Wiki mbili zilizopita nilipata fursa ya kwenda katika mikoa ya Tabora na Kigoma, kwa ajili ya kufundisha waandishi wa habari Azimio la Dar es Salaam juu ya Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji.
Azimio hili linaeleza haki na wajibu wa wadau mbalimbali wa vyombo vya habari. Linaeleza pia wajibu wa wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri, waandishi, serikali, watangazaji, wahisani na wengine wawao.
Lengo la msingi la azimio hili ni kuijengea jamii ya Tanzania maadili na uwajibikaji kwa jamii. Mkondo na mtazamo wa Azimio hili ni kulifanya taifa letu kurejea katika misingi ya maadili. Familia au taifa linapokosa maadili unakuwa mwanzo wa mmomonyoko wa umoja, amani, upendo na mshikamano. Siku zote tunapaswa kutanguliza maadili kabla ya sheria.
Baraza la Habari Tanzania (MCT) wameandaa tamko hili kwa nia ya kurahisisha utendaji ndani ya vyombo vya habari na kuwahisha maendeleo ya taifa hili. Jamii isiyo na habari za uhakika inakuwa sawa na jamii iliyopotea njia. Hatuwezi kuwa na habari za uhakika pale watoa habari wanapoficha habari.
Hatuwezi kuwa na habari za uhakika pale watangazaji kwa kutumia nguvu ya matangazo wanapozuia habari zenye umuhimu kwa taifa na kushadidia biashara zao kama kampuni za simu, ambazo kimsingi mbali na kuwezesha wananchi, lengo la msingi la kampuni hizo ni kuvuna hata kidogo walichonacho wananchi.
Utakumbuka kuwa kampuni nyingi baada ya kuwa zimetunyonya vya kutosha, siku hizi wakibaini kuwa umeishiwa na fedha kwenye simu yako wanakushawishi kukukopesha. Hii inamaanisha kuwa wanafanya hivyo kwa nia ya kuendelea kuchukua hata kidogo unachotarajia kukipata katika siku za usoni.
Azimio hili linalenga kuwabana wamiliki na wanasiasa kutotenda dhambi ya kuvilisha vyombo vya habari maneno na kuvielekeza cha kuandika kwa masilahi binafsi. Kwamba kundi hili linatakiwa kuwaacha wahariri na waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru wa hali ya juu, na kutimiza malengo ya msingi ya kuanzishwa kwa vyombo vya habari ambayo ni kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha.
Wahariri na waandishi wa habari nao – kwa masilahi ya jamii – Azimio hili linawataka kujenga maadili ndani yao yenye kuwawezesha kufanya kazi kwa masilahi ya taifa badala ya tumbo binafsi. Azimio hili lililoandaliwa na jopo la wajuzi wakiongozwa na Profesa Issa Shivji, linalenga kujenga Tanzania iliyostaarabika, Tanzania yenye maendeleo ya kweli.
Maadili yakitangulia, sheria itafanya kazi bila tabu yoyote. Hii maana yake nini? Maana halisi ya hili ni sawa na mfano wa salamu katika familia. Hakuna sheria inayomlazimu mtoto kumwamkia baba au mama asubuhi au jioni na hakuna anayeweza kupelekwa mahakamani kwa kutofanya hivyo. Hata hivyo, kwa uzito wa maadili ulivyojengeka, haitarajiwi mtoto asiwasalimie wazazi wake au aamke na kuwaambia; Mambo?
Kimsingi, Azimio hili linalenga kulifikisha hapo taifa. Kuwafanya wadau wote wa habari waichukie rushwa, fitina, hiyana, uzabizabina na walenge kuchapisha habari zinazoleta maendeleo kwa jamii. Kwa nchi zilizoendelea, vyombo vya habari hutumika kama nguzo ya umoja wa kitaifa na kama chombo cha kufikia malengo ya kitaifa.
Baada ya maadili haya kufundishwa nchi nzima, hatutarajii waandishi wa habari wawe wakala wa kuligawa taifa letu kwa udini, umajimbo, ukabila, umikoa, rangi au vinginevyo. Tunatarajia iwe sehemu ya wanahabari kuwa jicho la kuzibana benki zinazotoa mikopo kwa upendeleo kwa ngozi isiyo nyeusi, ikiwa inafanyika hivyo na vyombo vyetu viwaeleze wananchi njia halali za kupata kipato.
