Meli tatu za kivita za Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China  zimewasili katika Bandari ya Dar es Salaam zikiwa na wanajeshi kadhaa kwa ajili ya kushiriki mazoezi ya pamoja na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ikiwa ni sehemu  maadhimisho miaka 60 ya Jeshi hilo na ushirikiano kati ya Nchi ya Tanzania na China tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza leo Julia 24, 2024 katika Bandari ya Dar es Salaam wakati akipokea Meli tatu za Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China, Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji Tanzania NAVY, Rear Admiral Ameir Ramadan Hassan, amesema kuwa  ujio wa meli hizo kutoka Jamhuri ya Watu wa China ni sehemu ya  kuadhimisha ushirikiano wa miaka 60 kati ya Tanzania na China.

Rear Admiral Ameir Ramadan Hassan amesema  kuwa wakiwa nchini  watashiriki mazoezi ya pamoja kati ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China  kwa ajili ya kudumisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na China ambapo tangu kuanzishwa kwake imefika miaka 60.

Amesema kuwa sio mara ya kwanza Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China kuja nchini Tanzania kufanya mazoezi ya pamoja na Jeshi la JWTZ kwani mwaka 2014, 2019, 2020 walikuja kushiriki mazoezi.

“Ujio wa Jeshi la Ukombozi Watu wa China tutajifunza mbinu mbalimbali kutokana  wao wameendelea zaidi katika masuala ya kijeshi” amesema.

Amesema kuwa mazoezi ya pamoja na Jeshi la Watu wa China watashiriki  vikundi mbalimbali vya Jeshi la Ulinzi la Tanzania, huku akifafanua kuwa  kupitia mazoezi hayo yatawasadia kuongeza uwezo wa kijeshi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Please follow and like us:
Pin Share