Wanaukoo wa Burito ambao ndiyo chimbuko la ukoo wa Chifu Nyerere Burito, hivi karibuni ulifanya Mkutano Mkuu wa Ukoo wa mwaka 2015.
Mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi. Kulikuwa na wageni waalikwa wengi, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
  Haikushangaza kumuona Membe kijijini Butiama kwa sababu mara zote, na katika maandiko yake, anamtambua na kumheshimu Mwalimu Nyerere kama kiongozi aliyemvutia kiasi cha kumfanya awe mwanasiasa.
  Wanaukoo wengine waliokuwa wahudhurie Mkutano huo, lakini wakawa na safari nje ya nchi ni Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Jaji Joseph Warioba.


  Shughuli nyingi za Membe zinamfanya awe nje ya nchi kwa muda mrefu. Hali hiyo imemfanya aonekane Butiama kwa nadra. Pengine ni kwa sababu hiyo, ujio wake siku hiyo ulikuwa wenye mvuto wa aina yake. Alishangiliwa muda wote wa kuwasili na hata baada ya kumalizika kwa Mkutano majira ya jioni.
  Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, alikuwapo. Baada ya kumalizika kwa Mkutano, Mkono alimchukua Membe na kumpeleka kwenye miradi mingi ya shule aliyoijenga kwa mabilioni ya shilingi na kuikabidhi Serikali na taasisi za kidini.
Awali, alimpeleka sehemu ya ‘Cuba’ kunakotarajiwa kujengwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere. Baadaye alimpeleka katika Shule ya Wasichana ya Chifu Edward Wanzagi. Hapo Membe alilakiwa kwa shangwe kubwa na wanafunzi na walimu.
 Alipata wasaa wa kuzungumza na wanafunzi, na maneno yake yakawa kuwasisita wapende kusoma ili wajiandae kulitumikia Taifa. Alistaajabu kwa uzuri wa majengo na uwekezaji uliofanywa na Mkono.


  Baadaye alikwenda katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Oswald Mang’ombe. Hapo Membe alijionea majengo makubwa, mazuri na yenye huduma zote za kimasomo. Kama mipango itakwenda ilivyopangwa, majengo hayo yatakuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Sayansi na Kilimo.
  “Someni kwa bidii, nimetembea nchi yote hii, sijawahi kuona majengo mazuri ya shule ya sekondari kama haya. Nimeona mnayatunza, naomba muendelee hivyo hivyo ili myatumie ninyi na wadogo zenu watakaokuja baadaye,” Membe aliwaambia wanafunzi hao wa kidato cha tano na cha sita wa mchepuo wa sayansi.
 
Alichoiambia hadhira ya Burito
 
Membe alitumia muda mfupi kuzungumza maneno mazito ya kumsifu Mwalimu Nyerere, akisema ameipatia sifa kubwa Tanzania. Akasema wakati wa msiba wake mwaka 1999 viongozi na walimwengu wengi sana walimlilia kutokana na kutambua mchango wake kwa maendeleo ya wanadamu.
 “Mwalimu alipofariki, pale ubalozi wetu jijini Ottawa tuliweka vitabu 15 vikubwa (vya waombolezaji kuweka saini) na havikutosha. Umati wa viongozi wa dunia waliomiminika Ottawa, Canada kuomboleza pamoja na ndugu zao Watanzania walikuwa wengi sana.


  “Mwezi uliopita nimesema na leo narudia, jengo kubwa lililopo Addis Ababa, Ethiopia linalotaka sasa kushughulikia masuala ya amani na usalama limepewa jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa heshima ya nchi yetu.
  “Hapa nyumbani sihitaji kusema chochote kuhusu sifa kubwa za kiongozi huyu wa dunia. Mtanzania yeyote duniani na aliyeko nchini anajua Butiama ni kwao. Anajua wana-Burito ni nani. Wanamjua Chifu Edward Wanzagi pamoja na kaka yangu Japhet (Chifu Japhet Wanzagi). Wanajua Butiama iko wapi.
  “Wanajua wapi Mzee Chifu Nyerere amelala na leo tumeweka mashada hapa. Ni kijiji pekee katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachojulikana vizuri sana, na sasa hivi ni wilaya. Hongera.


