lakini hajajibu hadi leo,” anasema.
Anaendelea kusema kuwa alipokwenda katika kikao cha Kamati ya Maadili cha CCM akamuuliza Bashiru kwanini hakumjibu, akamwambia angeenda tu wakasikilizana.
“Nikamwambia wewe, mimi siwezi kuwa mjinga, ndiyo maana nikaomba siku na muda, kuna unyonge hapo, hata Mangula (Makamu Mweyekiti CCM Bara) aliniunga mkono akasema Bashiru amechemka, njoo tarehe fulani kwa maandishi kama nilivyoomba. Kama alitaka nije muda wowote nijibu basi – ijibu barua yangu, wewe uje muda wowote ule unione lakini haikujibiwa,” anasema na kuongeza:
“Kwa hiyo nilipogundua CCM inamshabikia Musiba, haitaki kushughulikia hili tatizo, nikaona sasa hakuna sehemu yoyote ya kukimbilia zaidi ya chombo kimoja kikubwa zaidi ambacho kinashughuikia haki za watu ambacho ni Mahakama Kuu.”
Kwake kuna mazuri yaliyofanywa na Magufuli?
Kuhusu mambo mazuri yaliyofanywa na uongozi wa Rais Magufuli, Membe anasema katika siasa kila mtu ana mazuri na mabaya yake.
Anasema tatizo la siasa ni moja tu, hata ukiwa na mazuri 99 na ukaharibu jambo moja, ukaua mtu mmoja, au ukaua mwandishi wa habari mmoja au wawili au ukafanya jambo moja la ovyo au lolote lile baya au doa moja tu linakuharibia.
Anasema si wingi wa mazuri aliyoyafanya mtu au kiongozi wa kisiasa, ila doa moja ndilo linalomharibia, huku akikiri kwamba zuri moja kubwa peke yake lililofanywa na Rais Magufuli ni miundombinu.
“Katika miundombinu alifanya vizuri ingawa kwa gharama kubwa, barabara ni miundombinu, ndege ni miundombinu, shule ni miundombinu, afya ni miunombinu, alikuwa Rais wa miundombinu, alitokea kuwa waziri wa miundombinu na akawa Rais wa miundombinu.
“Rais wa nchi lazima awe na uelewa mpana wa mambo mengi, aelewe na siku zote nilikuwa ninasema hamkunielewa. Nyuki anatengeneza asali tu na anafanya jambo jema, lakini hafai kuwa kiongozi, hawezi kuwa rais akasema anatengeneza asali tu, yaani kuanzia mwanzo hadi mwisho tunakula asali tu, asali tu.
“Kiongozi lazima ujue una wizara 27 na zote zina uzito, jeshi lako umeliwekaje kwa ajili ya kupambana na nchi nyingine, hiki si kipindi cha kuiruhusu Rwanda kwenda kuisaidia Msumbiji kupambana na magaidi.
“Msumbiji ni mtoto wetu, uhuru wa Msumbiji sisi tumeutafuta, sisi ndio tumezaa Msumbiji, mimi ukiniuliza nani jirani yetu wa kweli katika dunia hii, ni Msumbiji, hakuna nchi yoyote ambayo ni ndugu kupita Msumbiji, hakuna, huwezi ukaitelekeza Msumbiji.
“Kamwe ni dhambi kubwa, ni lazima majeshi yetu yawe yameimarishwa kwa maana ya lojistiki zake na fedha ili kusaidia nchi jirani kama Msumbiji, huhitaji kuombwa na Msumbiji kwenda vitani. Kama hamjui Msumbiji ni nchi pekee ambayo adui akiingilia kule ujumbe utakuja hapa kutunong’oneza kwamba pale bandarini kwake kuna silaha zinakwenda mahala fulani tunafanyaje? Na hakuna nchi nyingine inayoweza kufanya hivyo ila Msumbiji inaweza.”
Membe anasema moyo wake unaumia anapoona nguvu kubwa inawekwa katika miundombinu peke yake, lakini chombo nyeti (anakitaja) kinakwenda chini.
“Unashindwa sasa kusimama na unamuacha tu mtu mwingine anatamba. sijui sisi tunakwenda kuisaidia Msumbiji, kuna watu wanafanya kitu fulani. Mungu wangu, na hii yote ni kwa sababu hatuzipi uzito wizara zote wakati wote,” anasema na kuongeza:
“Haijawahi kutokea katika dunia yetu tangu tumepata uhuru unaiacha nchi ya jirani, unaacha mtu wa kaskazini anakwenda kuisaidia Msumbiji, tumeiacha Sahara Magharibi, na Palestina hivyo hivyo. Si hivyo tu, mkutano unaitwa Angola mwaka 2019, vyama vya ukombozi sita vya MPLA, ANC, SWAPO, CCM, ZANU PF na FRELIMO vinaitwa katika mkutano wa mshikamano na Polisario.
“CCM kupitia kwa Polepole inakataa, inasema hatutaki ajenda hii tuizungumzie na wala haituhusu, nyinyi mnaweza kuishughulikia nayo ila sisi hatutaki! Kweli, sisi tulikuwa Mwenykiti wa Kamati ya Ukombozi Afrika tangu mwaka 1963, Hashimu Mbitta angekuwapo angelia na kufa siku hiyo hiyo.”
Anasema sisi si wa kuiacha Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Palestina, na hiyo yote inaonyesha kwamba unapokuwa na rais wa nchi lazima awe na uelewa mpana wa mambo mbalimbali kwa kuunganisha taaluma na ujuzi awe nazo zaidi ya moja au mbili na aelewe umuhimu wa ulinzi, miundombinu, kilimo na vitu vingine.
“Lazima rais uulize, mwaka huu kilimo kimetupa mapato ya kiasi gani na matatizo yalikuwa wapi na waziri aweze kujibu kwamba mwaka huu tulipata dola bilioni 8 za Marekani kwa kuuza mazao kadha wa kadha, mwakani tutaongeza hiki na kile, kwa sababu tunataka kupata dola bilioni 16 za Marekani.
“Kwa sababu tunataka kuingiza bio-chemical inputs, mbolea au nini katika mazao fulani fulani, lakini kila siku daraja, barabara, lami, hapana kwanini unakuwa rais wa miundombinu peke yake unakuwa kama nyuki unatengeneza asali peke yake?” anahoji.
Nini kinamvutia kwa Serikali ya Rais Samia?
Kuhusu mwenendo wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, anasema kitu cha kwanza ni raha ya Watanzania ya kupokea mabadiliko ya uongozi wa nchi.
Pili, anasema kuingia kwa Rais Samia ambaye ni mwanamke, hewa ya uhuru na usalama nayo ikaingia nchini na kwa sasa hakuna lugha ya watu wasiojulikana kwa kuwa msamiati huo unaanza kufa.
“Sasa hivi husikii watu kukamatwa au kuona maiti zinaelea baharini au mtu kafa, husikii upotevu wa binadamu wenzako, wafanyabiashara au watu wa kawaida, kwa Watanzania hii lazima tuithamini,” anasema Membe na kuongeza:
“Nilihudhuria mazungumzo ya Bill Clinton na Jakaya baada ya kustaafu, Jakaya alimuuliza Clinton swali – uchaguzi unaendeleaje Marekani? Kwa sababu Hillary Clinton alikuwa anagombea wakati huo.
“Akajibu uchaguzi unaendelea. Je, kuna matumaini mama anaweza kushinda? Akasema hapana hakuna matumaini hayo kwa sababu wahafidhina wanafanya kosa kubwa kwa kudhani wakimchagua Hillary kuwa Rais wa Marekani atakuwa ananiiga mimi (Clinton).
“Akasema hakuna marais wanaofanana, asikudanganye mtu, hakuna, wao wana miaka zaidi ya 250 ya uhuru wao na marais wanajuana wote na hakuna rais atakayefanana kwa maneno na vitendo na rais mwenzake, kwa sababu kila rais atakutana na changamoto zake ambazo akiangalia nyuma hazijawahi kutokea, sasa unaiga nini?
“Clinton akasema hata ukimlazimisha Hillary amuige hawezi, kwa sababu kila mtu anatawala katika mazingira ambayo ni tofauti na ya jana, akasema kwa hiyo wahafidhina wa Marekani wanafanya kosa kwamba tukimchukua huyu atafanya hivi.
