Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA
Mchungaji mstaafu wa kanisa la Marekani ambaye aliongoza mazishi ya msichana wa miaka minane aliyetekwa nyara takriban nusu karne iliyopita nyara ameshtakiwa kwa mauaji yake.
Gretchen Harrington alitoweka katika kitongoji cha Philadelphia cha mji wa Marple asubuhi ya tarehe 15 Agosti 1975 alipokuwa akihudhuria kambi ya mafunzo ya Biblia ya msimu wa kiangazi.
Mapema mwaka huu, mwanamke ambaye jina lake halikujulikana aliwaambia wachunguzi kwamba aliamini kuwa baba yake rafiki yake mkubwa ndiye mhusika.
David Zandstra, 83, sasa anashtakiwa kwa mauaji na utekaji nyara wa mtoto mdogo.
“Yeye ndiye ndoto mbaya zaidi ya kila mzazi,” Wakili wa Wilaya ya Delaware Jack Stollsteimer aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu.
“Alimuua msichana huyu masikini mwenye umri wa miaka minane aliyemfahamu na ambaye alimwamini. Na kisha, akajifanya kama rafiki wa familia, sio tu wakati wa mazishi yake na kipindi cha baada ya hapo, lakini kwa miaka.”
Kuibuliwa kwa kesi hiyo kulitokana kwa sehemu moja na kitabu kilichochapishwa mwaka jana, kiitwacho Marple’s Gretchen Harrington Tragedy: Kidnapping, Murder and Innocence Lost in Suburban Philadelphia.
Mnamo 1975, Zandstra alikuwa mchungaji katika Kanisa la Trinity Christian Reformed. Kambi za mafundisho ya Biblia zilifanywa kwenye majengo yake kila asubuhi na kisha kuwasafirisha watoto hadi kwenye kanisa la pili.
Lakini Gretchen hakuwahi kufika katika Kanisa la Reformed Presbyterian, na ni Zandstra mwenyewe aliyeripoti kutoweka kwake kwa polisi asubuhi hiyo.
Mabaki ya mwili wake yalipatikana katika eneo la karibu la miti karibu miezi miwili baada ya kutoweka kwake.
Mshukiwa huyo ambaye alikuwa rafiki wa familia ya Harringtons, alisaidia kumtafuta na mtoto huyo na hata kusimamia kuongoza ibada ya mazishi, vyanzo viliiambia CBS News na kituo washirika wa BBC wa Marekani.