  “Kwa hiyo, tunapokutana siku ya leo kusherehekea pamoja na wana-Burito, tunamkumbuka mkombozi wa Taifa, Afrika na wa dunia.”
  Membe hakusita kulaani taarifa za uzushi zilizosambazwa kwenye mitando ya jamii zikidai Mama mjane wa Mwalimu Nyerere, Mama Maria Nyerere, alikuwa amefariki dunia. Taarifa hizo ziliibua taharuki, kiasi cha kuwafanya watoto wake wawili – Andrew Burito na Emil Magige – na wanandugu wengine wakose amani kwa muda. Hata hivyo, baadaye taarifa ilitumwa na binti wa Mama Maria, Anna Watiku, kutoka Dar es Salaam ambaye alithibitisha kuwa Mama Maria alikuwa mzima.
  Membe akasema: “Ni bahati mbaya kwamba tunapokuwa hapa tunasherehekea habari hii, wenzetu wasiotutakia mema wanaleta kwenye mitandao taarifa za uongo.
 “Nakushukuru Jackton kwa kukanusha; kwa simu zilizoingia kwa maandishi zinazozungumza jambo la hatari sana na la kipuuzi kwamba mama yetu (Mama Maria Nyerere) hayupo (amefariki dunia). Nachukua nafasi hii kwanza kuungana na Jackton kuzikanusha habari hizi kwa nguvu zote, lakini pili nachukua nafasi hii kuwaonya Watanzania kumwacha mama peke yake — tusimwingize katika masuala la kipuuzi yenye nia mbaya ya kutaka kusononesha watu hasa siku ya leo ambapo kila mtu amekuja kufurahia shughuli hizi. Wamuache peke yake.
  “Ndugu zangu wana-Burito, kwangu mimi kuja hapa kulinifanya nikubali kwa sababu mbili kubwa. Kwanza kwa sababu ya ukaribu huu tulionao na wana-Burito wengi na wazee na chifu. Niliona kwa kuwa nina nafasi isingekuwa vema nisije. Lakini pili unapopata nafasi ya kuja Butiama, au kualikwa Butiama, pia unapata nafasi ya kuja kuzuru makaburi, si tu ya kina mzee Edward Wanzagi, lakini unapata faraja ndani ya moyo unapokuja kuzuru kaburi la Baba wa Taifa. Kwa hiyo nilikimbilia haraka sana kuja kwa sababu hizi.


  “Naomba nimalize kwa kuwatakieni tena kila la kheri katika sherehe hizi, na sisi wenzenu wa nje tunajifunza mshikamano wa kweli wa ukoo huu wa wana-Burito ambao si rahisi kuukuta kwenye koo nyingine.
 " Tumejifunza mengi, mmeleta kiongozi wa dunia. Muendelee na mshikamano huu, na insha'allah Mwenyezi Mungu atawapa maisha marefu. Asanteni sana kwa kunialika. Chifu Japhet Wanzagi nakutakia maisha marefu sana ili uongoze jamii ya wana-Burito. Wazee wote wa Kizanaki na wana-Burito nawatakieni maisha marefu sana na mkae mkijua mlileta chombo duniani; chombo ambacho kitaendelea kukumbukwa milele na milele. Asanteni sana kwa kunisikiliza.”
 
Maneno ya mgeni rasmi Dk. Reginald Mengi
 
Dk. Mengi aliyekuwa ashiriki mkutano huo, alipata dharura, hivyo akamtuma mwakilishi wake, Jesse Kwayu, amwakilishe.
 Kwenye risala yake, Dk. Mengi alisema: “Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyekiti wa Ukoo wa Burito, Chifu Japhet Wanzagi, na wanaukoo wote wa Burito kwa ujumla kwa kunipa heshima na nafasi hii ya kuwa Mgeni Rasmi wa Ukoo katika Mkutano wenu wa Ukoo wa mwaka 2015. Naona fahari kubwa kwa heshima hii mlionipa na ninasema asanteni sana sana.
  “Napenda pia kuchukua fursa hii kuupongeza Ukoo wote wa Burito kwa utamaduni huu mzuri ambao mmejijengea kwa kukutana kila mwaka. Hakika ni jambo jema ambalo ningependa pia kushawishi na koo nyingine nazo ziige utaratibu kama huu. Ni jambo jema ndugu kukutana pamoja kwani hata maandiko matakatifu yanasisitiza ndugu kukaa pamoja kwa upendo.


