Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya
Wananchi wenye hasira katika Kata ya Ilemi jijini Mbeya wamemuua kwa kumpiga hadi kufa, mchungaji Golden Ngumbuke (66) wa Kanisa la Pentecostal Evangelical Fellowship Africa (PEFA), wakimtuhumu kuhusika na kifo cha jirani yake, Katekista Fadhili Komba (32) wa Kigango cha Mwansekwa, Parokia ya Mwanjelwa, Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.
Tukio hilo lilitokea juzi nje ya nyumba ya mchungaji Ngumbuke iliyopo katika Mtaa wa Mwafute, ambapo kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi walimshambulia na kusababisha kifo chake.
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limethibitisha tukio hilo na kusema watu wanne wanashikiliwa.
Mwili wa mchungaji ulizikwa jana katika Kijiji cha Lupeta, Kata ya Swaya, Wilaya ya Mbeya.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Ilemi, Herman Mbaga, alisema chanzo cha mgogoro kilianzia kwenye mzozo wa mpaka kati ya Mchungaji Ngumbuke na Katekista Komba, ambao ulifikia hatua ya vurugu baada ya Katekista kudaiwa kumpiga mke wa mchungaji.
“Uongozi wa mtaa uliitisha mkutano wa hadhara ili kujadili mgogoro huo. Baada ya kusikiliza pande zote, ilionekana Mchungaji Ngumbuke ameshindwa katika kesi hiyo. Inadaiwa alimtamkia Katekista kuwa yeye si mchungaji wa kawaida, na akamtaka aombe msamaha na kutoa sadaka, jambo ambalo Katekista alilitekeleza,” alieleza Mbaga.
Hata hivyo, siku chache baadaye, Katekista alianza kuumwa ugonjwa wa kuhara uliodumu tangu Desemba mwaka jana hadi Aprili 15, mwaka huu alipofariki dunia, hali iliyochochea tuhuma dhidi ya Mchungaji Ngumbuke kuhusishwa na kifo hicho kwa imani za kishirikina.
Mbaga aliongeza kuwa siku chache baada ya kifo cha Katekista, watu wasiojulikana walivunja vioo vya madirisha ya nyumba ya Mchungaji Ngumbuke na kumshambulia hadi kufariki dunia nje ya nyumba yake.
Kwa upande wake, Katibu wa Ulinzi wa Kata ya Ilemi, Tosha Nundu alisema mamlaka za mtaa zilimzuia mchungaji kurejea eneo hilo kutokana na taharuki iliyokuwepo, lakini alikaidi ushauri huo na kurejea kabla ya kutokea kwa tukio hilo la mauaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa watu wanne wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji hayo na kwamba uchunguzi unaendelea na taarifa kamili itatolewa baada ya kukamilika kwa upelelezi.
