Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya limashikiliwa Koplo Marwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Suguta Chacha akiwa chini ya Ulinzi.

Akielezea chanzo cha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amesema kuwa, kulitokea mabishano kati ya marehemu na askari huyo ambapo walikuwa wakijibizana kilugha, hali iliyopelekea baadhi ya askari kutokuelewa kilichokuwa kikizungumza, ndipo askari huyo alipochomoa kisu na kumchoma mtuhumiwa sehemu ya mgongoni.

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, gari liligeuzwa kwa ajili ya kumuwahisha hospitali lakini alifariki dunia.

Mapema leo asubuhi, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche ambaye ni kaka wa marehemu alitoa taarifa na kueleza kuwa, mdogo wake alikamatwa jana usiku na ameuawa na polisi kwa kuchomwa kisu.

Baba mdogo wa marehemu, Wegesa Suguta amesema tukio hilo lilitokea jana saa tano usiku katika eneo la Sirari mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Alisema usiku wa jana Chacha alikuwa akinywa pombe katika baa ya Casablanka ndipo polisi walipofika kwa ajili ya kukagua usalama na kuamuru baada ifungwe kutokana na muda ulikuwa umekwisha. Baada ya hapo, walimuweka chini ya ulinzi Chacha na meneja wa baa hiyo na kisha kuondoka nao kwenda kituoni.

Amesema, hawajui hapo katikati nini kilitokea, lakini walipofika kituo cha polisi leo asubuhi ndipo walipopewa taarifa za ndugu yao kufariki dunia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema kuwa, yeyote aliyehusika katika tukio hilo atachukuliwa hatua, kwani hakuna mtu aliyeko juu ya sheria.

Aidha, amesisitiza kuwa, hata kama ingekuwa ni yeye, sheria ingefuata mkondo wake kwani naye yupo chini ya sheria. Ameitaka familia ya Chacha kuwa na subira wakati suala hilo likishughulikiwa.