Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MCHEZAJI wa gofu wa kulipwa kutoka klabu ya Gymkhana Dar es Salaam, Fadhili Nkya ameibuka bingwa katika michuano ya Lina PG Tour yaliyofanyika katika viwanja vya gofu vya Gymkhana, Morogoro jana.

Michuano hiyo imeandaliwa na familia ya Nkya kwa kushirikiana na Chama cha cha Wanawake Tanzania (TLGU) imeshirikisha wachezaji wengi wa kulipwa na ridhaa kwa ajili ya kumuenzi Lina aliyefariki dunia Januari 19, 2021. Mchezaji huyo wa zamani alikuwa pia kiongozi wa TLGU.p

Ushindi huo umemfanya Fadhili kuondoka na zawadi ya kitita cha fedha kiasi cha Sh.Milioni 6.8 huku mshindi wa pili ambaye ni Frank Mwinuka wa Lugalo kuondoka na Sh.Milioni 4.3, mshindi wa tatu ni Abdallah Yusuph aliyepata Milioni 3.4, nafasi ya nne ikichukuliwa na Nuru Mollel aliyepata Milioni 2.7 na mshindi wa tano akiwa Hassan Kadio ambaye amepata Milioni 2.2.

Aidha kwa upande wa wachezaji wa ridhaa mshindi ni Enoshi Wanyeche kutoka klabu ya Lugalo Dar es Salaam ambaye ameondoka na kiasi cha Sh. Milioni 2.2 na nafasi ya pili ikichukuliwa na Isiaka Daud aliyepata Milioni 1.3.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Fadhili amesema mashindano yalikuwa magumu kwani wachezaji wote wa gofu wa kulipwa walijipanga vizuri lakini anamshukuru Mungu kwa kuibuka kidedea.

Amesema siri ya ushindi wake inatokana na kufanya mazoezi kila siku na kwamba anaendelea kujipanga ili aweza kushinda mashindano mengine yanayokuja baada ya masika kuisha.

“Mimi ni miongoni mwa wale ambao watakwenda kuliwakilisha Taifa katika mashindano makubwa nchini Dubai, nipo najiandaa ili kuweza kufanya vizuri katika michuano hiyo, hata hivyo tunaomba wadhamini wajitokeze kudhamini Lina PG Tour ili tuweze kupata mashindano mengi zaidi,” amesema Fadhili.

Kwa upande wake Wanyeche amesema mashindano ya Lina PG Tour ni mazuri kwani yamekuja kukuza vipaji na kuamsha mchezo wa gofu kwa ujumla kwani michuano imekuwa ni mengi kuliko huko awali.

“Tanzania tuna wachezaji wengi wa gofu wazuri lakini hawafahamiki kutokana na kukosa mashindano ya mara kwa mara lakini Lina PG Tour wamekuja kuamsha mashindano, tunaomba wadau wajitokeze kuwasapoti ili wachezaji wetu waweze kung’ara,” amesema Wanyeche

Naye Mwenyekiti wa mshindano hayo na Mkuu wa familia ya Nkya, Said Nkya amewaomba wadau hasa wadhamini kujitokeza kwa wingi kudhamini mashindano hayo ili kuwafanya wachezaji kupata michuano ya kutosha kwa lengo la kukuza ujuzi wao.

“Tunaziomba kampuni za Benki na sekta binafsi watupatie udhamini ili tuweze kukuza huu mchezo, pia tuwaombe wenye viwanja kuacha kutoa gharama kubwa wakati kwa wanaokuja kuomba michuano kufanyika katika viwanja vyao.

“Tunawaomba Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na serikali kwa ujumla watusaidie katika hili kuwaambia viongozi wa viwanja vya gofu kuacha kuzuia wachezaji wa Afrika kushiriki kufanya mazoezi na kuendesha mashindano, tunatakiwa kutafuta kwa pamoja mbinu za kukuza mchezo huu na siyo kuweka vikwazo,” amesema Nkya ambaye ni mume wa marehemu Lina.

Aidha Mzee Nkya amewashukuru wachezaji wote waliojitokeza katika mashindano hayo na kuwapongeza ambao hawakufanikiwa kushinda akiwahimiza wajitokeze katika mashindano mengine yatakayofanyika.

“Tunaishukuru pia klabu ya Gymkhana hapa Morogoro kwa kuturuhusu kufanyia mashindano haya katika viwanja vyao, nawashukuru timu nzima iliyoendesha mashindano haya ikiongozwa na binti yangu Yasmin Chali hakika tumefanikiwa,” amesema Said.