Sitanii, ni kwa misingi hiyo, leo mimi naanza kutoa mfano. Nimesafiri kwa njia ya barabara kutoka Mwanza hadi Tabora-Kigoma kisha nikarejea kutoka Kigoma-Kibondo-Kakongo-Nyakanazi-Geita-Mwanza. Njiani yapo niliyojifunza. Kwanza niseme nimefurahishwa na umakini wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwasa. Mkuu huyu yuko ‘serious’.
Hapa leo sizungumzi siasa bali nazungumzia uhalisia. Mkoani Tabora pale stendi uchafu ulikuwa umekithiri. Alichofanya Mkuu wa Mkoa ni kuwaamsha majumbani kwao wote – iwe Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na wote wawao – akawapeleka kufagia barabara saa nne usiku. Hili lilikuwa fundisho tosha.
Baada ya fatiki hii, ndani ya siku mbili kila eneo la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora lilikuwa safi kuliko maelezo. Hapa nimejifunza kuwa nchi yetu mambo hayaendi si kwa sababu haiwezekani, bali kutokana na ukweli kwamba viongozi wetu walio wengi ni legelege na hawawajibiki ipasavyo. Wakuu wa mikoa wanayo mamlaka lakini hawayatumii. Sitanii,ni kweli kabisa mamlaka waliyo nayo hawayatumii ipasavyo.
Baada ya kutoka Tabora nilikwenda Kigoma kufanya kazi ile ile ya kufundisha Azimio hili la Dar es Salaam linalohamasisha maadili katika vyombo vya habari. Nikiwa njiani nilishuhudia fursa za ajabu. Nimesema leo siandiki siasa maana Watanzania wengi tuna ugonjwa wa siasa. Leo nazungumzia fursa zilizopo Kigoma.
Daraja la Mto Malagarasi linajengwa sasa. Kilomita chache kutoka kwenye daraja hilo, kuna Mgodi wa Chumvi wa Uvinza. Pale watu wanakinga maji, wanakausha na kupakia magunia na magunia ya chumvi kwenda kuuza ndani na nje ya nchi. Mgodi ule ni wa kudumu. Kina cha maji pale hakipungui daima milele na chumvi haipotezi ladha yake.
Ukifika Kigoma Mjini, sura ya mji imebadilika. Nilikuwa Kigoma kiasi cha miaka minne iliyopita, lakini zamu hii hali nimeikuta tofauti. Mji umetamalaki barabara za lami, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wamejenga majengo yanayoupa heshima ya pekee mji ule. Kwa sasa Kigoma ina sura ya pekee.
Nilibahatika kwenda hadi Ziwa Tanganyika nilikoshuhudia wavuvi wakiandaa karabai kwa ajili ya uvuvi wa dagaa. Kimsingi nimebaini kuwa biashara kuu za Mkoa wa Kigoma ni kama nne. Wanauza dagaa ndani na nje ya nchi, chumvi, mawese na ndizi kwa mamwinyi wa mashujaa wa Unyanyembe. Tabora sasa wamebakiza asali na kuangiza ndizi kutoka Bukoba na Kigoma.
Sitanii, kuna jambo nililojifunza. Bonde la Mto Malagarasi linaweza kuilisha nchi hii. Kuna uwanda mpana ambao tukiamua kulima mpunga au mahidi, basi tunaweza kulisha majirani zetu na tukapata fedha za kutosha za kigeni. Si tunawaona wenzetu Thailand na mchele wao? Thailand ndiyo “pona” ya mataifa mengi. Sisi nini kimeshindikana?
Najua ubaya wa barabara uliopo kati ya Nzega-Tabora-Kaliua-Nguruka-Kasulu-Ujiji, lakini kuna dalili kuwa barabara hiyo sasa inajengwa. Ingawa kasi haridhishi lakini kuna kila dalili kuwa barabara hii itakamilika. Naomba kuchukua fursa hii kuwahamasisha wananchi kuwa barabara hii ikitumika sambamba na reli, Tanzania itavuna fedha za kigeni hadi Mungu achukie.
Leo nilifikiri kuwa yatupasa kuhamasishana kama wananchi kufanya kazi, kwani maendeleo hayatatukuta nyumbani au mitaani kwenye maandamano. Kwa asiyeamini maneno yangu akasome kitambu cha “Songs of Lowino” kilichoandikwa na Okot p’Bitek. Atashuhudia wapigania uhuru walivyorejea kulalia maboksi.