  “Sote tupo hapa tukiungana na ukoo huu ambao ndiyo chimbuko la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Kwa Watanzania, Mwalimu alikuwa ndugu, kiongozi, mchungaji na mtu mwema ambaye Mungu alitupa na kutuongoza katika kipindi chake cha utawala ambacho aliweka misingi imara ya Taifa hili kiasi kwamba leo tunajipiga kifua tukiishi kwa utulivu na amani.
  “Kazi na matendo ya Mwalimu kwa Taifa hili yametufanya kumwona kila siku akiwa nasi. Ingawa kimwili Mwalimu hayupo nasi baada ya kutangulia mbele ya haki mwaka 1999, bado tunaamini kiongozi huyu anaishi. Kazi zake alizofanya zinaishi, Taifa alilojenga linaishi na ataendelea kuishi nasi.
  “Ndiyo maana sisi bado tunampenda, tunamheshimu, tunamuenzi, na binafsi natambua kuwa Mwalimu ataendelea kuwa nguzo kubwa na imara ya Taifa letu. Sisi katika IPP tunatambua nafasi ya Mwalimu katika Taifa letu, ndiyo maana ITV bila kuchoka imekuwa inarusha vipindi vinavyomhusu Mwalimu kikiwapo kipindi cha WOSIA WA BABA WA TAIFA.


  “Tunafanya hivi ili kuwakumbusha Watanzania wenzetu na ulimwengu wote juu ya mafundisho ya Mwalimu. Ni mafundisho ya mchungaji mwema kwa kondoo wake.
  “Sote tunamjua Mwalimu kama mchungaji ambaye wakati wote aliishi akitetea maslahi ya kondoo wake hakuwahi kuweka maslahi yake binafsi mbele. Tunakumbuka kwamba katika juhudi za kujenga Taifa huru lenye usawa na haki, Mwalimu alitaifisha kampuni binafsi, hakika hakufanya vile ili kujinufaisha yeye, au ili kujilimbikizia mali, ila alifanya hivyo ili kila Mtanzania anufaike na uchumi wa Taifa lake. Hiki ni kielelezo cha juu kabisa cha kiongozi aliyeukana ubinafsi kwa matendo halisi. Mwalimu hakuwa mbinafsi.
 “Mwalimu alikuwa taa ya matumaini kwa wanyonge, aliheshimika na kuenziwa si tu ndani ya Tanzania na ndani ya Bara la Afrika, bali duniani kote. Ndiyo maana ukiwa nje ya Tanzania ni fahari kubwa kujitambulisha kuwa unatoka nchi ya Nyerere kuliko hata kusema unatoka Tanzania. Hii yote ni kwa kuwa sifa na hadhi ya Mwalimu katika kupigania haki na usawa ilivuka mipaka ya Tanzania na kuwa kiongozi mpigania haki dunia kote.


  “Sisi wenzenu katika IPP kwa uwezo wetu mdogo tunajitahidi kufuata nyayo za Mwalimu. Kila wakati Mungu anapotujaalia nguvu na uwezo tunajibidisha sana kujali jamii na kuwasaidia katika mambo mbalimbali ikiwamo misiba, maafa, shughuli za maenedeleo n.k.
 "Ni rai yangu leo kwamba kama kila Mtanzania atamuenzi Mwalimu katika kusaidiana, katika kutatua kero za jamii, katika kufuata maadili, katika kujitoa kwa ajili ya wengine kwa moyo mkunjufu, hakika amani na utulivu wa Taifa letu utaendelea kudumu vizazi na vizazi.
  “Natambua kuwa kaka yangu, marehemu Elitira Mengi na marehemu Chifu Edward Wanzagi Nyerere, walikuwa marafiki wakubwa. Hawa walikuwa na uhusiano wa kindugu, marafiki hao nao walitimiza wajibu wao kwa jamii. Yatupasa pia kuiga mazuri waliyotenda kwa jamii. Tunamuomba Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amen.
 "Nawashukuru sana na asanteni sana kwa kunisikiliza.”
 
Ujumbe wa Chifu Japhet Wanzagi
 
Chifu Japhet aliwashukuru wana ukoo na wageni waalikwa.
Akasema: “Ukoo wa Burito una historia inayotambulika katika ulimwengu wa wapenda umoja, mshikamano, amani na utulivu. Misingi hii madhubuti iliasisiwa na Chifu Nyerere Burito na ikarithiwa na Chifu Edward Wanzagi Nyerere na hatimaye ikashamiri nchi nzima chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
 “Ili amani ya Taifa letu iweze kustawi, hatuna budi kuhakikisha familia na koo mbalimbali, katika ngazi zao, zinaanza kujenga umoja, mshikamano na upendo miongoni mwao kwanza. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, sisi Ukoo wa Burito; kama sehemu ya Taifa hili, tumeonelea vema kila mwaka tuwe na mkusanyiko wa aina hii unaolenga kutathmini na kuona namna ya kuendelea na kuzilinda tunu hizi za amani.
 “Ukoo wetu wenye watu zaidi ya 1,600 hauwezi kukosa changamoto. Hata hivyo,  kupitia vikao mbalimbali vya ukoo tumeweza kukabiliana na changamoto hizo, ikiwamo ya nidhamu na kujenga upendo na mshikamano.


  “Kwa kuwa suala hili limekuwa utamaduni ndani ya ukoo wetu tangu zama za Chifu Nyerere, sisi kama wana ukoo huu tumeona tuna wajibu wa kuwakumbusha wananchi na viongozi wetu wa Tanzania umuhimu wa kudumisha amani, upendo, mshikamano na umoja. Imani yetu ni kwamba bila kuzienzi kwa vitendo tunu hizi, Taifa letu lenye makabila zaidi ya 120 litasambaratika. Vurugu na chuki zinazosababisha maafa makubwa ya watu katika mataifa mbalimbali vinatosha kutuonya Watanzania kuacha kabisa kuchezea amani yetu.
  “Katika siku za karibuni kumekuwapo viashiria kadhaa hatari vya uvunjifu wa amani katika Taifa letu. Mauaji ya albino, mauaji ya kina mama, na mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina ni viashiria vya kutoweka kwa amani ya Taifa letu.


  “Ukoo wa Burito tunalaani vikali mauaji haya ambayo ni kinyume kabisa na mapenzi ya Mungu. Watanzania watambue kuwa utajiri au maisha bora vinapatikana kwa kufanya kazi halali kwa juhudi, maarifa na kwa kumtanguliza Mungu mbele. Viungo vya binadamu haviwezi kumfanya mtu kuwa tajiri. Ni wajibu wa vyombo vya dola, viongozi wa dini, asasi za kiraia na zisizo za kiraia, wananchi na wapenda amani wote kuungana kukomesha matukio haya ambayo licha ya kuwa ni dhambi, pia yanachafua mno sifa nzuri ya Taifa letu. Ulimwengu unatushangaa kwa dhambi hii.
  “Mwaka huu wa 2015 ni mwaka mwingine wa Uchaguzi Mkuu. Ni mwaka ambao unaweza kuifanya Tanzania iendelee kung’ara au unaweza kuifanya sifa ya nchi yetu ya amani na utulivu kuwa shakani. Uchaguzi Mkuu unakusudiwa kutanguliwa na kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa. Haya mambo mawili ni makubwa. Tunatoa wito kwa mamlaka husika kuona namna ya kufanikisha mambo haya bila kuliingiza Taifa kwenye mivutano na vurugu. Yale yanayowezekana kufanywa mwaka huu, yafanywe na yale yasiyowezekana ambayo si ya lazima kikatiba, yanaweza kupangiwa muda mwingine. 
  “Tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu huku Taifa letu likiwa linakabiliwa na vimelea hatari vya ukabila, ukanda, udini na tofauti kubwa ya kipato kati ya maskini na matajiri. Maadui wa ndani na nje wangependa kuona hatari hizi zikiendelea kukua na hatimaye kulivuruga Taifa letu.


  “Sisi Ukoo wa Burito tunatoa wito kwa Watanzania wote kuwa makini na maadui hawa wa ndani na nje ya nchi yetu. Tunawahimiza wawaepuke wanasiasa waliojiandaa kutwaa madaraka kwa vyovyote hata kama ni kwa njia haramu.   
 "Tunapinga na kulaani matumizi makubwa ya fedha katika kuwashawishi wapiga kura. Tunalaani kwa nguvu zote wanasiasa na wapambe wao wanaotaka viongozi wa Tanzania wapatikane kwa njia za ukabila au ukanda. Vyama vya siasa viwe makini na wagombea na wanachama wote wanaohubiri mgawanyiko kwa misingi ya kanda, kabila, jinsi, dini, rangi au hali ya mgombea.”