Hali imezidi kuwa tete katika Chama cha Walimu Tanzania (CWT), baada ya baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutiliwa shaka na baadhi ya wanachama, JAMHURI limebaini.
Gazeti hili la JAMHURI limejiridhisha kuhusu kuwapo kwa mpasuko miongoni mwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, Katibu wa Bodi hiyo akipingana na wenzake kwa tuhuma kuwa wamekuwa wakilinda ‘uchafu’ unaokizonga chama hicho.
Mmoja wa wajumbe kutokana na hilo, amechukua hatua kadhaa ikiwamo kumtaka Kabidhi Wasii Mkuu kuzishikilia mali za CWT kwa niaba ya wanachama ili ufujaji wa mali hizo ufikie tamati.
Wakati Katibu wa Bodi ya Wadhamini, Hellen Mbezi, akichukua hatua hizo kunusuru mali za wanachama wa CWT, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Clement Mswanyama, anapinga madai hayo kwa kusema kuwa hakuna ufujaji, mali zote ziko salama.
Kauli hiyo inapingana na matokeo ya uchunguzi wa Kamati Maalumu ya CWT na uchunguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ombi la kushikilia mali
Kupitia barua ya Desemba 3, 2018 kwenda kwa Kabidhi Wasii Mkuu, Hellen Mbezi, ambaye ndiye Katibu wa Bodi ya Wadhamini, alitaka mali za Chama cha Walimu zishikiliwe na ofisi hiyo ya Kabidhi Wasii.
“Ombi hili la haraka limetokana na kushindwa kwa CWT kusimamia utekelezaji wa taarifa za kamati mbili zilizoundwa na Chama cha Walimu Tanzania, 2015, na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa agizo la Rais Dk. John Magufuli 2017, na kusomwa bungeni Januari, 2018,
“Hatua hii itasaidia kukinusuru chama. Utekelezaji huu uende sambamba na akaunti za chama, na zile zilizowekwa fedha za mitaji wa Benki ya Walimu tangu za mwaka 2012 hadi 2015 ambazo ni BOA Bank, ABC Bank na Azania ili (Kabidhi Wasii) ujiridhishe kama zimefungwa au la.
“Pia Katibu Mkuu wa CWT awasilishe mikataba yote anayotunza kwa niaba ya wadhamini, zikiwemo hati za majengo na viwanja nchi nzima (original). Pia kujiridhisha na uhalali wa kampuni inayokusanya kodi kwa jengo la walimu tangu mwaka 2011, TDCL, ikiwemo GMCO, kwa kuwa imebainika tume zote TDCL si ya walimu kisheria, hivyo kufanya Benki ya Walimu (MCB) kusajiliwa katika Kampuni ya TDCL na ambayo si ya walimu kisheria nayo uishikilie hadi utakapopatikana ufumbuzi wa ksheria. Utakapomwomba Katibu Mkuu mikataba akupatie pia na ya kampuni tangu 2011 mpaka 2018 zikiwemo taarifa za fedha,” inaeleza barua hiyo ambayo nakala imetumwa kwa Rais Dk. John Magufuli.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Clement Mswanyama, ameliambia JAMHURI: “Haya mambo hayana ukweli, yametungwa. Mali za walimu ziko salama kabisa. Kuhusu TDCL tulianzisha kwa kutumia wakurugenzi wa muda, vikao rasmi vilipendekeza majina. MEMAT (katiba ya kampuni) inasema kampuni inaendeshwa na wanahisa. Bodi ya wadhamini inamiliki hisa 99 kwa niaba ya wanachama wote. Katibu Mkuu anamiliki hisa asilimia moja,” amesema mwenyekiti huyo huku baadhi ya nyaraka zikionyesha kuwa hisa zinazopaswa kumilikiwa na katibu wa CWT kwa wadhifa huo zilikuwa zimeandikishwa kwa jina la mhusika tu na si wadhifa wake, kwa hiyo hisa hizo zilikuwa mali ya mwenye jina hilo na si wadhifa ambao hushikiliwa na yeyote kila baada ya mabadiliko ya uongozi wa kitaifa kwenye chama hicho.
Mwenyekiti huyo aliendelea kulieleza JAMHURI: “Waliotumika mwanzo wamekwisha kujiondoa, akiwamo Magreth Sitta, Juma Abdallah, Yahya Msulwa. Hata Justinian Rwehumbiza amekwisha kujiondoa, na anasema kuna watu wanamshawishi asijiondoe kwa kuwa kampuni iliyofunguliwa ni yake na mwenzake, kwa hiyo lazima kwanza alipwe shilingi bilioni moja. Tunajua kuna mwenzetu ndiye anayechochea haya mambo,” amesema Mswanyama bila kumtaja huyo mwenzao anayedhani anachochea mtafaruku huo wa usalama wa mali za wanachama wa CWT.
Mkono wa Ikulu
Gazeti hili limebaini kuwa baada ya walimu wa Shule ya Sekondari Jangwani ambako ni tawi la CWT kuandika barua Ikulu kueleza malalamiko yao, Ikulu kupitia barua yake ya Desemba 29, 2016 yenye kumbukumbu namba CAB 38/577/01F/6 ilitoa maelekezo kwenda kwa Katibu Mkuu (Kazi) Ofisi ya Waziri Mkuu, ikihusu vyama vya wafanyakazi kujihusisha katika biashara.
Sehemu ya barua hiyo ilieleza: “Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Shule ya Sekondari Jangwani wamewasilisha malalamiko yao RITA wakitaka ufafanuzi kuhusu umiliki wa mali za chama hicho.
“Sambamba na malalamiko hayo, wanachama hao wameishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuifanyia marekebisho sheria inayohusu vyama vya wafanyakazi ili kuvizuia vyama hivyo kufanya biashara na kuvifanya vibaki na jukumu moja tu la kutetea masilahi ya wafanyakazi.
“Kutokana na kuwepo kwa uwezekano wa uwekezaji wa kibiashara unaofanywa na vyama vya wafanyakazi kuwa chanzo cha migogoro na kuathiri malengo ya kuanzishwa kwa vyama hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi ameelekeza ufanyie kazi ushauri huo,” inaeleza barua hiyo iliyosainiwa na Dk. James Kilabuko, kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Gazeti la JAMHURI tangu wiki mbili zilizopita limekuwa likiandika habari kuhusu CWT. Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika kuwa majengo, Kampuni ya walimu ya TDCL, Benki ya Mwalimu si mali ya walimu kama ilivyokuwa ikidhaniwa na hali hiyo ni kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na vyombo viwili huru; ambavyo ni Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati Maalumu ya Kuchunguza ya Kampuni ya Maendeleo ya Mwalimu (TDCL) iliyoanzishwa Aprili 4, 2003.
Uchunguzi huo ulibainisha kuwa kampuni hiyo kwa mujibu wa Katiba yake (MEMART) ilipaswa kuwa na mtaji wa Sh milioni 10, zilizogawanywa kwenye hisa moja moja yenye thamani ya Sh 100,000 kila moja.
“Kinachosikitisha zaidi ni kuwa hao waliohisi wana mali nao hawakujali sana kusimamia kampuni hii na ndiyo maana hawakuona umuhimu wa aina yoyote ya kufuatilia ama kuisimamia kwa karibu kampuni hii.
“Kibaya zaidi Chama cha Walimu kilijenga jengo kwa gharama ya shilingi 5,943,000,000.00 na kutolikabidhi kwa TDCL (kisheria),” inasema sehemu ya taarifa ya kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe Hamisi Lissu (Mwenyekiti), Nuru B. E. Shenkalwa (Katibu), Amina Kisenge (Mjumbe), Abubakar Allawi (Mjumbe) na Moses Mnyazi (Mjumbe aliyejitoa).
Uchunguzi unaonyesha kuwa pamoja na TDCL ambayo ni kampuni ya walimu iliyoanzishwa mahususi kuendesha miradi ya walimu, bado kampuni hii iliingia mkataba na Kampuni ya GIMCO Africa inayoendesha jengo la Kitegauchumi cha Mwalimu, lililopo Ilala, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, wamiliki wa TDCL waliosajiliwa na Msajili wa Makampuni ni Justinian Rwehumbiza anayemiliki asilimia 50 ya hisa alizozilipia mtaji wa Sh milioni 5, na (marehemu) Juma Abdallah anayemiliki hisa 1, aliyoilipia Sh 100,000 kama mtaji.
“Katika vikao vyote vya chama na viongozi waliaminishwa na hata bodi zote zilizopita kuwa Kampuni ya Maendeleo ya Walimu ni ya wanachama wa Chama cha Walimu ambapo Katibu Mkuu ana hisa (01) na Chama cha Walimu kina hisa 99.
“Baada ya kuteuliwa Bodi mwaka 2014 nayo Bodi ilituaminisha kuwa chama kina hisa 70 na Katibu Mkuu ana hisa (01). Kwa mujibu wa Katiba ya kampuni na kanuni zake kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni Na. 12 ya Mwaka 2002 maelezo yote hayo hayakuwa sahihi.
“Tume hii mpaka imeundwa, kampuni iko chini ya umiliki wa wanahisa wawili ambao ni Justinian Rwehumbiza na Juma Abdallah na Katibu wa Kampuni ni Ndugu Riyaz Takin ambaye hakuna kiongozi hata mmoja anayemfahamu.
“Katika uchunguzi tulibaini kuwa hakuna mahali popote katika Katiba ya kampuni inatamka kukitambua Chama cha Walimu na tulishindwa kubaini kwa nini wanahisa hawaendeshi kampuni yao au kuna jambo wanalisubiria ndipo waje kuiendesha kampuni yao,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ya uchunguzi uliofanywa na CWT.
Umiliki wa Kampuni hii ya Maendeleo ya Walimu unaonyesha mkanganyiko mkubwa wa umiliki. Wakati Brela ikionekana wamiliki ni Rwehumbiza na Abdallah, Taarifa ya Mwaka 2005 ya TDCL inaonyesha wanahisa wafuatao:-
“Justinian Rwehumbiza hisa (50), Magreth Sitta (10), Yahaya Msulwa (10) na Juma Abdallah hisa (1). Na katika certificate ambayo chama (CWT) kilipewa na TIC inaonekana kuwa wanahisa wa TDCL ni registered trustees wa Chama cha Walimu wenye hisa (50) na wengine wanabaki, isipokuwa Justinian Rwehumbiza ambaye ametolewa katika certificate hiyo,” inasema sehemu ya taarifa ya uchunguzi.
Hapo katikati taarifa zilipoanza kuvuja kuwa TDCL si mali ya CWT, viongozi wajanja wamekwenda Brela kujaribu kubadili umiliki wa kampuni kutoka TDCL, ila wamekwama kutokana na hofu ya uongozi wa Rais Magufuli.
Akiwa jijini Dodoma katika mkutano wa CWT, Desemba, 2017 Rais John Magufuli aliwaambia miradi mingi ya CWT ni hewa, kwani hata Benki ya Mwalimu (MCB) ni mali ya watu wengine wasio walimu, suala lililothibitika kutokana na muundo wa umiliki wa MCB. Inamilikiwa na TDCL na wanahisa wengine.
Ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, umeonyesha matatizo sawa na yaliyobainishwa na tume iliyoundwa na walimu.
Hata hivyo, taarifa zilizolifikia JAMHURI zinaonyesha kuna vita kubwa inaendelea ndani ya CWT. Taarifa zinaonyesha Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif, anapambana kufumua mifumo ya ulaji iliyoota mizizi ndani ya CWT na sasa wahafidhina hawapendi.
“Mkutano mkuu unaitishwa si kwa nia njema, bali kufanya mapinduzi. Deus amekata mafungu hewa waliyokuwa wanapokea hawa wakubwa. Watu walikuwa wanapokea Sh milioni 20, hadi 50 kutoka CWT bila kuzifanyia kazi, sasa ameziba hii.
“Kuna wilaya zilikuwa zinaonyesha wanastaafu walimu 44 kila mwezi, zinapata mabati 20 kwa kila mwalimu anayestaafu kumbe ilikuwa hewa. Kwa sasa mwalimu akistaafu fedha zinawekwa kwenye akaunti yake. Idadi imepungua hadi walimu wanne kwa mwezi, ina maana 40 walikuwa hewa, hawa hawapendi… matatizo yapo, ila wanaojifanya kumpinga Deus ndio walioyatengeneza na ni wanufaika,” amesema mmoja wa viongozi wa CWT.
Kamati Maalumu ya Walimu tayari imekusanya saini za wajumbe 700 kati ya 1,200 wa mkutano mkuu na wanataka mkutano mkuu wa kurekebisha Katiba ya CWT ufanyike kabla ya mwisho wa mwaka huu ilivyoelekezwa na Mkutano Mkuu mwaka 2017, badala ya 2022 kama alivyoelekeza Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi.