Mbunge wa Arumeru Magharibi, Gooluck ole Medeye (CCM), ameibuka na kuanika siri ya migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.
Ole Medeye ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mkazi, akikagua ujenzi wa barabara Arumeru Magharibi hivi karibuni, amesema migogoro ya ardhi inatokana na kuwapo kwa mashamba makubwa ya wakulima yaliyogawiwa wakati wa ukoloni.
“Tangu wakati wa ukoloni mashamba haya makubwa yamekuwa yakitembea kwenye mikono yao, hata kama mmiliki wa kwanza akiondoka anamwachia ndugu yake au rafiki. Sehemu kubwa ya ardhi imeshikwa na hawa wanaoitwa wakulima wakubwa,” amesema.
Medeye anabainisha kwamba pamoja na kumiliki mashamba hayo makubwa, bado baadhi yao kwa sasa hawayaendelezi.
Tayari wameanza kufanya upembuzi wa kuwabaini wote ambao hawayaendelezi kisha waweke utaratibu wa kuyachukua na kuyagawa kwa watumiaji wengine, wakiwamo wananchi wa kawaida.
Akitolea mfano wa uhaba wa maeneo hususani kwa taasisi kama za shule, Medeye anasema kwamba shule nyingi wilayani humo zimejengwa maeneo ya hekari moja au mbili. Kwa kawaida shule hupaswa kujengwa kwenye eneo la ukubwa wa hekari saba hadi 10.
“Inabidi sasa tutafute ardhi ya kuwafidia wananchi wanaoishi jirani na shule ili tupanue maeneo ya shule. Hakuna eneo jingine zaidi ya hayo mashamba makubwa.
“Hatusemi tutachukua kila shamba hapana, tutachukua yale yaliyotelekezwa,” anasema Ole Medeye.
Anataja chanzo cha pili kinachosababisha mgogoro wa ardhi kuwa, ni historia ya mji wa Arusha na maeneo yanayouzunguka. Kwamba wakati wa utawala wa Wajerumani baadhi ya wananchi walihamishwa kwenye maboma yao yaliyokuwa katika ya mji wa mji.
“Mimi pia boma letu lilikuwa katikati ya mji wa Arusha na tulihamishwa na hatukupewa ardhi.
“Tuliambiwa ondokeni hapa na ndiyo maana wananchi wengi wenyeji wa Arusha wanaishi maeneo ya milimani, kwani ndiko walikokimbilia baada ya kufukuzwa na Wajerumani.
“Hivi sasa tumeongezeka kwa idadi lakini baya zaidi kuna watu wengine wameuza ardhi kwa matumaini ya kwenda wilayani Kilindi na Handeni,” anasema.
Pamoja na wananchi hao kukimbilia katika wilaya hizo, bado wamekosa ardhi kama walivyotarajia na badala yake baadhi yao hivi sasa wameanza kurejea tena Arumeru, mahali ambapo tayari walishauza ardhi.
“Naomba nitoe mwito kwa wananchi kuacha mara moja kuuza ardhi kidogo waliyonayo, kwani vizazi vijavyo vinahitaji ardhi iliyopo leo.
“Mfano maeneo ya Keranyi na maeneo mengine leo hii ukienda hawana mahali pa kuzikwa wanapofariki dunia.
“Sisi tumezoea kuzikana nyumbani, hivi sasa hatuna hata makaburi na hatujajenga makaburi, kwa hiyo inabidi upelekwe makaburi ya Manispaa,” anaongeza.
Kuhusu barabara zinazojengwa, Medeye anasema matarajio yake hayajakamilika kwani amepanga kuona hadi kipindi anapokabidhi jimbo kwa wananchi, barabara zote na ahadi nyingine ziwe zimekamilika.