Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, amesema msimamo wa Waziri wa wizara hiyo wa kurejesha kitalu cha uwindaji wa kitalii kwa kampuni ya Green Miles Safaris Limited, ni sahihi, umezingatia sheria na hauwezi kutenguliwa.
Amesema kampuni ya Wengert Windrose inayong’ang’ania kitalu hicho kilichopo Pori Tengefu la Ziwa Natron (East), inajitahidi kuufanya mgogoro kuwa ni wa kimataifa, ilhali ukweli ukiwa kwamba Green Miles ndiyo walioshinda kisheria na kukabidhiwa kwa barua.
Pamoja na Wengert Windrose, kampuni nyingine zilizo chini ya Friedkin Conservation Fund ni Tanzania Game Trackers Safaris Limited na Mwiba Holdings Limited.
Kampuni hizo zina vitalu Ziwa Natron, Ranchi ya Mwiba, Makao WMA, Maswa Mbono na Maswa Kimali, Makere na Uvinza.
Katika mahojiano na JAMHURI, Meja Jenerali Milanzi amesema Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, na jopo la wataalamu baada ya kupitia rufani ya Green Miles kama sheria inavyoagiza, aliridhika kuwa Wengert siyo waliopewa kitalu hicho na Kamati ya Ushauri Ugawaji Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii.
Anasema kelele za Wengert zilianza baada ya uamuzi wa Serikali ambao kimsingi ulitokana na Bunge, wa kuongeza mapato kwa kugawa vitalu.
“Awali Wengert walikuwa wana eneo lote, kwa hiyo lilipogawanywa bado wakataka wapewe vitalu vyote. Lakini ujue hapo kulikuwa na Kamati ya Ushauri Ugawaji Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii ambayo haiingiliwi. Ilipitia maombi na mshindi akawa Green Miles. Ijulikane kuwa tangu awali hawa Wengert walikuwa wanapinga ugawaji – hawawezi kupinga uamuzi wa Bunge ambao ulikuwa unatekelezwa na Serikali. Picha wanayotoa sasa kwa jumuiya ya kimataifa si nzuri kwa sababu imejaa upotoshaji.
“Tumeshajua kuna mpango wa kulifanya jambo hili la kitaifa au kimataifa. Nataka kukuhakikishia kuwa uhusiano wa Tanzania na Marekani kwenye sekta ya Maliasili na Utalii ni mkubwa. Wengert ni sehemu ndogo sana ya uhusiano, na hatujui walimpa taarifa gani balozi wao za kumpotosha kwa sababu wao wenyewe wanajua si wenye kitalu wanachong’ang’ania,” amesema.
Anasema Serikali ya Tanzania inaendelea kushirikiana vizuri kwenye mapambano dhidi ya ujangili, na hiyo inathibitisha kuwa hili si suala la kusababisha mjadala mrefu.
Meja Jenerali Milanzi anasema wakati wa kupeleka maombi ya vitalu, Wengert waliomba vitalu viwili – North South na North. Green Miles waliomba kimoja tu (North) ambacho kilibadilishwa jina la kuitwa East. Rekodi za Wengert za malipo ya awali zinaonesha walilipia dola 30,000 za Marekani kwa kitalu walichopewa cha North South ambacho ni cha daraja la pili. Sasa wanaibuka na kusema wanalipia kitalu cha East cha daraja la kwanza kwa dola 60,000.
“Kumbukumbu zote za haya mambo zipo wizarani. Tunataka kujua imekuwaje maofisa wetu wanaohusika na malipo wameweza kukubali malipo ya kitalu kwa kampuni ambayo si yenye hicho kitalu na kwa daraja ambalo ni tofauti na lile walilolipia mwanzo kabisa,” amesema.
Amethibitisha kuwa ni upotoshaji kudai kuwa kampuni ya Green Miles Safaris inamilikiwa na raia wa kigeni. Amesema kampuni hiyo inamilikiwa kwa asilimia 52 na Watanzania.
“Nataka nikuhakikishie kuwa msimamo wa wizara ni kama ulivyotolewa na Mheshimiwa Waziri (Profesa Maghembe) bungeni.
“Nao ni kuhakikisha kitalu kinarudishwa kwa Green Miles (jambo lililokwishafanyika) na kuwataka Wengert kuondoka. Wengert hawakuridhika, wakaenda mahakamani kupinga uamuzi wa waziri, Mahakama ikatupilia mbali. Tunataka Wengert wafuate na waheshimu sheria za nchi. Waondoke, matarajio yetu ni kuwa wataheshimu sheria,” amesema Meja Jenerali Milanzi.
Kurejeshewa leseni
Meja Jenerali Milanzi ameeleza kushangazwa kwake na juhudi zinazofanywa za kupinga kurejeshwa kwa leseni ya Green Miles ambayo ilifutwa na uongozi wa wizara uliopita.
Anasema sheria inampa mamlaka waziri mwenye dhamana kupitia rufaa na kuona kama kuna sababu za kufungiwa leseni au la!
“Kimsingi kile kitendo kilichofanywa (cha kuua wanyama) bila kuzingatia sheria tunakilaani. Serikali imekubali wahusika walifanya makosa.
“Violation ya sheria haikubaliki tukafanya legal opinion review.
“Msimamo wa waziri na wizara kwa jumla ikawa kwamba hili suala lazima lifike mwisho – uamuzi ufikiwe.
“Kwenye Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 waziri hapewi mamlaka ya kunyang’anya leseni kwa kuamua isipokuwa kwa Mahakama. Lazima uoneshe unamshitaki nani, nani amekosa? Je, ni kosa la PH (mwindaji bingwa) au ni askari wanyamapori.
“Kamati maalumu ikaundwa, waliohusika wakajulikana. PH na askari wanyamapori wanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria na watashitakiwa.
“Kwa wale wageni waliofanya vitendo vya kuua wanyama kinyume cha sheria hawaruhusiwi kuja kuwinda tena nchini,” amesema Meja Jenerali Milanzi.