“Haiwezekani, kwa sababu wewe Kikwete ulikuwa na changamoto zako tofauti na Mkapa, na Mkapa alikutana nazo tofauti na Mwinyi, kwa hiyo wewe haiwezekani changamoto zako zikafanana na Mkapa. Huwezi kusema mimi niliendeleza shughuli za Mkapa, hapana, huwezi kusema hivyo.”
Katika hatua nyingine, anasema pia si sahihi kusema kwamba Rais Samia afanane na Magufuli kwa sababu yeye ana changamoto zake ambazo ni lazima ziende kwa uwiano wa kipekee na mazingira yake anayokutana nayo.
Anasema kwa sasa anachokifanya Samia ni kizuri, kwa sababu anaangalia swichi kubwa ya umeme na vitufe vyote vilikuwa vimezimwa, kwa mfano swichi ya mambo ya nje ilikuwa imezimwa na sasa ameiwasha.
“Swichi ya Bunge ‘live’ ilikuwa imezimwa nayo akaiwasha, ile ya gesi ya Lindi ilizimwa na yeye kaiwasha na sasa kuna mazungumzo na ndiyo utaalamu mzuri.
“Na unaona kabisa huyu mama anajua madhara ya swichi kuzimwa na kuwasha na lazima tumpe heshima yake na huyu ni mama, duniani kuna wanawake sita tu viongozi wa nchi na mmojawapo ni Rais Samia wanaoongoza na hiyo ni bahati.
“Tunapopata bahati hii lazima tuiheshimu, tukianza hapa huyu mama hatufai ataondoka. Katika siasa ili ukubalike nchini na duniani kuna mambo lazima yafanyike, haki za msingi za binadamu – kwanza uthamini kwamba umwagaji wa damu ya Mtanzania mmoja itakugharimu, kwamba ni lazima ukiwa kiongozi uzingatie uhuru wa vyombo mbalimbali, kuwe na uhuru wa wananchi wako kwenda kokote wanapotaka.
“Tatu, demokrasia na utawala bora, lazima tuwe na uongozi wa sheria na pia tuwe na demokrasia na unapokuwa hivyo unakuwa na taasisi za kidemokrasia. Mfano vyama vya upinzani viheshimu. Kwa hiyo huo ndiyo msingi wa uongozi. Kwa hiyo ni lazima utengeneze muundo au mfumo wa kwako unaoutaka wewe, lakini si lazima ufanye hivyo siku hiyo hiyo.”
Membe anasema ukiwa kiongozi lazima ujiulize, kwanini fulani alikuwa anapenda mfumo huu au ule na utajifunza. Na kuna kitu kinaitwa mpito na anaamini kwa sasa bado tuko katika kipindi kifupi cha mpito.
“Sasa mtu mwingine atakwambia kipindi cha mpito cha miezi sita ni kikubwa sana, hapana, kumbuka hii ni siasa, kuna mashimo katika njia hiyo hiyo na miiba. Kwa hiyo lazima uje taratibu kumpa nguvu mama na kumpa muda ili aweze kufanya marekebisho,” anasema na kuongeza:
“Huyu ni mama, mama yeyote yule hata mama yako mzazi ni mtu ambaye hakawii kukata tamaa, nyinyi watoto wote mkienda kinyume naye ataumwa kichwa, tofauti na baba yenu ambaye atawachapa. Mama Samia lazima tumpe heshima yake.”
Membe anasema atamuunga mkono Rais Samia mwaka 2025 na hiyo inaeleza tafsiri yake kwamba hapa katikati asiwe na wasiwasi wowote ule.
Anasema atakwenda mbali zaidi na Rais Samia, kwa sababu kuna nguvu zinapenda aondoke na sasa wanachotakiwa kufanya ni kumpa moyo na kumpa nguvu kwamba wanamuunga na watamuunga mkono.
“Kwamba suala la kumuunga mkono kwake lisiwe tatizo na hivi ndivyo inavyokuwa,” anasema Membe.
Kwa mengine mengi, yakiwamo uhusiano wake na Edward Lowassa, Rostam Aziz, mgombea binafsi, Katiba mpya, utawala wa Rais Jakaya Kikwete, alivyoishi ndani na nje ya CCM, na safari yake ya kurejea CCM; usikose toleo lijalo.