Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Maliasili na Utalii,Mohamed Mchengerwa (Mb) amesema Wizara yake imejipanga kuitangaza Tanzania duniani kwa kutumia mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na timu za mpira wa miguu za kimataifa ili kuvuka lengo la idadi ya watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025.
Amesema hayo leo wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kilichofanyika katika Ukumbi wa Utawala Annex, Bungeni jijini Dodoma.
“Tumejipanga kwenda kuitangaza nchi yetu kimataifa hasa kwenda kwenye maeneo ambayo wenzetu hawajafika mfano kuvitumia vilabu vya mpira wa miguu vya kimataifa ambavyo vina wanachama na mashabiki wengi katika historia ya mpira wa miguu duniani” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Kufuatia hatua hiyo,Mchengerwa amesema ili kuvuka lengo hilo Wizara inatarajia kufanya mabadiliko ya utendaji kazi kuanzia kwa Wakuu wa Taasisi mpaka kwa watumishi ambapo watendaji watapimwa pia ni kwa namna gani wameondoa migogoro kwenye Hifadhi na wananchi.
“Mabadiliko hayo yatashuka kila idara na kila eneo, ni lazima kila mtumishi abadilike katika utendaji kazi, kila mmoja kwenye idara yake afanye kazi ya kutafuta na kuongeza idadi ya watalii na yeyote atakayetuchelewesha tutamuweka pembeni” amesisitiza Mchengerwa.
Katika hatua nyingine,Mchengerwa amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya Hifadhi kwa kujenga barabara ambazo ni rafiki na shughuli za uhifadhi ambazo zitadumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) ameishukuru kamati hiyo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha maono ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yanatimia katika sekta ya utalii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Timotheo Mnzava amewataka watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha wanasimamia vizuri mifumo ya ukusanyaji wa mapato yatokanayo na utalii.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi amesema wako tayari kuleta mabadiliko makubwa katika Wizara hiyo na ameahidi kuyafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa kwenye kamati hiyo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji na baadhi ya Watumishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake.